Sunday, March 24, 2013

HESHIMA YAKO NI THAMANI KATIKA JAMII

Kila mmoja wetu anapenda kuishi maisha ya uadilifu na ya kuheshimika kwa jamii nzima inayomzunguka. Tunapoteleza kimaadili kwa bahati mbaya au makusudi bado tungependelea heshima yetu kwa jamii ibaki pale pale. Mwenyenzi Mungu ametubariki wanadamu kuwa na hekima na busara katika kufanya maamuzi ambayo yanasaidia kulinda heshima yetu. Ni vizuri kurekebishana kwa heshima pale tunapoona mmoja wetu anapotoka kimaadili ili heshima yake katika jamii ibakie vile vile au kuongezeka zaidi. Inaeleweka katika jamii wanadamu tunaweza kutofautina kimsimamo au kimaamuzi ila tujitahidi isifikie katika hatua ya kuondoleana heshima mbele ya jamii. Haimpendezi Mungu kabisa kuona kwamba mwanadamu anachangia kumwondolea mwanadamu mwenzake heshima yake katika jamii.

Mfano mzuri wa somo la leo tunaupata kutoka katika kitabu cha Mwanzo 9: 20-27 - “Nuhu akaanza kuwa mkulima, akapanda mizabibu; akanywa diva; akalewa; akawa uchi katika hema yake. Hamu, baba wa Kaanani, akauona uchi wa baba yake, akawaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje.  Shemu na Yafethi wakatwaa vazi, wakalitanda mabegani mwao wote wawili, wakaenda kinyumenyume, wakaufunika uchi wa baba yao, na nyuso zao zilielekea nyuma, na wala hawakuona uchi wa baba yao. Nuhu akalevuka katika ulevi wake, akajua mwana wake mdogo alivyomtendea. Akasema, Na alaaniwe Kaanani; Atakuwa mtumwa kabisa kwa ndugu zake. Akasema, Na atukuzwe BWANA Mungu wa Shemu; Na Kaanani awe mtumwa wake. Mungu akamnafisishe Yafethi. Na akae katika hema za Shemu; Na Kaanani awe mtumwa wake.”

Hivyo basi wapendwa, kitabu hiki cha Mwanzo kinatukumbusha ni jinsi gani mwanadamu anavyokwazika pale heshima yake katika jamii inapoondoka. HESHIMA yako katika jamii ndio inayokupa msukumo wa kufanya maamuzi ya busara na ya maendeleo kwako mwenyewe na kwa jamii nzima inayokuzuguka na zaidi kuwa na uhusiano mzuri na baba yetu wa mbinguni. Heshima hiyo ikiondoka, ni vigumu mno kufanya maazuri ya busara na mwisho uhusiano na Mungu wetu unavunjika. Tujitahidi kuwaheshimu wenzetu na vile vile kuwasaidia kurudisha heshima yao pale wanapopotoka bila kukusudia au kwa kukusudia. Hata itakapofikia suluhisho limeshindikana katika maamuzi au misimamo, bado tuna wajibu wa kutunziana heshima. Mwenyenzi Mungu aendelee kutubariki katika kufanya maamuzi ya hekima na busara ili heshima yetu katika jamii iendelee kuthaminika.

Mbarikiwe!

No comments:

Post a Comment