Monday, October 13, 2014

Neno la leo

Wafilipi 2:12 “Basi, wapendwa wangu kama vile mlivyotii sikuzote si wakati mimi nilipokuwa tu, bali sasa zaidi sana mimi nisipokuwapo, utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka”

TAFAKARI: Maandiko matakatifu yanatuasa kuutimiza wokovu wetu kwa kuogopa na kutetemeka. Tudumu katika neno lake na kuzitii amri zake ili tuweze kusimama imara katika imani yetu ya wokovu. Na zaidi tuepuke kulitumia neno la wokovu kwa kuficha mambo yetu mabaya. Katika kufanya haya yatupasa kujitwika msalaba wake na kuwa mfuasi wake na kufanya yale yampendezayo. Vile vile kutambua eneo lako kama mkristo ni lipi ambalo litakufanya utimize wokovu wako.


SALA: Bwana Yesu, tunakuja mbele zako kwa unyeyekevu kabisa tukiomba utujalie maskio ya kuskia na kudumu katika neno lako. Tuwezeshe kuutambua wokovu wetu na kuushika tusiterereke kamwe. Zaidi tusaidie kuwa mfano wa wafuasi wako tukiubeba msalaba wako kwa imani na ya kwamba ipo siku tutafurahia matunda ya wokovu wetu. Tunaomba hayo na kupokea, Amen.

Wednesday, September 4, 2013

Neno la Leo


Marko 11:25-26, Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. [Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.]

TAFAKARI: Kuna maombi mengi katika maisha ya wakristo hayajibiwi sio kwa sababu ya dhambi au shetani ana nguvu sana bali ni kwa sababu kuwa wengi hawajasemehe. Kuna wengi wetu tunaishi na vinyongo vya watu ndani mwetu, tuna mengi tumeyabeba na kuna uchungu wa mambo mengi ambao hatutaki kuachilia. Hii imepelekea maombi yetu kutojibiwa maana kutosamehe ni jambo mojawapo inayopelekea kutojibiwa maombi. Samahe leo hii.


SALA : Mungu wangu na Baba yangu, naomba unipe neema ya kusamehe na kuachilia katika maisha yangu. Nisadie nisamehe hata yale ambayo vidonda vyake bado vibichi mpaka leo ili na wewe upate kunisamehe. Kwa Jina la Yesu, Amina.

Wednesday, August 14, 2013

Neno la LeoEfe 5:33 “Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe”

TAFAKARI: Ndoa ni zawadi ya muhimu na inatoka kwa Mungu. Tumuombe Mungu aziangalie na kuzilinda ndoa zetu. Na zaidi atusaidie kuheshimu maamuzi ya kila mmoja wetu katika ndoa (Mme na mke).

SALA: Mwenyezi Mungu nasema asante kwa kunipa mme mzuri. Naomba umuongoze katika kunipenda na kunijali tunapofanya kazi pamoja kwa ajili ya maisha yetu ya baadae. Bwana, naomba kwamba siku zote tutegemee muongozo wako, na zaidi tufwate mfano wa upendo wako usio na kifani. Tunaomba utuonyeshe njia ambazo tunaweza kuinuana wenyewe kwa wenyewe hasa pale tunapokutumia wewe. Katika jina la Yesu naomba na kupokea, Amen.

Tuesday, July 30, 2013

Neno la leoYoh 14: 6-7 “Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia na kweli na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba; tangu sasa mnamjua, tena mmemwona”

TAFAKARI: Ni baraka kubwa kuweza kumuona Mungu. Kwa  kusoma neno lake tunapata picha ya sifa zake, uhalisia wake na upendo wake.

SALA: Mwenyezi Mungu, kila siku najitahidi kumjua Yesu Kristo kwa sababu natambua yeye ataniweka karibu nawe zaidi. Atanisogeza karibu na ukweli wa uumbaji wako na ukamilifu wako. Nimekuwa na nguvu kuliko kawaida kwa sababu nafwata hii kiu ya kukuelewa wewe na mwanao Yesu, Kristo. Naomba mapenzi yako yatimie katika haya yote, Amen.

Eee Bwana Niinue!!!


Monday, July 1, 2013

Neno la leo


Zab 119: 30 “Nimeichagua njia ya uaminifu, Na kuziweka hukumu zako mbele yangu”

TAFAKARI: Sio njia zote huwa zinapitika kwa maana nyingine zina miba ama vitu vingine vya hatari ambapo si rahisi kwa mwanadamu kupita. Hivyo basi, tumuombe Mungu atuonyeshe njia zile ambazo tunapaswa kupita.

SALA: Nashukuru sana nimegundua ukweli kwa wakati muafaka, kwa maana nilikuwa kila mahali na maswali ya hapa na pale. Bwana, wakati mwingine sikujua niulize maswali gani ili tu nikate kiu yangu ya kuelewa na kujitambua. Asante kwa kuwa umenitoa kwenye ujinga na kunionyesha nuru ya moyo wako, na hapo mambo yangu yalianza kwenda kama wewe ulivyopendezwa. Naomba uzidi kunionyesha njia Mungu wangu ili niingie kwenye mitego ya muovu shetani. Naomba hayo na kupokea katika jina la mwanao Yesu Kristo, Amen.

Monday, June 24, 2013

Neno la Leo


Mat 21:22 “Na yoyote mtakayoyaomba katika sala mkiamini, mtapokea”

TAFAKARI: Jambo la muhimu la kujiuliza hapa ni kwamba unaamini? Unaamini ya kwamba Bwana Mungu yupo na pindi tumuombapo kitu chochote hutupatia?

SALA: Bwana nakiri ya kwamba naamini uwepo wako na ninajua ya kuwa nikiomba unanijibu sawasawa na mapenzi yako. Hata pale ambapo ninatambulika kwa kukosa kujiamini, ninachoomba kutoka kwako ni muongozo, busara na amani katika mambo nifanyayo. Unaniongezea Imani Bwana, pale unapojibu sala zangu. Naomba mkono wako wa busara na hekima usinipungukie ninapoendelea kukutumaini wewe katika maisha yangu. Katika jina la Yesu Kristo naomba na kupokea, Amen.