Friday, April 19, 2013

Neno la leo

Zab 51:10 “Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu”

TAFAKARI: Kwa jinsi Mungu anavyotuandalia makao yetu basi nasi hatuna budi kuandaa mahali pazuri akae hapo. Tumuombe atengeneze mioyo yetu iwe tayari na safi yenye kumtukuza yeye. Iwe mioyo yenye kukaribisha uwepo wa Mungu
SALA: Bwana Mungu, nataka moyo ambao unang’ang’ania ahadi zako. Naomba nipe roho iliyotulia ambayo itashikilia neno lako ndani yangu na unifanye niwe sehemu ambayo ina thamani ya kuitwa nyumba yako. Kadri ninavyoendelea mbele, Bwana nitakufikiria wewe ushiye ndani yangu ya kwamba unanineemesha kwa chakula chenye kunijenga kiroho kila siku. Naomba na kupokea katika jina mwanao Yesu Kristo, Amen.

Thursday, April 18, 2013

Neno la leo

Mit 17:24 “Hekima huwa machoni pake mwenye ufahamu; Bali macho ya mpumbavu huwa katika ncha za dunia”

TAFAKARI: Kuna wakati mtu huwa na shauku juu ya mipango aliyopanga. Kutaka kujua labda ningefanya hivi itakuwaje, je nitafanikisha, ama nini matokeo yake? Mwisho wa mambo hayo hukosa mwelekeo hivyo kuenenda katika njia ambazo hakuzifikiria.
SALA: Bwana Mungu naomba nisaidie niweze kuweka hekima yako na kuitazama kwa macho yaliyo wazi. Mara nyingine napoteza mtazamo wangu juu ya kipi ni chema na kipi kibaya, lakini nimekutumaini wewe kwa kuwa najua utaniokoa. Naomba nishike mabega yangu na uniongoze Bwana katika njia nzuri. Katika jina la Yesu, naomba na kupokea, Amen.

Wednesday, April 17, 2013

Neno la leo

Zab 31:14 “Lakini mimi nakutumaini wewe, BWANA, Nimesema, wewe ndiwe Mungu wangu.

TAFAKARI: Tunapokiri kuwa Mungu wetu yupo basi tujaribu kufanya matendo yetu yaendane na kile tunachokiri. Tumuombe Mungu atusaidie kumkubali kwa nguvu bila kuona aibu.
SALA: Bwana Mungu, nataka midomo yangu ikuimbie wewe katika hali zozote, ziwe sherehe, misiba ama matatizo mengine, nataka mawazo yangu kwanza yawaze kukuimbia wewe na kukutukuza kwa sababu nakuamini wewe pekee katika maisha yangu. Naomba kila kitu nifanyacho kiwe ushuhuda wa kuamini kwangu. Nitasimama imara katika Imani niweze kutatua matatizo yangu. Naomba niwezeshe Bwana na usiniache kamwe. Naomba na kupokea katika jina la Yesu, Amen.

Tuesday, April 16, 2013

Neno la leo

Zab 13:5-6 “Nami nimezitumainia fadhili zako; Moyo wangu na uufurahie wokovu wako. Naam, nimwimbie BWANA, kwa kuwa amenitendea kwa ukarimu”

TAFAKARI: Kwa yale yote mema Mungu aliyokutendea, huna budi kumwimbia nyimbo na kumshukuru.Wapo watu wengine hawawezi kuomba msaada pale wanapokuwa na shida, lakini kutokana na wema wao Mungu hupendezwa nao na kuwaletea watu wa kuwasaidia bila wao kuomba msaada. Ni jambo la kumshukuru sana Mungu hasa kwa kutambua mengi aliyokutendea.
SALA: Mwenyezi Mungu, umekuwa mwema sana kwangu. Nakuamini wewe na yale ufanyayo katika maisha yangu. Saa nyingine naona kabisa uwepo wako na kufarijika moyoni mwangu. Naomba ukawaguse na wengine ambao bado hawajapitiwa na mkono wa upendo na ukarimu. Wapanguse machozi wanaolia Bwana, na uwape tumaini waliokata tamaa. Naomba na kupokea katika jina la Yesu, Amen.

Monday, April 15, 2013

Neno la leo

1Pet 1:13 “Kwa hiyo vifungeni viuno vya nia zenu, na kuwa na kiasi; mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika Ufunuo wake Yesu Kristo”

TAFAKARI: Siku zote tunatakiwa kujiandaa kwa kitu chochote iwe vita, ama kazi ngumu ya aina yoyote. Labda mtu atafikiria natakiwa kufanya mazoezi ili niyakabili matakwa ya maisha ya kila siku, kitu ambacho si rahisi. Tunakiwa kujiandaa kiroho kwa kusoma neno la Mungu na kudumu katika imani, ili siku neema ikifunuliwa tuwe miongoni mwa wateule wa Mungu.
SALA: Bwana Mungu, nasoma neno lako kila siku na kufuata mafundisho yako, lakini Bwana nakiri kwamba mimi bado ni dhaifu. Wakati mwingine napatwa na matatizo na kujaribu kutatua shida hizo kwa akili zangu mwenyewe. Nisaidie Bwana nijiandae kiroho hata nikiteleza nisianguke pabaya, bali mikononi mwako. Naomba na kupokea, Amen.