Friday, April 26, 2013

Neno la leo

Kol 4:2 “Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani”

TAFAKARI: Yatupasa kumuomba Mungu kwa bidii zote ili atufungulie milango ya baraka na kueneza siri ya neno lake la uponyaji. Tumuombe zaidi Mungu atupe shauku la kutaka kusali.
SALA: BWANA, nataka kuona na kutambua kazi yako katika maisha yangu. Yaongoze macho yangu katika kuona pale unaposikia na kujibu sala zangu. Na zaidi nipate kukujua wewe vizuri kila siku ninapokutana na wewe. Naomba unijaze kwa maarifa yako na akili zako Ee BWANA, nipe nguvu nisimame imara katika kujitoa kwangu, kwako. Naomba hayo yote katika jina la Manao Yesu Kristo ashiye na kutawala daima milele.

Thursday, April 25, 2013

Neno la leo

Zab 6:9 “BWANA ameisikia dua yangu; BWANA atayatakabali maombi yangu”

TAFAKARI: Wakati mwingine tunakuwa tunajiuliza maswali mengi juu ya mambo yanayotokea. Ama pengine mtu anapitia majaribu kadhaa na kudiriki kushuku uwepo wa Mungu kama yupo ama ala. Mungu anasikia kila hitaji la mwanadamu, na hata majaribu mtu apitiayo ni sehemu moja wapo ya kupima imani ya mtu.
SALA: Mwenyezi Mungu, Baba wa Rehema, nasema asante kwa kusikia sala zangu. Kuna wakati nilikuwa nimechoka na kukata tama lakini wewe umenitoa kwenye mitego ya mwovu shetani. Sasa mimi ni kiumbe kipya na ninaukubali ukamilifu wako, Ee Mungu wa rehema. Naomba na kupokea katika jina la Yesu Kristo, Amen.

Wednesday, April 24, 2013

Neno la leo

Zab 91:1-2 “Aketiye mahali pa siri pake aliye juu, Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi. Nitasema BWANA ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu nitakayemtumaini”

TAFAKARI: Ukuu wa Mungu ni mkubwa kiasi kwamba hauwezi kulinganishwa na chochote. Nguvu zake ni za ajabu na hutushindia mengi na kutukinga na uovu wa aina yoyote.
SALA: Mwenyezi Mungu, wewe uliye mlinzi mkuu wa Israeli, kwa namna ya pekee naja mbele yako nikiomba ulinzi wa familia zetu dhidi ya ajali, magonjwa, majeraha na madhara ya aina yoyote ya mwili, akili na hisia. Naomba utuwezeshe kukimbilia daima vivulini mwa mbawa zako ili tuepukane na mabaya hayo. Moyo wangu umekutumaini wewe kwa makuu makubwa unayozidi kunitendea, nifanye BWANA nidumu daima katika pendo lako. Katika jina la Yesu Kristo naomba na kupokea, Amen.

Tuesday, April 23, 2013

Neno la leo

Mt 6:3-4 “Amin, nawaambieni, wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume. Sadaka yao iwe kwa siri; na baba yako aonaye sirini atakujazi”

TAFAKARI: Ni vigumu kwa mtu kutoa msaada na asitake julikana ya kwamba amesaidia. Watu wengi wakitoa misaada mbalimbali hupenda kuhusisha vyombo vya habari ili wajulikane ya kwamba wanasaidia. Lakini tunasahau kwamba Mungu anaona mioyo yetu na hupendezwa na utoaji wetu.
SALA: Bwana Mungu, niwezeshe nione kwamba kila ninapotoa sadaka, misaada yangu na wakati wangu iwe ni kwa utukufu wako. Kwa maana napata vyote toka kwako hivyo sifa na utukufu nakurudishia wewe. Nipe roho ya unyenyekevu ili kwamba baraka za utoaji zikae ndani ya moyo wangu. Naomba na kupokea katika jina la Yesu Kristo, Amen.

 

Monday, April 22, 2013

Neno la leo

Mit 5:21 “Kwa maana njia za mwanadamu zi mbele za macho ya BWANA, Na mienendo yake yote huitafakari”

TAFAKARI: Mungu huzichunguza njia za mwanadamu. Yawezekana mtu mwingine akafanya kitu kibaya akijiamini kwamba hakuna anaemuona. Lakini yeye aliye mbinguni huona na kuitafakari mienendo yetu wote.
SALA: Bwana Mungu, naomba nifundishe njia zako ili niweze kudumu na kuenenda katika njia hizo. Najua nimekuudhi na kukuangusha na hata nimejiangusha mwenyewe Mungu, lakini Bwana hujaniacha. Nichunguze Bwana, wala usinichoke zaidi nivute katika tumaini lako. Wewe uliyenifichia aibu katika yale niliyokutenda naomba unikumbatie kwa mbawa zako na kunisamehe. Katika jina la Yesu naomba na kupokea, Amen.