Saturday, January 26, 2013

UHUSIANO WETU NA BABA YETU WA MBINGUNI

Labda nianze kwa kuuliza uhusiano wa mzazi na mtoto kwa maisha yetu ya kila siku ukoje? Kwa maisha ya kawaida mtoto akiamka humuomba Baba ama Mama ampe kitu chochote au amfanyie kitu chochote na mzazi huyo bila kusita atafanya.
Lakini kadri mtoto anavyokua na kuendelea kumuomba mzazi wake kitu inafikia wakati mzazi anachoka na pengine kuanza kulalamika ya kuwa mtoto huyu anaomba sana.
Vivyo hivyo ni sawa na maisha yetu na Mungu baba wa mbinguni. Naye vile vile huwa anachoka pale kila saa tunapoomba atutimizie mahitaji yetu.
Yoh 1:11-13 “Alikuja kwake wala walio wake hawakumpokea. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu”
Anatuambia wale wote waliompokea wamefanyika kuwa watoto wake. Je unamfurahishaje baba yako wa mbinguni kama umfurahishapo mzazi wako. Waweza kusema ni kwa kufuata yale atufundishayo na kuendenda katika njia anazotuongoza yeye. Lakini kwa kumfanyia vitu ambavyo yeye atajiskia furaha ya kuwa mwanangu kafanya haya machoni pangu na imenipendeza.
Ni vyema unapoamka ukamshukuru Mungu kwa kukuamsha salama. Mwambie asante Mungu kwa kuniamsha salama nikiwa mwenye nguvu na afya tele. Muulize Mungu nikufanyie nini kwa siku ya leo? Ama nikuimbie nyimbo gani leo? Nikusomee zaburi gani Bwana? Mueleze ya kwamba unatambua vipaji vingi alivyokupa na muulize ungependa uwabarikije wengine kwa vipaji hivyo? Nina hakika kwa kufanya hivyo moyo wako utakua umejawa na furaha na siku yako itakuwa nzuri.
Hata katika maisha ya kawaida si mzazi unafurahia sana pale mtoto anapokufanyia kitu? Unafurahi kuona mtoto amekupikia, amekununulia zawadi kwa uwezo wake mwenyewe na mambo mengine yanayofanana na hayo. Hiyo ni mifano ya kufananisha na maisha ya kumtumikia Mungu wetu.

Jenga tabia hiyo ya kuamka na kumuuliza Mungu umfanyie nini badala ya kuamka na kumuomba tu kila siku akusikilize na akusaidie wewe tu. Kwa kufuata haya moyo wako utakusukuma kufanya mambo mengi kwa kuongozwa na roho mtakatifu.

Mbarikiwe!

Friday, January 25, 2013

Neno la leo

Mithali 13:2-3 “Mtu atakula mema kwa matunda ya kinywa chake; Bali nafsi ya mtu haini itakula jeuri. Yeye alindaye kinywa chake huilinda nafsi yake; Bali afunuaye midomo yake atapata uharibifu”

TAFAKARI: Maneno mema huleta thawabu, lakini matokeo ya maneno ya hila ni jeuri. Kauli yenye nidhamu ni muhimu kwa sababu maneno yenye ukali huleta uharibifu.
SALA: Mwenyezi Mungu, wewe uketiye mahali pa juu palipoinuka, asante kwa wema wako kwangu. Mungu naomba utakase kinywa changu nikapate kutamka yale yanayokupendeza.Nipe ulimi wa kunena maneno yenye busara kamwe nisiteleze na kutamka maneno yenye kuleta uharibifu. Katika jina la Yesu naomba na kupokea, Amen.

 

Thursday, January 24, 2013

Neno la leo

Mithali 10:18 “Yeye afichaye chuki ana midomo ya uongo, na yeye asingiziaye ni mpumbavu”

TAFAKARI: Siku zote mtu mwenye chuki ndani ya moyo wake maneno yake huwa ya unafiki ama yenye kuudhi au uchochezi.
SALA:  Mwenyezi Mungu wewe uliye mwingi wa rehema, naomba usininyime rehema zako Baba, niangazie nuru ya uso wako na zaidi ukaniepushe na watu wabaya, wenye chuki na wachonganishi. Katika jina la Yesu naomba na kupokea, Amen.

Wednesday, January 23, 2013

Neno la leo

Mithali 10:8-9 “Aliye na akili moyoni mwake atapokea agizo; Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka. Aendaye kwa unyofu huenda salama, bali apotoshaye njia zake atajulikana”

TAFAKARI: Mtu hujenga hekima kwa njia ya kujifunza na si kwa njia ya kujisifu. Mtu mwenye kuishi maisha ya unyofu humpatia hekima na usalama na si kwa njia ya shughuli zake za hila.

SALA: Bwana nimekutumaini wewe sikuzote nisiaibike, naomba unijaze maarifa, hekima na uniondolee majivuno ndani ya moyo wangu ili nikaishi kwa kukufurahisha na kukutumikia wewe. Amen

Tuesday, January 22, 2013

Neno la leo

Mithali 10:6-7 “Baraka humkalia mwenye haki kichwani; bali jeuri hufunika kinywa chake mtu mwovu. Kuwakumbuka wenye haki huwa na baraka, bali jina la mtu mwovu litaoza”

TAFAKARI: Matendo ya mtu huonyesha tabia yake ikiwa ni mbaya au nzuri na sifa yake itaendelea kuwepo hata baada ya kufa.

SALA: Mwenyezi Mungu nakushukuru kwa upendo wako mkuu kwangu. Bwana naomba niongoze nikaishi kwa kufuata misingi yako niepukane na majaribu ya kutenda uovu. Vishawishi ni vingi katika ulimwengu wa sasa lakini naamini nikikutegemea wewe kamwe sitaanguka katika uovu. Nipe faraja ya kulitamka jina lako kila inapoitwa leo. Naomba hayo nikiamini katika jina la Yesu Kristo, Amen.

Sunday, January 20, 2013

Ujumbe wa Jumapili ya leo

Zab 27:3 “Jeshi lijapojipanga kupigana nami, moyo wangu hautaogopa. Vita vijaponitokea, hata hapo nitatumaini”

TAFAKARI: Ukiwa unamtegemea Mungu hakuna upanga utakaosimama juu yako. Ukiwa naye ndani ya moyo wako hakuna vita yoyote itakayokushinda kwa maana yeye ni mshindi wa yote.

SALA: Mungu baba, wewe uliye jemadari wa vita naomba ukaimarike ndani ya moyo wangu nikutegemee wewe siku zote. Nataka kufanana nawe Mungu wangu kwa maana wewe  haubadiliki kama wanadamu. Mkono wako wa baraka usinipite eeh Mungu mwenye rehema nyingi. Katika jina la Yesu naomba na kupokea, Amen.