Neno LAANA katika kamusi limetafsiriwa kama ukosefu wa radhi za
mwenyezi Mungu, hasira ya Mungu. Au ni apizo atoalo mtu kwa mtu mwingine ili
afikwe na ubaya, uovu, msiba au hasira ya Mungu. LAANI limetafsiliwa kama, shtakia kwa Mungu, au
ombea uovu.
Zipo laana nyingi lakini leo ningependa kuzungumzia laana
zifuatazo:-
- Ukoo/familia:-
laana zinazojiendeleza kwenye ukoo hutokana na matokeo ama matunda ya
dhambi. Kwa mfano unakuta katika familia husika kuna wengine wana laana za
magonjwa sugu kama kansa, kwenye hiyo hiyo familia wengine hawaolewi,
wengine wameolewa lakini ndoa hazidumu, wengine hawapati mimba. Familia
nyingine utakuta kuna vifo vya ghafla, wanaanza maisha na kufanikiwa na
kuwa na mali na biashara kubwa au kazi lakini mwisho wao wanaishia
kufilisika na kufa kwa mateso makali.Unatakiwa kuomba maombi ya rehema na
toba na lazima utamke kilichofanyika na matokeo yake. Kwa sababu kila dhambi iliyofanyika ni
kutokana na kuwa na miungu mingine. Dhambi inatokea pale mtu anapomwacha
Mungu wa kweli na kusikiliza miungu mingine. Sasa unapokosa msaada wa
Mungu wa kweli unapata misaada ya miungu inayokusababisha wewe kutenda
kinyume na Mungu. “Usiwe na miungu mingine ila Mimi- Kumbukumbu
la torati 5:7”
- Laana
za kulaaniwa na mtu mwingine:- Yawezekana ulikosana na
rafiki yako ama mtu mwingine pengine mwalimu wako wa shule akakuchukia na
kukulaani. Anaweza kukulaani kuwa na kamwe hutakaa uendelee kwa kila
utakalofanya usifanikiwe.
- Laana
za kujilaani mwenyewe:- Kuna watu hawaridhiki na
jinsi walivyo ama niseme viungo vya miili yao, yaani kwa ufupi
hawajikubali ama kujiamini. Utakuta mtu analalamika na kusema “aah mimi
kwa ufupi huu sidhani kama nitakaa nipate mwanamke mrefu atakaenipenda,
ama mwingine atajilaani kwa kusema kamwe hawezi kuwa mtu wa kwanza
darasani kwa sababu tu ya mtu fulani nyumbani kwao hajawahi kuwa” Siku
zote maneno huumba na kujiumba, kwa maana hiyo yale uyatamkayo mdomoni
kwako vivyo hivyo yanafanyika.
- Laana
ya vitu visivyoisha: Kuna watu wamelaaniwa kwa kila
wakigusacho kisiendelee na matokeo yake hujikuta wameanzisha vitu mbali
mbali bila hata kimojawapo kukamilika. Mfano mtu anataka kujenga lakini
anaishia nusu na kuanza kitu kingine ambacho nacho hakifiki mbali. Nataka
kuanzisha biashara ya nguo, atanunua sehemu ya kuuzia nguo lakini hakuna
kitakachoendelea. Watu kama hawa ni wale wanaonena kwa midomo lakini
hawatekelezi.
- Laana ya kufanya tendo la ndoa na dada
yako au kaka yako, baba yako au mama yako
Kuna mambo mengine sio rahisi hata kuelezea lakini yapo na yanafanyika mtu amelala na Dada yake, mwingine na kaka yake, laana ya Mungu imeagizwa juu yao “Kumb 27:22 Na alaaniwe alalaye na umbu lake, binti ya babaye au Binti ya mamae. Na watu wote waseme Amina”
Haya yote yanatokana na UPOFU wa mawazo. Akili ikifungwa mtu
hawezi kufanya maamuzi yoyote. Pia akili ikifungwa mtu haoni ugumu wa dhambi. “2Wakorintho 3:14 ila fikira zao zilitiwa uzito. Kwa maana
hata leo hivi wakati lisomwapo Agano la kale, utaji uo huo wakaa, yaani
haikufunuliwa kwamba huondolewa katika Kristo”. Soma pia Waefeso 4:18
NAVUNJAJE
VIFUNGO?
Biblia inapozungumza habari ya watu waliofungwa wapate
kufunguliwa, hii ina maana ya kuwa kuna watu wamefungwa chini ya utawala wa
nguvu za giza katika ulimwengu wa Roho. Watu hawa wamefungwa kwenye magereza na
Ibilisi.
Tutambue ya kuwa Yesu aliposema amekuja kutuokoa hii inamaanisha
kwamba kuna mahali ambako tusingeweza kujikwamua wenyewe bila nguvu yake yeye
mwenywe kuingia kati yetu.
Aliyahidhirisha haya kwenye kitabu cha nabii Isaya 61:1-2 Roho ya Bwana Mungu i juu yangu kwa sababu Bwana
amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema, amenituma ili kuwaganga
waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za
kufunguliwa kwao”.
Vunja uhusiano wako na hiyo miungu pamoja na kazi zake na agano
lililofanyika kati ya familia au ukoo wako na hiyo miungu. Kila unapotamka
mwisho wake sema kwa sababu nimesamehewa. Ipo mistari mingi ya kuvunja maagano
lakini mimi nitakupa kifungu hiki cha mstari katika kuvunja maagano na mapoozo
ya aina yoyote. “Tena itakuwa katika siku hiyo mzigo
wake utaondoka begani mwako na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa
kwa sababu ya kutiwa mafuta” Isaya 10:27
Kifungu kingine ambacho waweza tumia ni kwa kutaja maneno haya
wakati wa kuvunja vifungo ama laana “Bwana Yesu, nasimama
mbele zako na katika ulimwengu wa roho, kujiachanisha nafsi yangu (Taja jina
lako) na vifungo vya kuzimu kwa upande wa baba yangu na mama yangu kwa sababu
nimesamehewa.” Endelea vivyo hivyo kwa kutaja, roho na mwili kwa kutumia
maneno hayo hayo uponyaji hufanyika katika nafsi, mwili na roho.
Mtegemee Roho
Mtakatifu kwa maana atakufundisha mengi ikiwemo kuomba na maagizo ya Yesu. Na
kwa kufuata maagizo ya Yesu na kuenenda kwa roho hivyo vifungo vya nafsi
vitakwisha. Soma Wagalatia 5:16-25, Luka 22:40-46. Kudumu katika maombi,
kuenenda kiroho na kuepuka uovu ni muhimu kwa sababu kwa kufuata misingi hiyo
ndipo unafunguliwa vifungo kwa kuombewa ama kwa nguvu inayotenda kazi ndani
yako kupitioa roho mtakatifu. Lakini pia ni muhimu kujua ya kwamba sala ya toba
pekee haitoshi kumfungua mtu kama ana vifungo na sio imani tu bali na juhudi
binafsi ya mtu itasaidia katika kumuweka huru. Wapo watu wanaotaka kupokea
miujiza bila ya kuwa na mabadiliko yoyote, ama bila kusoma neno la Mungu na
kukua kiroho ama bila kuomba. Wao husubiria siku za maombi, ama mikesha ama
makongamano ya maombi ili waombewe kisha baada ya hapo hawajishughulishi katika
kukua kiimani.
Kuwa hodari
katika Bwana ili upate ulinzi wa Mungu. Waefeso 6:10-11 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa
nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu mpate kuweza kuzipinga hila za shetani”
Maana ya kuwa
hodari katika Bwana ni kukaa kwenye maombi, kusoma na kulishika neno lake liwe
ndani yako, na kutaka kumjua yeye zaidi. Sikuzote Sali kwa bidii katika
kupambana na muovu shetani ndo mana tunaambiwa vaeni silaha zote za Mungu ili
kuweza kupingana na hila za muovu shetani.
Mbarikiwe na
Mungu!