Friday, March 8, 2013

Neno la leo

Yoh 12:26 “Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo”

TAFAKARI: Leo tuna nafasi iliyotolewa na Yesu kwa wanafunzi wake, yaani hatuwezi kumtumikia bila kusimama imara na kufuata maelekezo yatolewayo na neno lake. Ameahidi kuwepo popote pale tutakapokuwapo, kwa hiyo hakuna budi kumtumikia yeye.
SALA: Bwana Yesu, tunaomba tusikie uwepo wa ahadi yako ya kuwepo nasi pale shughuli tuzifanyazo za kukutumikia wewe zitatupeleka. Usikae mbali nasi Bwana kwa maana tunahitaji muongozo wako pale tutakapokwama. Ni katika jina lako takatifu tunaomba na kupokea, Amen.

 

Thursday, March 7, 2013

Neno la leo

Yoh 10: 4 “Naye awatoapo nje kondoo wake wote, huwatangulia; na wale kondoo humfuata, kwa maana waijua sauti yake”

TAFAKARI: Kama wanadamu tunafahamu kondoo walivyo, hivyo basi tujiweke kwenye huu mfano wa kondoo wanaochungwa. Kwa mfano kondoo wengine ni wale wasio na muelekeo, wengine wanatembea taratibu sana na hata hulazimika kuchapwa ndiyo wapige hatua. Na wale wanaosikia sauti ya mchungaji akiamuru na hupiga hatua kufuatana na hiyo. Tujue kwamba, kusikia na kutambua sauti si tatizo, bali cha muhimu ni kumfuata mchungaji.
SALA: Bwana Yesu tunaomba utuongoze tusikie sauti yako na kukufuata wewe kwa sababu tunafahamu wewe utatulinda na kutulisha chakula kilicho kamili. Katika jina la Yesu tunaomba na kupokea, Amen.

Wednesday, March 6, 2013

Neno la leo

Luka 9:61 “Mtu mwingine pia akamwambia, Bwana nitakufuata; lakini nipe ruhusa kwanza nikawaage watu wa nyumbani kwangu”

TAFAKARI: Tunapoweka ahadi ya kumfuata Yesu, lazima tukumbuke kwamba hakuna kugeuka nyuma. Ukijitoa kwake basi fanya kazi zake kwa kutimiza mapenzi yake. Lakini endapo tutakuwa tumejitoa kwa kazi nyingi basi kuna wakati tutapata sababu za kujiengua kuwa karibu naye.
SALA: Mwenyezi Mungu, tupe busara na maarifa ya kutenga vipaumbele vyetu katika misingi iliyo sahihi na zaidi tupe nguvu ya kufanya maamuzi yetu kwa hekima. Tunaomba hayo kupitia mwana wako na Bwana wetu Yesu Kristo, Amen.

Tuesday, March 5, 2013

Neno la leo

Luka 7:9 “Yesu aliposikia hayo alimstaajabia, akaugeukia mkutano uliokuwa ukimfuata akasema, nawaambia, hata katika Israel sijaona imani kubwa namna hii.

TAFAKARI: Kuna wakati watu wanakua wadadisi juu ya kwamba wakae na makundi gani pindi wakiwa wamempokea Yesu na kumfuata yeye. Huangalia kwamba huyu mtu ana imani gani juu ya Mungu ambapo anaweza kuwa mfano kwa wengine. Lakini Yesu, anasema tusibague watu na tuwe wakarimu kwa watu tusiowajua, tuwapende wale wenye mapungufu na tofauti nyingi, kufungua milango kwa wageni. Tuzidishe Imani yetu kwa yeye kwa sababu ndiye mponya wa pekee.
SALA: Bwana Yesu, tunaomba usikie vilio vyetu pale tukuitapo. Tujaze mioyo yetu kwa Imani kuu inayoshangaza na kuponya wengi. Katika jina la Yesu tunaomba na kupokea, Amen.

 

Monday, March 4, 2013

Neno la leo

Yoh 8: 12 “Basi Yesu akawaambia tena akasema, mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima”

TAFAKARI: Katika maisha ya kawaida wengi wetu tunaogopa giza, hii inatokana na kwamba tumekuwa tukiambiwa kwamba mambo mabaya mengi hufanyika gizani. Basi kwa hofu hiyo hiyo tuache mambo ambayo yanatuweka gizani na tumfuate Yesu, yeye awe taa itumulikiayo usiku na mchana.
SALA: Mwenyezi Mungu tunaomba utumulike katika maisha yetu, ili tunapokufuata katika njia yako tusiteleze na kuanguka chini. Katika jina la Yesu tunaomba na kupokea, Amen.