Friday, February 22, 2013

Neno la leo

Mt 9:9 “Naye Yesu alipokuwa akipita kutoka huko aliona mtu ameketi forodhani, aitwaye Mathayo, akamwambia, Nifuate. Akaondoka, akamfuata”

TAFAKARI: Pengine wakati ule wa kipindi cha utozwaji wa ushuru wa hali ya juu na unyanyaswaji wa watu, ulimuingia Mathayo na kuchoshwa nao. Huenda aliskia habari za Yesu aliyekuwa anahubiri habari njema kuhusu ufalme wa mbinguni, alikuwa anaponya wengi na kuwavuta karibu. Aliposkia tu sauti ya Yesu akimuita aliruka haraka na kumfuata. Je, tunajifunza nini juu ya habari hii?
SALA: Bwana tunaomba uwe mwenye uvumilivu nasi pale tunapojishauri kuitikia mualiko wako wa kukufuata.Tunaomba utuvute karibu nawe nasi tuwe miongoni mwa wafuasi wako, katika jina la Yesu tunaomba na kupokea, Amen.

Thursday, February 21, 2013

Neno la leo

Mt 8: 22 “Lakini Yesu akamwambia, Nifuate; waache wafu wazike wafu wao

TAFAKARI: Katika hadithi hii kitu cha kwanza tunachotakiwa kufanya ni kuskia sauti ya Mungu na kufwata yale anayotuelekeza, na mengine yatakuja baadae. Si rahisi kufanya hili kama hujajitoa na huna hofu ya Mungu.
SALA: Bwana Mungu, tuwezeshe na utupe sikio la kusikia ili tufuate sauti yako ya upendo pindi pale unapotuamuru kufanya kazi yako, kukufuata na kutupa maagizo ya kukutumikia wewe. Katika jina la Yesu tunaomba na kushukuru, Amen.

Wednesday, February 20, 2013

Neno la leo

Mt 8:19 “Mwandishi mmoja akamwendea, akamwambia, Mwalimu, nitakufuata kokote uendako”

TAFAKARI: Ukisoma hadithi ya mwandishi aliyeonekana katika kitabu hichi cha Mathayo kwa haraka unaweza kusema ameonyesha maana ya kumfuata Yesu na Kujitoa kwa ajili yake (to follow and then made a daring commitment). Lakini vilevile, waweza kusema kuwa alikubali kumfuata bila kujua kuna gharama yake, yaani safari ya kwenda mbinguni sio rahisi lazima mtu utakumbana na vikwazo. Mungu anahitaji watu ambao watajitoa kwake kwa moyo wote na sio kwa kusita sita na kurudi nyuma.
SALA: Mwenyezi Mungu, tunaomba utusaidie tuweze kusikia sauti yako na kuyatoa maisha yetu kwako ili tuishi kwa kukutegemea wewe daima. Katika jina la Yesu tunaomba na kupokea, Amen.

Tuesday, February 19, 2013

Neno la leo

Yohana 14:27 “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo”

TAFAKARI: Mungu ametuachia amani. Na vitu anavyotupa haviwezi kufanana na vile atoavyo mwanadamu. Yamkini ni magari ya kifahari, pesa nyingi, na vingine vifananavyo na hivyo, kamwe haviwezi kufanana na vitu atupavyo Mungu.
SALA: Mwenyezi Mungu tunakushukuru kwa upendo wako wa ajabu. Umetupa amani katika nchi zetu lakini kwa kukosa maarifa tumeshindwa kutumia ipasavyo yale unayotupa. Tusamehe Bwana na tunaomba ukalete amani na upendo miongoni mwetu. Katika jina la Yesu tunaomba na kupokea, Amen.

Monday, February 18, 2013

Neno la leo

Zab 55:22 “Umtwike Bwana mzigo wako naye atakutegemea, Hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele”

TAFAKARI: Ukuu wa Mungu ni mkubwa sana, hakuna chochote kitakachoweza kufananishwa naye.Mueleze shida zako naye atakutendea mema.
SALA: Mungu wangu na Baba yangu, nashindwa kuelezea ukuu wako kwa jinsi ulivyo mkubwa. Maisha yangu yamebadilika kutokana na matendo ya ajabu uliyonifanyia. Wewe mwenye haki nitakushukuru siku zote za maisha yangu na najiachia kwako daima. Naomba na kupokea katika jina la Yesu, Amen.