1 Yohana 4:16"Mungu ni
upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani
yake".
Upendo wa Mungu wetu ni mkuu sana
na unapita vitu vingi mno. Hata mtu akianza kuandika leo hii juu ya Upendo wa
Mungu wino utakwisha kwa maana ni mkubwa mno hauelezeki. Mungu aliupenda
ulimwengu hata akamtoa mwana wake wa pekee Yesu Kristo ili kila amwaminie yeye asipotee
bali awe na uzima wa milele. Yesu alitufia msalabani kwa ajili ya dhambi zetu,
hii inadhihirisha jinsi gani Mungu amempenda mwanae huyo wa pekee afe kwa ajili
ya mimi na wewe.
Upendo huleta amani, furaha na
faraja. Ndani ya moyo wangu nina amani tele na furaha. Nampenda Kristo kwa
sababu ameniokoa kwa damu ya thamani. “Utanijulisha njia ya uzima; mbele za uso
wako ziko furaha tele; na katika mkono wako wa kuume mna mema ya milele,”
Zaburi 16:11
Upendo hutoka kwa Mungu na kila
mwenye upendo ni mtoto wa Mungu. “Twampenda yeye kwa sababu yeye alitupenda
kwanza na akaichukua mioyo yetu kwake mwenyewe” 1 Yohana 4:19. Hakuna kitu
muhimu katika maisha ya binadamu kama UPENDO. “Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabiri;
haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu;
hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia
yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote. Upendo haupungui neno
wakati wowote - 1Wakorintho 13:4-8
Mtu mwenye kukosa upendo huyo
hayuko ndani ya Kristo na siku zote huwa na chuki. Hata katika Biblia
imeonyeshwa kwamba mtu akisema anampenda Mungu ana anachukia ndugu yake ni
muongo. “1Yohana 4:20 Mtu akisema, nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu
yake ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi
kumpenda Mungu ambaye hakumwona”.
Si vyema kuchukiana juu ya mambo
madogo madogo.Huna sababu ya kumchukia ndugu yako sababu ya wivu ama kumchukia
jirani yako sababu ana maendeleo ambayo wewe huna. Hata amri ya pili inasema
mpende jirani yako kama nafsi yako, sasa iweje unamchukia jirani ama ndugu yako
wa kuzaliwa naye. Hii haimpendezi Mungu na yakupasa kumrudia yeye na kujifunza
neno lake ndipo utaelewa maana halisi ya upendo. Tuzishike amri za Mungu na kukaa katika pendo lake.
Upendo haujalishi umpendaye ni
tajiri ama maskini. Kuna watu ambao huchagua watu wa kuwapenda yaani ambao
wanaona wako kwenye status zao. Huo sio upendo bali ni kutafuta watu ambao
unadhani utapata furaha kwa sababu tu pengine anaendesha benzi, anakula sehemu
za bei ya juu, anavaa vitu vya bei na vitu vingine vinavyofanana na hivyo.
Tuwe na upendo wapendwa kwa
sababu ukiwa na upendo siku zote utakua na amani. Kwa maana mtu mwneye Upendo
hulipa mabaya kwa mazuri, kamwe hawi wenye visasi. Mwenye upendo siku zote ni
mnyenyekevu mbele za watu na hujali wengine zaidi yake mwenyewe.
Usiruhusu mwanadamu akurudishe
nyuma na ukatoka katika pendo. Binafsi tangu niijue Biblia maisha yangu yamekuwa
ya furaha sana na amani. Na ndiyo maana nasema maisha yangu ni biblia yangu
mahali ambapo napata faraja kila nisomapo. Through biblia nimejifunza nini
maana halisi ya upendo, na mambo mengine mazuri.
Tujitunze katika upendo wa Mungu,
huku tukingojea rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo kwa kutazamia uzima wa milele.
Na haya yote yanapatikana kwa kumuomba roho mtakatifu akuongoze uwe na upendo.
Mimi nawapenda, muwe na Jumapili njema.