Friday, March 1, 2013

Neno la leo

Mt 7:17 “Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri na mti mwovu huzaa matunda mabaya”

TAFAKARI: Neno liko wazi kabisa, kwamba hakuna mti ambao umestawi kwa kuwekewa mbolea nzuri ukazaa matunda mabaya. Na vivyo hivyo, mzabibu hauwezi kuzaa miiba, ama mchungwa kuzaa maembe. Muombe Mungu akusaidie utende mema na uzidi kumtegemea yeye. 
SALA: Mwenyezi Mungu, Asante kwa kutukomboa kwa damu ya mwana wako Yesu Kristo, Bwana tunaomba uzidi kutunyunyizia mbolea yako ya Imani ili tukastawi na kukua zaidi kiroho, kamwe tusirudi nyuma. Katika jina la Yesu tunaomba na kupokea, Amen.

Thursday, February 28, 2013

Neno la leo

Mk 2: 15 “Hata alipokuwa ameketi chakulani nyumbani mwake, watoza ushuru wengi na wenye dhambi waliketi pamoja na Yesu, na wanafunzi wake kwa maana walikuwa wengi wakimfuata”

TAFAKARI: Mara nyingi watu huchagua marafiki ambao tabia na hadhi zao zinaendana. Hii hupelekea kujitenga na wale wanaoonekana watenda dhambi na penginge kuwanyooshea vidole. Lakini katika maisha ya kumfuata Yesu hatufundishwi hivyo, bali anahimiza kuwa karibu na wenye dhambi ili tuweze kuwasaidia katika hatua zao za kubadilisha maisha yao.
SALA: Bwana Yesu, tunaomba utusaidie ili tuweze kukaa pamoja na wenye dhambi wanaojitoa kukufuata wewe. Tupe busara na maarifa katika kushiriki nao kwenye shughuli mbali mbali na hata kuwapa mafundisho utoayo wewe tukiongozwa na roho mtakatifu wako. Katika jina la Yesu tunaomba na kupokea, Amen.

Wednesday, February 27, 2013

Neno la leo

Rum 8: 14 “Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu”

TAFAKARI: Wakati wa kwaresma ni muda ambao tunakuwa wenye kusafishwa na roho wa Mungu. Ni roho mtakatifu wa Mungu ndiye anaetukusanya pamoja na wote wamfuatao Kristo, ni kama kondoo waliopotea wanaporudishwa zizini hali kadhalika habari za mwana mpotevu nae alipoamua kurudi kwa baba yake. Hivi vyote havikutendeka pasipo kuongozwa na roho wa Mungu.
SALA: Bwana Yesu, tunaomba roho wako mtakatifu atuongoze ili tuweze kutambua nafasi zetu katika familia na kutenda yale yanayokupendeza wewe. Katika jina la Yesu tunaomba na kupokea, Amen.

Tuesday, February 26, 2013

Neno la leo

Mt 9: 27 “Yesu alipokuwa akipita kutoka huko, vipofu wawili wakamfuata wakipaza sauti, wakisema, Uturehemu mwana wa Daudi”

TAFAKARI: Kuna wakati mtu unaona muda huu ni mdogo hautoshi kwa Mungu kuniskia pale nitakaposali, lakini kwa imani ukipaza sauti na kuomba kwa nguvu, hatimaye maombi yako hujibiwa. Ni imani tu inapeleka mtu kupata hitaji lake toka kwa Bwana ama kupona.
SALA: Bwana Mungu, tusamehe pale ambapo tumekosa na kushindwa kukuamini wewe ya kuwa unatenda miujiza. Tusaidie tuone na kwa imani tu tuwezeshe tuone zaidi na zaidi rehema zako za ajabu. Katika jina la Yesu, tunaomba na kupokea, Amen.

Monday, February 25, 2013

Neno la leo

Mt 19: 21 “Yesu akamwambia, ukitaka kuwa mkamilifu, enenda ukauze ulivyo navyo, uwape maskini nawe utakuwa na hazina mbinguni; kasha njoo unifuate”

TAFAKARI: Katika hili zawadi ya bure ya Mungu inakuja na gharama na ulazima. Ni juu ya sisi kutambua ni vitu gani tunavijali zaidi. Lakini vilevile, tunapata faida kubwa pale tujuapo mualiko wa Mungu ni wa haraka mno na kujua maisha ya kumfuata yeye ni ya utajiri mkubwa.
SALA: Bwana, tunaomba utangulize matakwa ya maskini na wahitaji wako juu yetu hasa pale tunapokuwa na nafasi ya kuchagua katika vile ulivyotupa.  Katika jina la Yesu tunaomba na kupokea, Amen.