Friday, April 5, 2013

Neno la leo

1Yoh 5:14 “Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia”

TAFAKARI: Mungu husikia kila hitaji la mtu endapo tunamuomba kwa kuamini ya kwamba atatutimizia mahitaji yetu. Masikio yake yako wazi kusikia vilio vya mioyo yetu, hivyo hatuna budi kumuangalia yeye daima.
SALA: Bwana Mungu, asante kwa kunisikiliza. Natambua ya kwamba ni zawadi pekee kwa mimi kujiachia kwako Mungu kwa maana utaniondolea wasi wasi ndani ya moyo wangu. Mara nyingine nimekuwa na maswali ya ajabu na hata kuuliza juu ya mahitaji yangu, lakini wewe hukuacha kunisikiliza. Nakupenda Mungu wangu na kamwe sitaacha kukutumikia wewe. Katika jina Yesu naomba na kushukuru, Amen.

Thursday, April 4, 2013

Neno la leo

Zab 71:5 “Maana ndiwe taraja langu, Ee Bwana MUNGU, Tumaini langu tokea ujana wangu”

TAFAKARI: Ni jambo la faraja sana pale mtu anapompokea Kristo kuwa mwokozi wa maisha yake. Anakuwa mwenye nguvu mpya, mwenye wingi wa busara na hekima na zaidi Imani yake huongezeka maradufu kwa kumtegemea Mungu.
SALA: BWANA, nasema asante kwa nguvu unazonipa kila siku.Yale madirisha madogo ya bahati niliyokuwa nayo sasa yamekuwa milango mikubwa iliyo wazi. Kila kitu kiko sawa nikisimama kwa jina lako. Mungu naomba nizidishie imani hii ili nikadumu kwako daima milele. Katika jina la Yesu naomba na kupokea, Amen.

Wednesday, April 3, 2013

Neno la leo

2The 3:5 “Bwana awaongoze mioyo yenu mkapate pendo la Mungu, na saburi ya Kristo”

TAFAKARI: Ni vizuri kufuata muelekeo mzuri na kuendenda katika zile njia Bwana anatuongoza.Tusichezee mioyo yetu katika kufanya mambo ambayo yanahatarisha na si ya kumpendeza Bwana.Tumuombe Mungu tuzidi kukua katika imani
SALA: Bwana Mungu naomba niwezeshe niendelee kuwa kwenye muelekeo unaotaka niwepo.Nisaidie nisiingie kwenye majaribu ya kuabudu miungu mingine bali wewe. Katika jina la Yesu naomba na kupokea, Amen.

Tuesday, April 2, 2013

Neno la leo

Wakolosai (Kol) 4:6 “Maneno yenu yawe na neema siku zote, yakikolea munyu, mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu”

TAFAKARI: Kuna wakati mtu anakosa maneno yenye busara wakati wa maongezi na wengine. Ama mtu anaweza akose kabisa maneno ya kumwambia mtu aliyefikwa na matatizo kama msiba ama matatizo ya aina yoyote ile. Yatupasa kumuomba Mungu atupe hekima na busara katika kuchagua maneno ya kuongea na wenzetu.

SALA: Bwana Mungu naomba unisaidie niguswe na pendo lako pale ninapotafuta maneno mazuri ya kusemezana na wenzangu. Naomba nipe hekima ya kuweza kutumia kinywa changu kuwabariki wengine nikiongozwa na roho wako mtakatifu. Katika jina la Yesu naomba na kupokea, Amen.

Monday, April 1, 2013

Neno la leo

Yer 29: 13 “Nanyi mtanitafuta na kuniona mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote”

TAFAKARI: Neno la Mungu linasema yeye yule anaemtafuta  kwa moyo wake wote akiamini Bwana atajidhihirisha kwake. Endapo unapitia kwenye jambo gumu lolote, mtafute na umuite Mungu kwa moyo wako wote.

SALA: Mwenyezi Mungu, wewe uliyesema tukutafute maadamu unapatikana, tunakuja mbele zako tukiomba ujidhihirishe kwetu pale tukuitapo. Tumejua ya kwamba wewe pekee ndio kimbilio letu Bwana, hivyo tunaomba usiwe mbali nasi Bwana. Tunahitaji mkono wako wa baraka siku zote za maisha yetu. Katika jina la Yesu tunaomba na kupikea, Amen.