Saturday, January 5, 2013

Tumia talanta yako vizuri kwa mwaka huu 2013

Je mpendwa, umepangaje kutumia talanta yako mwaka huu mpya wa 2013? Utachimba shimo uifukie kama yule mtumishi aliyepewa talanta moja au utaitumia ili izae matunda na kuongeza talanta nyingine ili Bwana atakaporudi akute talanta zimeongezeka.
“Mara yule aliyepokea talanta tano akaenda akafanya biashara nazo, akachuma faida talanta nyingine tano. Vile vile na yule mwenye mbili, yeye naye akachuma nyingine mbili faida. Lakini yule aliyepokea moja alikwenda akafukua chini, akaificha fedha ya bwana wake,” Mathayo 25:16-18
Ni dhahiri ya kuwa yule mtu aliyekuwa na talanta moja alikuwa haendendi katika imani. Kama Bwana angetaka talanta ile ifichwe asingehangaika kumpa yule mtu afiche bali angefanya mwenyewe. Bwana alikuwa anapima imani yake (yule mwenye talanta moja aliyeificha). Kwa kifupi haijalishi ni talanta gani unakuwa nazo wakati wa kuzaliwa bali unafanyia nini hzo talanta zako.
Mpendwa talanta ni kipaji chako ulichobarikiwa na mwenyezi Mungu ambacho unapaswa kukitumia kikamilifu ili sifa na utukufu zimrudie yeye.
Ndugu yangu umekirimiwa kipaji cha pekee ambacho unatakiwa kukitumia vizuri katika kuishi kwako hapa duniani. Kila mwaka unapoisha unatakiwa ufanye tathmini ya kwamba umeitumiaje talanta yako. Je umeweza kuzalisha matunda kwa kwa kutumia talanta uliyoanza nayo mwanzo wa mwaka? Hayo ni maswali ambayo ukipata majibu yake yatakuwezesha kuuanza mwaka mpya vizuri na kuweza kupanga upya jinsi ya kutumia talanta ulizo nazo ili zizae matunda mwisho wa mwaka.
“Akaja yule aliyepokea talanta tano akaleta talanta nyingine tano, akisema, Bwana uliweka kwangu talanta tano; tazama, talanta nyingine tano nilizopata faida. Bwana wake akamwambia, vema, mtumwa mwema na mwaminifu, ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi ingia katika furaha ya bwana wako,” Mathayo 25: 20-21
Talanta yako unaweza kuitumia kanisani, kazini, mashuleni, mashambani ama sehemu mbali mbali za biashara na kwingineko. Ukiwa kanisani kipaji au talanta yako unaweza kuitumia kwa jinsi ulivyobarikiwa, ikiwa ni pamoja na uimbaji (je umejipangaje kuinua kipaji chako hiko na kumtukuza Mungu kupitia nyimbo, kuhubiri neno lake kupitia nyimbo?), huduma za kanisa na jamii inayokuzunguka.
Mbarikiwe!

Friday, January 4, 2013

Heri ya Mwaka Mpya!

Zab 5:1 “Ee Bwana, uyasikilize maneno yangu, ukuangalie kutafakari kwangu”

TAFAKARI: Mungu wetu husikiliza tumuitapo na kutuwezesha kufanya maamuzi katika mambo yetu pale tumshirikishapo.
SALA: Mwenyezi Mungu nasema asante kwa maana umeniwezesha kuuona mwaka huu mpya. Bwana naomba unisaidie katika kuutafakari mwaka huu na uniongoze kuyafikia yale niliyoazimia kwa mwaka huu.Zaidi nizidishie maarifa, busara na hekima ili niweze kuishi vyema na jamii inizungukayo. Katika jina la Yesu naomba na kushukuru, Amen.

 

 

Monday, December 31, 2012

Kwa heri mwaka 2012!

Zaburi 100 "Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote, mtumikieni Bwana kwa furaha, njooni mbele zake kwa kuimba. Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu; ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake,
na tu watu wake, na kondoo wa malisho yake. Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru, nyuani mwake kwa kusifu; mshukuruni, lihimidini jina lake. Kwa kuwa Bwana ndiye mwema, rehema zake ni za milele, na uaminifu wake vizazi na vizazi"

Unapouaga mwaka 2012, hauna budi kumshukuru mungu kwa matendo mengi na makuu aliyokutendea. Umebarikiwa kwa mambo mengi mwaka unaisha leo na inakupasa kumshukuru Mwenyenzi Mungu kwa baraka zote na hata pale ambapo matarajio yako hayakukamilika. Wapo wengi waliotaka kuiona siku na saa kama hii lakini hawapo na sisi. Jihesabie ya kuwa wewe umepata neema ya pekee kwa kuumaliza mwaka huu salama. Kabla ya kulalamika na kulaumu ya kwamba mwaka huu 2012 haukuwa wa matunda kwako, jiulize ni wangapi ambao walishindia mlo mmoja ili hali wewe unakula mara tatu kwa siku na una kazi inayokuingizia kipato, jiulize wakati unalalamika maisha magumu, kuna mwingine anaomba hata tone la mvua lidondoke apate kukinga kinywa chake kwa sababu tu ya kukosa maji, chakula, malazi n.k? Kuna mambo mengi ambayo Mungu amekuepushia hivyo ni vyema kumrudishia sifa na utukufu yeye. Unapoumaliza huu mwaka 2012, mwombe Mungu msamaha pale ambapo ulisahau kumshukuru alipokubariki. Vilevile akusamehe ili uweze kuwasamehe waliokukosea mwaka 2012 na pia usamehewe na uliowakosea ili kesho uanze ukurasa mpya wa mwaka 2013 na baraka pamoja na furaha tele moyoni. Ukianza mwaka mpya na furaha moyoni, hakika kila jambo utakalolifanya mwaka 2013 litabarikiwa.
Mwenyenzi Mungu akupe hekima na busara ya kutafakari mwaka uliopita na kupanga malengo mapya ya mwaka ujao.
Ubarikiwe!