Saturday, January 5, 2013

Tumia talanta yako vizuri kwa mwaka huu 2013

Je mpendwa, umepangaje kutumia talanta yako mwaka huu mpya wa 2013? Utachimba shimo uifukie kama yule mtumishi aliyepewa talanta moja au utaitumia ili izae matunda na kuongeza talanta nyingine ili Bwana atakaporudi akute talanta zimeongezeka.
“Mara yule aliyepokea talanta tano akaenda akafanya biashara nazo, akachuma faida talanta nyingine tano. Vile vile na yule mwenye mbili, yeye naye akachuma nyingine mbili faida. Lakini yule aliyepokea moja alikwenda akafukua chini, akaificha fedha ya bwana wake,” Mathayo 25:16-18
Ni dhahiri ya kuwa yule mtu aliyekuwa na talanta moja alikuwa haendendi katika imani. Kama Bwana angetaka talanta ile ifichwe asingehangaika kumpa yule mtu afiche bali angefanya mwenyewe. Bwana alikuwa anapima imani yake (yule mwenye talanta moja aliyeificha). Kwa kifupi haijalishi ni talanta gani unakuwa nazo wakati wa kuzaliwa bali unafanyia nini hzo talanta zako.
Mpendwa talanta ni kipaji chako ulichobarikiwa na mwenyezi Mungu ambacho unapaswa kukitumia kikamilifu ili sifa na utukufu zimrudie yeye.
Ndugu yangu umekirimiwa kipaji cha pekee ambacho unatakiwa kukitumia vizuri katika kuishi kwako hapa duniani. Kila mwaka unapoisha unatakiwa ufanye tathmini ya kwamba umeitumiaje talanta yako. Je umeweza kuzalisha matunda kwa kwa kutumia talanta uliyoanza nayo mwanzo wa mwaka? Hayo ni maswali ambayo ukipata majibu yake yatakuwezesha kuuanza mwaka mpya vizuri na kuweza kupanga upya jinsi ya kutumia talanta ulizo nazo ili zizae matunda mwisho wa mwaka.
“Akaja yule aliyepokea talanta tano akaleta talanta nyingine tano, akisema, Bwana uliweka kwangu talanta tano; tazama, talanta nyingine tano nilizopata faida. Bwana wake akamwambia, vema, mtumwa mwema na mwaminifu, ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi ingia katika furaha ya bwana wako,” Mathayo 25: 20-21
Talanta yako unaweza kuitumia kanisani, kazini, mashuleni, mashambani ama sehemu mbali mbali za biashara na kwingineko. Ukiwa kanisani kipaji au talanta yako unaweza kuitumia kwa jinsi ulivyobarikiwa, ikiwa ni pamoja na uimbaji (je umejipangaje kuinua kipaji chako hiko na kumtukuza Mungu kupitia nyimbo, kuhubiri neno lake kupitia nyimbo?), huduma za kanisa na jamii inayokuzunguka.
Mbarikiwe!

No comments:

Post a Comment