Friday, February 15, 2013

Neno la leo

Isa 64:3 “Maana tangu zamani za kale watu hawakusikia, wala kufahamu kwa masikio, wala jicho halikuona Mungu, ila wewe atendaye mambo kwa ajili yake amngojaye”

TAFAKARI: Nyakati za sasa mambo mengi yanatokea na pengine tunajiuliza maswali mengi bila kupata majibu. Kuna wakati Mungu atashuka mwenyewe kwa ajili ya kuokoa kile kilichopotea. Muamini yeye na sikiliza neno lake udumu kiroho.
SALA: Bwana Mungu nimekukimbilia wewe nisiaibike milele, nimechagua kukusikiliza wewe siku zote za maisha yangu, hivyo nakuomba mkono wako wa rehema na uokoaji usinipungukie Bwana. Katika jina la Yesu naomba na kupokea, Amen.

Thursday, February 14, 2013

Neno la leo

Yona 2:4 “Nami nikasema, nimetupwa mbali na macho yako; lakini nitatazama tena kukabili hekalu lako takatifu”

TAFAKARI: Kuna kipindi mtu unajitenga na Mungu na kuwa mbali naye lakini kumbuka macho ya Bwana Mungu wetu yanaona kila mahali.
SALA: Asante Mungu kwa maana umeniokoa. Kuna wakati nilikuwa gizani Bwana lakini nilikutumaini wewe nikatazama hekalu lako na kujua ya kwamba bado hujanitupa mwana wako. Wewe usiyelala wala kusinzia naomba uzidi kuniangalia na kunitunza Mungu wangu, Katika jina la Yesu naomba na kushukuru Amen.

Wednesday, February 13, 2013

Nawatakia Kwarema njema!

Rum 2:4 " Au waudharau wingi wa wema wake na ustahimili wake na uvumilivu wake, usijue ya kuwa wema wa Mungu wakuvuta upate kutubu"

TAFAKARI: Hili ni somo zuri kwa ajili ya Jumatano hii ya majivu. Sababu kubwa ya Mungu kukuita kuwa karibu naye ni kutokana na upendo na wema alionao. Mungu anakuita utubu dhambi zako ili uweze kubadilika na kufuata njia mpya katika maisha yako. Katika kipindi hichi cha kwaresma, kutubu inachukua nafasi kubwa sana. Muombe Mungu akusaidie uweze kusamehe na kuwasamehe wale wote waliokukwaza namna yoyote ile.

SALA: Bwana Mungu, wewe mwenye ukarimu na wema wa ajabu, tunaomba utuongoze katika maisha mapya ambayo yanatuelekeza kutubu, ili tukaishi kwa upendo na amani ndani ya mioyo yetu tukijua ya kwamba umetusamehe nasi tumewasamehe waliotukosea, Katika jina la Yesu naomba na kupokea, Amen.

Tuesday, February 12, 2013

Neno la leo

Isa 59:1 “Tazama mkono wa Bwana haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia”

TAFAKARI: Mungu wetu anasikia pale tumuitapo. Mkono wa Bwana ukikugusa kamwe hutapungukiwa na kitu. Muelezo shida zako, furaha yako naye atakuwa pamoja nawe kwa kila kitu.
SALA: Bwana Mungu nakuja kwako kwa unyenyekevu kabisa nikiomba mkono wako wa baraka usinipungukie. Wewe utendaye miujiza kwa wengi, naomba usinipite Bwana kwa maana nakuhitaji sana. Sikiliza kilio cha moyo wangu Bwana na ukanibariki sawa sawa na mapenzi yako. Katika jina la Yesu naomba na kupokea, Amen.

 

Monday, February 11, 2013

My hope is in you Lord!

Neno la leo

Zab 107:20 “Hulituma neno lake, huwaponya, huwatoa katika maangaamizo yao”

TAFAKARI: Mungu ametuma neno lake ili litulishe, lituokoe, lituponye na kutushibisha kiroho.Mwamini yeye nawe utapata kuokolewa. 
SALA: Mwenyezi Mungu, nakushukuru kwa sababu, kwa kupitia neno lako nimepata neema ya msamaha, limeniokoa na nimeweza kudumu katika imani. Naomba uzidi kuniangalia mwanao na uzidi kuwa mponya kwa wale wanaokuamini. Jihidhihirishe kwa mataifa wasiokuamini wakapate kujua kwamba hakuna mkuu kama wewe. Katika jina la Yesu naomba na kupokea, Amen.