Friday, January 18, 2013

Enjoy!


Neno la leo

Zab 37:7 “Ukae kimya mbele za Bwana, nawe umngojee kwa saburi. Usimkasirikie yeye afanikiwaye katika njia yake, wala mtu afanyaye hila”

TAFAKARI: Mungu wetu hupenda wale wasikivu, wapole na wanyenyekevu mbele zake. Furahia maendeleo ya mwenzako na wala usimchukie mtu mwenye hila. Mngoje Bwana kwa saburi na hakika utamuona.
SALA: Mungu wangu na baba yangu, wewe uketiye mahali pa juu sana nakuomba unijalie hekima, busara na maarifa ili niwe na moyo wa kupenda wenzangu pale wafanikiwapo. Niondolee jicho la wivu ndani ya moyo wangu bwana, na unijaze roho wako mtakatifu ili nikaishi kwa kukutegemea wewe. Katika jina la Yesu naomba na kupokea, Amen.

Thursday, January 17, 2013

Neno la leo

Zab 103:8 “Bwana amejaa huruma na neema, haoni hasira upesi,ni mwingi wa fadhili”

TAFAKARI: Mungu wetu ndiye anayeendesha maisha yetu na hakuna chochote kizuiacho nguvu zake za ukombozi kwetu sisi. Hata tunapokosa ama kuenenda katika njia zimchukizazo kwa maksudi kabisa, yeye huokoa nafsi zetu.
SALA: Mungu baba, wewe uliye mwepesi wa hasira nakuja mbele zako nikiomba msamaha kwa yale niliyokutenda. Bwana naomba unisaidie kuyasahau yale ya kale na uniongoze katika kukumbuka yale mambo ambayo yatanisaidia katika maisha ya yangu ya sasa na ya baadae. Nakupenda Bwana, naomba uwe ngome yangu milele, Amen.

Wednesday, January 16, 2013

Neno la leo

Zab 123: 1-2 “Nimekuinulia macho yangu wewe uketiye mbinguni. Kama vile macho ya watumishi kwa mkono wa bwana zao, kama macho ya mjakazi, kwa mkono wa bibi yake. Hivyo macho yetu humwelekea bwana, Mungu wetu, hata atakapoturehemu”

TAFAKARI: Siku zote tunamuangalia Bwana Mungu wetu ili tupate kubarikiwa. Yeye ni macho yetu, nuru yetu na nyota ituangaziayo wakati wa usiku na kutuongoza. Uwepo wake kwetu sisi ni upendo wa ajabu sana.
SALA: Bwana Mungu, nakuinulia macho yangu nikikuomba uwepo wako katika maisha yangu udumu. Wewe umekuwa msaada wangu usiniache kamwe bwana. Takasa njia zangu zote nipitazo na uniepushe na mitego ya muovu shetani. Naomba na kupokea katika jina la Yesu Kristo, Amen.

Tuesday, January 15, 2013

Neno la leo

Zab 145:17-18 “Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote, na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote. Bwana yu karibu na wote wamuitao,wote wamuitao kwa uaminifu”

TAFAKARI: Ukuu wa Mungu ni mkubwa katika kila atendalo nay eye hutimiza ahadi zake. Ni mwenye haki kwa kila kitu afanyacho na ni mwenye kujaa ukarimu wa pekee. Yeye yu karibu kwa wale wote wamtegemeao na kumuita kwa kwa kweli.
SALA: Mwenyezi Mungu, baba wa rehema nyingi na za ajabu machoni pangu, nakushukuru baba kwa maana umenifadhili mimi kwa kiasi kikubwa na umejibu maombi yangu. Naomba univute kwako niwe karibu nawe Bwana wangu na nikutumikie daima milele. Naomba hayo yote nikipokea, Amen.

Sunday, January 13, 2013

Enjoy!

You never dissapoint with your songs Emmy! Mungu azidi kubariki kazi ya mikono yako....

Jiwekee hazina mbinguni

Ni kawaida yetu kujiwekea hazina hasa tunapokuwa na nguvu na tunapofanya kazi ili tusipate shida katika maisha yetu ya uzeeni pale tutakapostaafu.Tunategemea kwamba akiba/hazina tunayojiwekea kidogo kidogo itatusaidia baadae.
Inapotokea mtu anashindwa kujiwekea akiba, kwa hakika maisha yake ya baadae yatakua ya mahangaiko na atakua hana msaada wowote kwa sababu hakuwa na malengo ya baadae katika maisha yake.

Maisha ya mwanadamu hapa duniani katika kujiwekea akiba ya uzeeni/wakati wa kustaafu, hayatofautiani sana na maisha yake ya kujiwekea hazina mbinguni kwa maisha ya milele.
Kwenye biblia maisha ya mwanadamu ni miaka 70 na kwa wale waliobarikiwa wanafikisha miaka hadi 100. Baada ya hapo maisha yake ya milele ni mbinguni.

Biblia inatukumbusha zaidi kujiwekea hazina mbinguni kuliko ya kujiwekea ya duniani pekee, kama tulivyoambiwa maisha ya mwanadamu hapa duniani si marefu. Kwa maana kwamba hazina yako ikiwa mbinguni hakutakuwa na kitu cha kuivuruga tofauti na hazina ya duniani.
“Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi,” Mathayo 6:19-20
Tukumbuke kuwa maisha yetu ya mbinguni ni ya milele, hivyo pale ambapo hazina yetu itakuwepo ndipo na mioyo yetu itakapokuwapo. “kwa kuwa hazina yako ilipo ndipo utakapokuwapo na moyo wako” Mathayo 6:21

Ufanyeje ili ujiwekee hazina mbinguni?
Kujiwekea hazina mbinguni ni kufanya yale yote tuliyoagizwa na Kristo Yesu ili kurithi ufalme wa mbinguni. Baadhi ya mambo tunayopaswa kufanya ni kuzishika amri kumi za Mungu, na kutenda yale yote yanayompendeza mwenyezi Mungu.
Kwenye kitabu cha Marko 10 tunaonyeshwa ile hadithi ya mtu mmoja mwenye mali nyingi alipomkimbilia Yesu na kumuliza mwalimu mwema nifanyeje ili nipate kuurithi uzima wa milele? Yesu akamueleza juu ya kuzishika amri za Mungu na kuuza mali zake ili awasaidie maskini na aweze kupata nafasi ya kumfuata Yesu kwa kujiwekea hazina mbinguni.

“Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, umepungukiwa na neno moja. Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini nawe utakuwa na hazina mbinguni, kasha njoo unifuate,” Marko 10:21
Yesu anatukumbusha kuwa mali tunazochuma duniani zisiwe kizuizi cha kujiwekea hazina mbinguni na kumfuata Yesu.
Mpendwa msomaji swali tunalokumbushwa leo hii ni hazina yako unaiweka wapi?

Mbarikiwe!