Sunday, January 13, 2013

Jiwekee hazina mbinguni

Ni kawaida yetu kujiwekea hazina hasa tunapokuwa na nguvu na tunapofanya kazi ili tusipate shida katika maisha yetu ya uzeeni pale tutakapostaafu.Tunategemea kwamba akiba/hazina tunayojiwekea kidogo kidogo itatusaidia baadae.
Inapotokea mtu anashindwa kujiwekea akiba, kwa hakika maisha yake ya baadae yatakua ya mahangaiko na atakua hana msaada wowote kwa sababu hakuwa na malengo ya baadae katika maisha yake.

Maisha ya mwanadamu hapa duniani katika kujiwekea akiba ya uzeeni/wakati wa kustaafu, hayatofautiani sana na maisha yake ya kujiwekea hazina mbinguni kwa maisha ya milele.
Kwenye biblia maisha ya mwanadamu ni miaka 70 na kwa wale waliobarikiwa wanafikisha miaka hadi 100. Baada ya hapo maisha yake ya milele ni mbinguni.

Biblia inatukumbusha zaidi kujiwekea hazina mbinguni kuliko ya kujiwekea ya duniani pekee, kama tulivyoambiwa maisha ya mwanadamu hapa duniani si marefu. Kwa maana kwamba hazina yako ikiwa mbinguni hakutakuwa na kitu cha kuivuruga tofauti na hazina ya duniani.
“Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi,” Mathayo 6:19-20
Tukumbuke kuwa maisha yetu ya mbinguni ni ya milele, hivyo pale ambapo hazina yetu itakuwepo ndipo na mioyo yetu itakapokuwapo. “kwa kuwa hazina yako ilipo ndipo utakapokuwapo na moyo wako” Mathayo 6:21

Ufanyeje ili ujiwekee hazina mbinguni?
Kujiwekea hazina mbinguni ni kufanya yale yote tuliyoagizwa na Kristo Yesu ili kurithi ufalme wa mbinguni. Baadhi ya mambo tunayopaswa kufanya ni kuzishika amri kumi za Mungu, na kutenda yale yote yanayompendeza mwenyezi Mungu.
Kwenye kitabu cha Marko 10 tunaonyeshwa ile hadithi ya mtu mmoja mwenye mali nyingi alipomkimbilia Yesu na kumuliza mwalimu mwema nifanyeje ili nipate kuurithi uzima wa milele? Yesu akamueleza juu ya kuzishika amri za Mungu na kuuza mali zake ili awasaidie maskini na aweze kupata nafasi ya kumfuata Yesu kwa kujiwekea hazina mbinguni.

“Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, umepungukiwa na neno moja. Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini nawe utakuwa na hazina mbinguni, kasha njoo unifuate,” Marko 10:21
Yesu anatukumbusha kuwa mali tunazochuma duniani zisiwe kizuizi cha kujiwekea hazina mbinguni na kumfuata Yesu.
Mpendwa msomaji swali tunalokumbushwa leo hii ni hazina yako unaiweka wapi?

Mbarikiwe!

No comments:

Post a Comment