Saturday, December 15, 2012

Kwa nini Mungu alimtaka Ibrahimu amtoe Isaka kama sadaka?

Waeb 11:17-19 Kwa imani Ibrahimu alipojaribiwa, akamtoa Isaka awe dhabihu; na yeye aliyezipokea hizo ahadi alikuwa akimtoa mwanawe, mzaliwa pekee, naam yeye aliyeambiwa, Katika Isaka uzao wako utaitwa, akihesabu ya kuwa Mungu aweza kumfufua hata kutoka kuzimu, akampata tena toka huko kwa mfano”  Huu ni utoaji kwa sura ya mtoaji. Biblia inaandika kitu gani kilimsukuma Ibrahimu kutoa sadaka kutoka kwenye sababu ya Ibrahimu.  Mwanzo 22:7-8 “Isaka akasema na Ibrahimu baba yake, akinena, Babangu! Naye akasema, Mimi hapa mwanangu. Akasema, tazama moto upo, na kuni zipo, lakini yuko wapi mwana-kondoo kwa sadaka ya kuteketezwa? Ibrahimu akasema, Mungu atajipatia mwana-kondoo kwa hiyo sadaka mwanangu. Basi wakaendelea wote wawili pamoja,” Isaka aliuliza hili swali kwa sababu alishawahi kumsindikiza baba yake kutoa sadaka wakiwa na mwana-kondoo. Sasa ameuliza asijerudishwa baadae kumleta mwana –kondoo ili hali anajua safari ni ndefu. Ibrahimu akamwambia Mungu atajipatia mwana-kondoo kwa hiyo sadaka, maana yake sadaka nitakayotoa itazaa mwana-kondoo.

Kwa jicho la Mungu, alikuwa anataka nini? Mwanzo 22: 1-2 “Ikawa baada ya mambo hayo Mungu alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema mimi hapa. Akasema, umchukue mwanao, mwana wako wa pekee umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmoja wapo nitakaokuambia,”
Kwa lile neno “Mungu alimjaribu” tunaweza kusema Mungu alimpa mtihani. Jaribu ni jambo linalokuweka njia Panda ya kufikia uamuzi utii unachoambiwa au usitii. Mtihani ni tukio linalopima uwezo wako wa kustahimili na kuyaweza yaliyoko mbele yako katika ngazi inayofuata ya maisha yako.
Wakati Mungu anamuambia Ibrahimu amtoe Isaka kama sadaka ya kuteketezwa, hakuwa na shida na Isaka. Alikuwa na shida na Ibrahimu. Mungu alimpa Ibrahimu maagizo kutaka kujua kama yuko tayari kwa ngazi inayofuata. Yaani kama yuko tayari kufanya kazi ya Mungu anayotaka afanye. Na halikuwa jambo jepesi kwa Ibrahimu. Somo juu ya mtihani huu lilikuwa nini ? Hapa tumepewa somo Mwanzo 22:12Akasema usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno, kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee”
Mungu alimuambia Ibrahimu sasa najua,ya kwamba wewe ni mcha Mungu. Mungu alikuwa anampa mtihani Ibrahimu kwa njia ya sadaka ili kucheki kiwango chake cha Uchaji (kumcha Bwana). Ni wachache sana wakitoa sadaka wanajifunza uchaji. Wengi wanatoa sadaka kwa kutegemea kupata in return. Mungu akikutana na sadaka yako cha kwanza anaangalia Imani yako.
Mbarikiwe!

Friday, December 14, 2012

Ee Mungu tupe Amani....

Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu. Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, kando ya maji ya utulivu huniongoza. Hunihuisha nafsi yangu; na kunio­ngoza katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, sitaogopa ma­baya; kwa maana wewe upo pamoja nami, gongo lako na fimbo yako vyanifariji. Waandaa meza mbele yangu, ma­choni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, na kikombe changu kinafurika. Hakika wema na fadhili zitanifuata siku zote za maisha yangu; nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (ZAB 23:1-6).
Tukiwa katika kipindi cha majonzi kutokana na tukio la kusikitisha la jana Ijumaa lililotokea katika shule ya elementary ya Sandy Hook huko Newtown,Connecticut,(USA)ni maswali mengi tunayojiuliza kwa nini mambo haya ya kusikitisha na kutisha yanatokea hasa kwa watoto wa kati ya umri wa miaka 5 na 10. Ni kipindi kigumu hasa kwa wazazi ambao huwa wanawaaga watoto asubuhi wakienda shuleni na wakitegemea kwamba watakuwa salama siku nzima. Watoto wadogo huwa na mategemeo mengi ya maisha ya mbeleni na hasa katika kipindi hiki tunachokaribia sikukuu ya kukumbuka kuzaliwa kwa mwokozi wetu Yesu Kristo. Ni jambo la kusikitisha mategemeo na ndoto zao zilivyokatishwa ghafla na matukio ya duniani ambayo mengi yanasababishwa na kutokuwa na upendo na amani. Pamoja na tukio la jana, bado tunakumbushwa kwamba bwana ndiye mchungaji wetu na atatupitisha katika majaribio mengi ambapo wakati mwingine tulifikiria kukata tamaa. Tuendelee kumtegemea Mwenyezi Mungu naye atatupitisha katika vipindi vyote vigumu na mwisho tutakaa naye milele. Zaidi ya yote, tupendane sisi kwa sisi kama alivyotupenda yeye na pia tuwe na amani.
Kwa kumalizia, tunaomba Mwenyenzi Mungu azifariji na kuzipa nguvu familia za wale wote waliopoteza maisha katika tukio la jana. Pia awapumzishe mahali pema watoto wote na watu wazima waliopoteza maisha yao jana. Zaidi awanyooshee mkono wa uponyaji majeruhi wote kwa uponyaji wa haraka.

 

 

Pass me not O gentle saviour


Thursday, December 13, 2012

Neno la leo

“Basi ni vivi hivi wakati huu wa sasa yako mabaki waliochaguliwa kwa neema. Lakini ikiwa ni kwa neema, haiwi kwa matendo tena au hapo neema isingekuwa neema.” Warumi 11:5-6
Tafakari: Matendo hayatuokoi bali neema hutuokoa. Mungu pekee ndiye atakayetuokoa na hivyo basi haina budi umkiri na kumwamini ndiyo wokovu unaingia halafu matendo yanafuata.
Sala: Mwenyezi Mungu, nasema asante kwa maana umeniokoa kwa damu ya thamani ya mwana wako Yesu Kristo. Naomba uyatawale maisha yangu, nielekeze katika kujua kuufanyia kazi wokovu wangu ili nipate neema yako. Naomba mapenzi yako yatimizwe katika hilo. Amen
Ubarikiwe!

 

Wednesday, December 12, 2012

Neno la leo


Zab 133:1Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza; Ndugu wakae pamoja kwa umoja
Tafakari: Kama neno linavyosema Mungu anapendezewa na watu wakiishi pamoja kwa upendo na amani.Tunajua ya kwamba umoja ni nguvu na utengano ni dhaifu. Hivyo hatuna budi kushirikiana kwa kila jambo pale ambapo mwenzako, jirani ama ndugu yako anahitaji uwepo wako.
Sala: Mungu Baba, naomba uniepushe na ndimi zenye kuleta ugomvi, nipe moyo wa kupenda kushirikiana na jamaa zangu ili nikaishi kwa amani na jamii inizungukayo, na zaidi nikikuomba uimarishe upendo kati ya ndugu na ndugu. Naomba hayo kupitia Kristo Yesu, Amen.
Siku njema!
 

Bwana umenichunguza


Monday, December 10, 2012

U raise me up!


Neno la Leo

Zaburi 56:4 “Kwa msaada wa Mungu nitalisifu neno lake. Nimemtumaini Mungu, sitaogopa, Mwenye mwili atanitenda nini”
Tafakari: - Mungu atusaidie kumwamini, kumtegemea na kumwogopa yeye siku zote za uhai wetu.
Sala:- Mwenyezi Mungu tunasema asante kwa kuwa wewe umekuwa kimbilio letu na ngome yetu kila tunapokuhitaji. Tunaomba uzidi kutuongoza na kutuimarisha katika neno lako siku zote tukaishi kwa kukutegemea wewe na kukuamini.  Tunaomba hayo kupitia mwanao mpendwa Yesu Kristo, mpatanishi na mwokozi wetu, Amen.
Mbarikiwe!