Katika Biblia kazi imeonekana kwa sehemu kubwa na hii inaonyesha
umuhimu wake jinsi ulivyo. Ni dhahiri kila mmoja wetu anajua umuhimu wa kazi
katika maisha ya kila siku ya mwanadamu. Biblia inaonyesha pia ni kwa namna
gani mtu ambaye hafanyi kazi atakavyoishi.
Kitabu cha Waraka wa Pili wa Paulo Mtume kwa Wathesalonike
kinaonyesha wazi kabisa kuwa asiyefanya kazi na asile. Mtu kama huyo asiwe
mzigo kwa wengine kutokana na uvivu wake.
“Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu
tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi asile
chakula” 2Wathesalonike 3:10
Katika yote haya muda ni muhimu sana kwenye kazi. Pasipo kuzingatia
muda basi mtu atajikuta hapati maendeleo kwa sababu hajawekea maanani kipengele
cha muda. Wapo watu ambao wanafanya kazi bila kujiwekea malengo fulani ya
kufikia kwa wakati muafaka walioweka. Nasema hivi kutokana na kwamba utakuta
mtu anafanya kazi ili mradi atimize wajibu wa kuingia ofisini asubuhi na
kumaliza jioni. Tena mwingine anaweza kukuambia anasubiria kwa hamu muda wa
jioni ufike atoke kazini ama sehemu yoyote ya kibarua afanyacho ili hali siku
hiyo hajavuna chochote na muda umeenda.
Ni vyema kujiwekea malengo mazuri katika kazi kwa sababu pia sio
kila anaefanya kazi ana mafanikio. Mtu mwingine utakuta anafanya kazi zaidi ya
moja lakini haoni mafanikio yake, hii ni kwa sababu hajajiwekea malengo katika
kazi yake. Yaani kwa mfano mtu anaweza
kusema anafanya kazi ya kufundisha kwa muda wa miaka kumi ama zaidi na katika kazi hiyo atasave kiasi cha dola kumi
ama zaidi ama elfu ishirini kwa kila malipo atakayopata. Na kiasi hicho atakachohifadhi
kitamsaidia kuendeleza shughuli nyingine
za kumletea maendeleo.
Kipengele cha muda ni muhimu sana katika kuleta maendeleo. Hata
katika Biblia inatuonyesha jinsi Mungu alivyofanya kazi yake na kumaliza kwa
wakati. “Na siku
ya Saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya, akastarehe siku ya Saba,
akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya” Mwanzo 2:2
Sasa kama mtu atakuwa mvivu na muda unazidi kusonga mbele ni
hakika maisha yake yatakuwa ya kuhangaika. Muda ukisogea mbele kamwe haurudi na
umri wako unazidi kuongezeka. Swali la kujiuliza ni kwamba je, muda wako unautumia vizuri? Pengine una
wazo la biashara ya aina fulani unataka kuianza na unaona ni vyema
kumshirikisha rafiki yako akushauri, na labda atakubali kukushauri na katika ushauri
huo itawekwa mbegu ya LAKINI!!! Kwa maana kwamba lakini biashara hiyo unayotaka
kufanya haina faida kabisa, tena hasara ni kubwa kuliko faida. Basi kama wewe
ni mtu ambaye unapenda kusikia vitu positive tu ni hakika utakwama katika
kuanzisha biashara hiyo. Na kila saa maneno ya kukukatisha tamaa ndio yatakujia
kila mara na hapo unajikuta unashindwa kutimiza ndoto yako. Cha ajabu
utashangaa mtu Yule yule aliyekushauri kutoanzisha hiyo biashara yeye ndo
anaifanya, matokeo yake unabaki kulalamika huku muda unazidi kwenda. Tangu una
miaka 25 unawaza kufungua kampuni yako ya ukandarasi mpaka unafika miaka 40
bado unaendelea na ndoto yako bila kuamua kuchukua hatua.
Ni muhimu kuelewa kuwa sio kila ndoto yako itakubaliwa na watu,
la hasha lazima kuna kupingwa hata na watu wako wa karibu. Kama unaifahamu
huduma yako ni muhimu kuifanyia kazi pengine wewe ni fundi muwashi, mwanamuziki
ama mpishi jibiidishe katika huduma yako na Mungu atakubariki.
Vifungu vingine vya kusoma kuhusu kazi ni “KUTOKA 5: 9, 13,
1WAKORINTHO 3:12
MAHUSIANO
NI KAZI KATIKA FAMILIA
Kuwa na mahusiano mazuri na watu wa familia yako nayo ni sehemu
muhimu ya kazi. Kuna watu tangu waanze kufanya kazi zao pengine ni mwaka wa
tano hawajawahi kuwasaidia ndugu wanaowazunguka.
Ni vyema kuwasaidia ndugu ambao unadhani wanahitaji msaada nawe
utabarikiwa katika kazi yako. Na sio ndugu tu, bali kuna watu wenye shida mbali
mbali nao wanahitaji msaada. Naomba pia nieleweke sio tu watu wanaohitaji
msaada, wazazi ni sehemu kubwa ya baraka haijalishi wanahitaji msaada ama la
cha muhimu ni kwamba unawasaidiaje wazazi wako. Ni baraka kuwakumbuka wazazi au
walezi wetu kwa zawadi yeyote. Wanaweza wakawa wamejitosheleza kiuwezo na hawaihitaji
msaada lakini zawadi utakayowapa wataifurahia na kukuombea baraka katika kazi na
maisha yako. Hata kama ni matajiri kiasi
gani, chochote utoacho kwao wataona unawajali nawe utazipata nyingi baraka.
Kuna watu wanafanya kazi na wanapata pesa ya kutosha lakini
haidumu mikononi mwao wanabaki kujiuliza. Ni dhahiri kabisa mtu huwezi pata
maendeleo ya kazi yako kama huwasaidii wale wahitaji hususan wazazi wako ama
walezi.
“Lakini mtu yeyote asiyewatunza walio wake yaani wale
wa nyumbani mwake, hasa ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini,”
1Timotheo 5:8
Ni vyema ukakaa na kujiuliza hasa watu ambao wako mbali na familia
zao, ni kwa muda gani umewakumbuka ndugu zao wa mbali na kuwasaidia.
Jumapili Njema!