Saturday, March 16, 2013

Neno la leo

Mk 6:34 “Naye aliposhuka mashuani, akaona mkutano mkuu, akawahurumia; kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji; akaanza kuwafundisha mambo mengi”

TAFAKARI: Neno liko wazi linasema Yesu aliwahurumia wale makutano. Wale watu walio kuwepo kwenye mkutano walikuwa na matatizo mengi ambapo kwa hali ya kawaida hata wangefanya matangazo ama kampeni zozote matatizo hayo yasingekwisha kuelezewa. Hata sasa tunaonyeshwa kwamba huruma yake ni muhimu sana na inapita vitu vyote, zaidi ya yote yeye atakuwa pamoja nasi popote tutakapoenda.

SALA: Bwana, kwa huruma yako tunaomba utusaidie kama ulivyowasaidia wale makutano uliowaona. Tufundishe neno lako na mambo mengi tusiyoyajua kwa maana hakuna mchungaji wa pekee kama wewe. Tunaomba hayo kwa jina lako takatifu, Amen.

 

Friday, March 15, 2013

Usikate tamaa ipo siku utayashinda majaribu na mateso yote...

Neno la leo

Mt 15:14 “Waacheni hao ni viongozi vipofu wa vipofu. Na kipofu akimuongoza mwenzake watatumbukia shimoni wote wawili.

TAFAKARI: Katika maisha ya kawaida tunahitaji vingozi wanao ona. Kiongozi asiyeona vizuri bila shaka huyo ataleta matatizo. Kama tukiwa wenye busara, tunamfuata Kristo kwa sababu yeye huona vizuri zaidi. Na kwa ajili yake wale wenye kuona anawapa sababu ya kwamba yeye ndiye kiongozi mkuu na hakuna wa kufanana nae.
SALA: Bwana Yesu, tunaomba tusiwe vipofu wa upofu wa wale wanaotuongoza isivyo. Tunaomba kwa ajili ya kuona na usalama katika maisha yetu. Katika jina la Yesu tunaomba na kupokea, Amen.

Thursday, March 14, 2013

Neno la leo

Mt 17: 1 “Na baada ya siku sita, Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo na Yohana nduguye, akawaleta juu yam lima mrefu faraghani”

TAFAKARI: Baadhi ya hadithi za Yesu zinaonyesha ukweli wa mambo yajayo. Kila mara tunaposali, tunaposoma neno la Mungu, ama kutafakari juu ya Imani aliyotupa, tunapata sababu ya kumwamini hasa pale anapotuamuru kumfuata yeye.
SALA: Mungu wetu na Baba yetu, tunataka utuongoze juu ya kilele cha mlima ili tupate uzoefu mkubwa wa kutambua sauti yako utuitapo na kuweza kubadili maisha yetu. Katika jina la Yesu tunaomba na kuamini, Amen.

 

Wednesday, March 13, 2013

Neno la leo

Mt 24:4 “Yesu akajibu akawaambia, angalieni mtu asiwadanganye”

TAFAKARI: Maandiko yanaonyesha Yesu anapatwa na wasiwasi juu ya wanafunzi wake kuhusiana na habari watakazosikia na kuingia katika majaribu ya kufuata viongozi wabaya. Aliwaonya kuhusiana na manabii wa uongo, roho wachafu na matapeli waliodhani wanaweza kuendesha maisha ya baadae.
SALA: Mwenyezi Mungu tunakuomba, utufanye tusiongozwe pabaya, badala yake utupe muongozo wa kuenenda katika njia nzuri. Katika jina la Yesu tunaomba na kupokea, Amen.

Tuesday, March 12, 2013

Neno la leo

Yoh 21:19 “Akasema neno hilo kwa kuonyesha ni kwa mauti gani atakayomtukuza Mungu, Naye akiisha kusema hayo akamwambia, Nifuate”

TAFAKARI: Hata baada ya kutwaliwa kwa Bwana Yesu, tumesikia hili neno nifuate ili kuepukana na mabaya mengi. Matendo na njia zetu za kumfuata Yesu Kristo ni mojawapo ya njia za maisha hususan maisha mapya ambayo hutuongoza kule apendako yeye tuelekee.
SALA: Bwana Mungu, tunaomba utuweke karibu nawe, hasa pale tunapokufuata kwa matumaini ya ufufuo wako. Katika jina la Yesu tunaomba na kuamini, Amen.

Monday, March 11, 2013

Neno la leo

Yoh 13: 36 “Simon Petro akamwambia, Bwana, unakwendapi? Yesu akamjibu, niendako huwezi kunifuata sasa; lakini utanifuata baadaye”

TAFAKARI: Yesu ana ratiba na ajenda yake juu yetu sisi kama tutamfuata yeye na zaidi ya yote anajua akili ya kila mmoja wetu zaidi ya tujitambuavyo wenyewe. Kwa mantiki hii katika somo hili Peter hakujijua lakini Yesu alimjua kwa undani zaidi. Pengine unasita sita kumfuata Yesu sasa, kumbuka yeye anakujua zaidi na ipo siku utamfuata yeye.
SALA: Mwenyezi Mungu, tunaomba utusaidie tujitambue wenyewe na zaidi kufahamu mipango yako juu yetu na ahadi zako kwetu sisi. Katika jina la Yesu tunaomba na kupokea, Amen.