Friday, May 24, 2013

Neno la leo


Flp 2:13 “Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema”

TAFAKARI: Kusudi la Mungu katika maisha yetu ni jema. Mara nyingine ni vigumu kuelewa Mungu anataka nini kutoka kwetu sisi. Tumuombe Mungu atufanye tujue ya kwamba kusudi lake kuu hugusa imani ya wale wanaotuzunguka.

SALA: Mwenyezi Mungu, naomba ufanye kazi katika maisha yangu, nitumie Bwana vile upendavyo kwa maana najua una kusudi kubwa na mimi. Kuna wakati nilikuwa sielewi mambo yanayotokea kwenye maisha yangu, lakini sasa nimejua ya kwamba ulikuwa ukiniongoza kwenye kusudi lako kuu. Asante Bwana kwa kuwa naelewa kuna uzuri wa kusudi lako kuu kutimilika. Naomba hayo na kupokea katika jina la mwanao mpendwa wetu Yesu, Kristo anaeishi na kutawala daima milele, Amen.

Thursday, May 23, 2013

Neno la leo



Yak 4:4 “Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu”

TAFAKARI: Kuna wakati mtu anafikiri anahitaji kufanya jambo fulani akubalike na ulimwengu. Chembe ya kutokujiamini hujiinua na kuona ni vyema afanye yale wengine wayafanyayo kwa kuwaridhisha wao. Tumwamini Mungu kwa maana yeye ndiye rafiki mkuu.

SALA: Bwana, nisamehe pale nilipochagua mambo ya dunia juu yako.Wewe umenifanyia mema sana mpaka nashindwa kuelewa kwanini naingia katika majaribu ya kufwata ya ulimwengu. Nisamehe Bwana,kwa kufuata vitu vya mpito wakati kwako wewe kuna utukufu mkuu. Naomba nirudishe kwako Bwana wangu, katika jina la Yesu Kristo naomba na kupokea, Amen.

Tuesday, May 21, 2013

Neno la leo

Ayu 16:20-21 “Rafiki zangu hunidharau, Lakini jicho langu humwagia Mungu machozi. Laiti angemtolea mtu hoja mbele ya Mungu, amtetee na mwanadamu mbele ya jirani yake”

TAFAKARI: Kuwa na rafiki anayemjua Mungu ipasavyo ni jambo la kumshukuru Mungu. Rafiki mzuri huombea rafiki zake, iwe ni wakati wa raha ama huzuni. Unaweza kupokea baraka kutokana na sala za wengine, hivyo usijidhanie nafsi yako kwa kusema ni kwa nguvu zako mwenyewe na sala zako.
SALA: Bwana, asante kwa maana najua umenipa rafiki anaeniombea. Mara nyingine nakuwa nimetingwa na uchovu wa kazi za kila siku na kujawa na hasira, lakini gafla napokea amani kutokana na juhudi za mwingine. Napatwa na faraja kubwa kujua ya kwamba rafiki yangu anasemezana na wewe juu yangu. Asante Bwana kwa sababu ya rafiki yangu na kwa kuwa sote tuna rafiki aliye wa kweli, ambaye ni wewe.

Monday, May 20, 2013

Neno la leo

Zab 38:15 “Kwa kuwa nakungoja wewe, BWANA, Wewe utajibu, Ee Bwana, Mungu wangu”

TAFAKARI: Kuwa na kiu ya Mungu ni jambo la kumpendeza sana. Na mtu akiwa kwenye hali hiyo hatataka kufanya maongezi ama kupata ushauri kutoka kwa marafiki. Kiu ya moyo wake ni kumuona Bwana kwa maana yeye ndiye mwenye upendo ulio kamili.
SALA: Bwana, mapigo ya moyo wangu yanaenda mbio nikisubiri uwepo wako kwangu. Nimekuita wewe katika nyakati zangu kuu za mahitaji na umejibu. Unanijua sana na kuona yaliyo ndani ya moyo wangu. Ee Bwana, asante kwa rehema zako, asante kwa kusikia vilio vyangu,asante kwa kunipenda jinsi hivi nilivyo, naomba univute kwenye ngome yako na unipe amani ya moyo. Katika jina la Yesu naomba na kupokea, Amen.