Friday, January 11, 2013

Neno la leo

Waefeso 3: 20 “ Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuombayo au tuyawazayo, kwa kadri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu”

TAFAKARI: Ama hakika hakuna mwenye ukuu kama Mungu. Yeye anaweza kukutendea mambo ya ajabu ambayo hata hujafikiria kwa akili zako ungeweza kuyafanya. Hutenda kwa wakati na pindi muda wake unapotimia hakuna awezaye kuzuia na hivyo hatuna budi kumtukuza yeye.

SALA: Mwenyezi Mungu, nasema asante kwa maana matendo yako yashangaza wengi. Nimeuona mkono wako wa baraka kwangu na ninaliinua jina lako na kulibariki milele. Utukuzwe daima na ninakuomba baba mkono wako wa baraka usinipungukie kamwe. Katika jina la Yesu naomba na kupokea, Amen.
Mbarikiwe!

Thursday, January 10, 2013

Neno la leo

Zab 23: 6 “Hakika wema na fadhili zako zitanifuata, siku zote za maisha yangu. Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele,”
TAFAKARI: Yeye atuokoaye hawezi kutuacha wakiwa na wenye upungufu wa pendo lake. Ameahidi wema na fadhili zake zitakuwa pamoja nasi basi haina budi kukaa nyumbani mwake milele.
SALA: Mwenyezi Mungu nasema asante kwa maana nimeona mkono wako Bwana. Wewe ni mwenye wingi wa rehema, upendo na amani. Naomba wema wako na fadhili zako zinifuate siku zote na unitunze katika pendo lako. Zaidi nikiomba nidumu katika Imani na kukaa kwako daima. Katika jina la Yesu naomba na kushukuru, Amen.

 

Wednesday, January 9, 2013

Neno la leo

Zab 23: 5 “Waandaa meza mbele yangu, machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu na kikombe changu kinafurika”
TAFAKARI: Bwana Mungu wetu atapigana kwa ajili yetu na kutuweka huru. Juu ya yote vikombe vyetu vitajaa upendo wake na wema wake kwetu sisi.
SALA: Mungu wetu na baba yetu, asante kwa kuwa umeniokoa, asante kwa maana umeniandalia meza mbele ya watesi wangu na umenipaka mafuta kichwani mwangu. Naomba mafuta haya yanitakase na kuniangazia nuru ya uso wako siku zote za maisha yangu. Katika jina la Yesu naomba nikipokea, Amen.

Mbarikiwe

Tuesday, January 8, 2013

Neno la leo

Zab 23: 3-4 “Hunihuisha nafsi yangu na kuniongoza katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti sitaogopa mabaya, kwa maana wewe upo pamoja nami,gongo lako na fimbo yako vyanifariji”

TAFAKARI: Yeye Mungu anatuambia atatuongoza kwenye haki pale tunapoelekea pasipo. Atatukinga na mabaya kwa kutumia gongo lake na fimbo yake, hakuna lolote litakaloweza kupigana na hivyo.
SALA: Bwana Yesu asante kwa maana wewe umekuwa ngome yangu na msaada wangu kila nikuitapo. Wewe umesema utakuwa pamoja nami nipitapo katika bonde la uvuli wa mauti. Wewe uliyehuisha nafsi yangu naomba usiniache baba, siku zote za maisha yangu nikutumaini wewe. Katika jina la Yesu naomba nikipokea, Amen.

Mbarikiwe!

Monday, January 7, 2013

Zab 23:1-2 “Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu. Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, kando ya maji ya utulivu huniongoza”

TAFAKARI: Ukiwa unamtegemea Mungu kamwe hautapungukiwa na kitu. Yeye ndiyo jibu la kila kitu na atakuweka mahali pazuri na kukukinga na mabaya.

SALA: Bwana Mungu, nakiri ya kwamba wewe ndiye mchungaji wangu na kamwe sitapungukiwa na kitu ukiwa nami.Umenitoa mbali na umeniongoza kwenye njia sahihi, sina budi kusema asante baba. Naomba unishike mkono Mungu wangu, nisirudi nyuma bali nikae kwako milele. Katika Jina la Yesu naomba na kupokea, Amen.
Mbarikiwe!