Friday, February 1, 2013

Neno la leo

Zaburi 63:3 “Maana fadhili zako ni njema kuliko uhai; midomo yangu itakusifu”

TAFAKARI: Fadhili za Bwana ni za milele na hivyo hatuna budi kulitangaza jina lake na kumsifu yeye daima.
SALA: Kitu ninachokipenda katika maisha haya ni mifano ya uzuri wako, wewe utendaye miujiza mikuu siwezi kamwe kuwa na mashaka nawe. Naomba nikuimbie nyimbo za kukusifu na kukuinua wewe Mungu, zaidi ndimi zangu ziinue jina lako Bwana kwa maana hakuna kitu chochote kizuri kitakachoshindana na upendo wako. Katika jina la Yesu naomba na kushukuru, Amen.

Thursday, January 31, 2013

Neno la leo

Yeremia 5:23 “Lakini watu hawa wana moyo wa kuasi na ukaidi; wameasi, wamekwenda zao”

TAFAKARI: Moyo wa kuasi na wenye ukaidi humtenga mtu asiwe karibu na Mungu.
SALA: Mungu wewe uchunguzaye moyo wa kila mtu na kujua tabia zao naomba nimulike Mungu wangu kwa taa yako, nakiri kwamba natakiwa niache tabia yangu hii mbaya, ni nani wa kuniweka huru kama sio wewe Bwana wangu? Niondolee ukaidi ndani ya moyo wangu na zaidi unitenge na maovu mengi ya dunia hii.Asante Bwana kwa maana umeniweka huru. Naomba na kupokea katika jina la Yesu kristo, Amen

 

Wednesday, January 30, 2013

Neno la leo

1Yohana 5:14 “Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia.

TAFAKARI: Mungu husikia pale tumuitapo na tumuombapo kitu. Ni zawadi kubwa pale unapojishusha kwa Muumbaji wetu. Hata zile nyakati ambapo mtu huona kwamba amekata tamaa akilitaja jina la Bwana hujua ya kwamba yeye anasikia.
SALA: Bwana asante kwa kuniskia. Maskio yako, yako wazi kwa moyo wangu huu mhitaji, Umenijibu maswali mengi yaliyo kichwani na moyoni mwangu, hakika nasema asante. Naja mbele zako nikitafuta tumaini lako na majibu yenye baraka. Katika jina la Yesu, naomba na kupokea, Amen.

Tuesday, January 29, 2013

Neno la leo

Mithali 18:22, 24 “Apataye mke apata kitu chema; naye ajipatia kibali kwa Bwana. Ajifanyiaye rafiki wengi ni kwa uangamivu wake mwenyewe; lakini yuko rafiki aambatanaye na mtu kuliko ndugu.”

TAFAKARI: Mke mwema ni rafiki bora kuliko wote na vile vile urafiki wa kweli hauvunjiki upesi wala hautofautishi tajiri na maskini.

SALA: Bwana Mungu asante kwa kunipa mke mzuri uliyemchagua wewe. Naomba ukazidi kuibariki ndoa yetu tukaishi kwa amani na furaha siku zote. Zaidi tunakuomba utupe marafiki wema na ututenge na wale marafiki wabaya. Katika jina la Yesu Kristo naomba na kushukuru, Amen.

Monday, January 28, 2013

Ee Bwana uniinue kwa Imani...


Neno la leo

Mithali 14: 6, 8 “Mweye dharau hutafuta hekima asiipate; bali maarifa huwa mepesi kwa mwenye ufahamu, akili za mwenye busara ni kujua njia yake; lakini upumbavu wa wapumbavu ni udanganyifu”

TAFAKARI: Mtu mwenye kufikiri kwamba anajua mambo yote kamwe hawezi kuwa na hekima ya kweli. Kwa maana hiyo hatakuwa na utambuzi mzuri kuhusu maadili mema ya maisha.

SALA: Mungu wangu naomba utakase ufahamu wangu ili niweze kutambua na kuchuja mema na mabaya. Zaidi nijaze roho wa kujishusha mbele ya macho yako na jamii inizungukayo.Naomba baraka zako ziwe nami daima. Katika jina la Yesu Kristo naomba na kushukuru, Amen.