Friday, February 8, 2013

Neno la leo

Ebr 10:37-38 “Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, yeye ajaye atakuja, wala hatakawia. Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye”

TAFAKARI: Mngoje Bwana kwa matumaini makubwa kwa maana siku zi karibu kama anenavyo kwenye maandiko yake matakatifu. Kama utakuwa ni mtu mwenye imani haba, Mungu hatakuwa na furaha juu yako.
SALA: Mwenyezi Mungu nasema asante kwa maisha haya uliyonipa. Bwana naomba ukanizidishie imani ndani ya moyo wangu nikungoje wewe bila kuchoka, nijaze roho wako mtakatifu aliye msaidizi wa kila aliye mwaminifu ili imani yangu isitereleke. Naomba na kupokea katika jina la Yesu, Amen.

 

Thursday, February 7, 2013

Neno la leo

Gal 5:5 “Maana sisi wa roho tunalitazamia tumaini la haki kwa njia ya imani”

TAFAKARI: Pengine wewe ni mwenye imani haba, muombe Mungu akuongoze katika haki ili uweze kulifikia tumaini jema.Ukiwa unaamini hakika mambo yako mengi yatakuendea vyema. 
SALA: Niseme nini Bwana zaidi ya kushangaa makuu yako mengi,na umeniwezesha katika kufikia malengo yangu mengi. Bwana hata pale ninapokutana na vikwazo vingi, naomba uendelee kunipigania zaidi nikawe mwenye misimamo na kutokata tamaa.  Niimarishe katika kukuamini wewe Bwana kwa maana kwako tu ndo kuna tumaini jema.Naomba na kupokea, Amen.

Wednesday, February 6, 2013

Neno la leo

Ebr 4:13 “Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu”

TAFAKARI: Hakuna kitu ambacho Mungu hawezi kuona kwa mwanadamu. Wakati mwingine mtu anaweza kutenda jambo la kikatili asijue ya kwamba Mungu anamuona, ila tambua ya kwamba Mungu anaona kila mahali.
SALA: Mungu baba, nakuja kwako kwa unyenyekevu nikiomba unisamehe dhambi nilizotenda ambazo machoni pa wanadamu hazifahamiki bali wewe wazitambua. Naomba uniweke huru kwa damu yako ya thamani, katika jina la Yesu naomba na kupokea, Amen.

 

Tuesday, February 5, 2013

Neno la leo

Tito 2:11-12 “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa”

TAFAKARI: Katika misemo ya kawaida kwa maisha yetu tunaposema kitu kumefunuliwa basi jua kina uwezo wa kufunikwa. Mungu ametoa neema kwa wanadamu wote kwa kutupa uhai na hivyo yatupasa kutenda mema, kwa maana ipo siku neema itafungwa na tumeshindwa kutimiza wajibu wetu kwa wakati tuliopewa hakika tutalia.

SALA: Mwenyezi Mungu asante kwa maana umenipa neema kuu machoni pangu. Nipe akili ya kutoweza kuichezea neema hii uliyonipa bure, niwezeshe katika muda wangu huu wa kuishi nikutumikie wewe daima.Naomba na kupokea katika jina la Kristo Yesu, Amen.

Monday, February 4, 2013

Neno la leo

Luka 11:28 “Lakini yeye alisema afadhali, heri walisikiao neno la Mungu na kulishika,”

TAFAKARI: Imetupasa kumwogopa Mungu na kumheshimu,na tusiwakasirishe wazazi wetu, ila tuwatumikie, tuwatii na kuwapenda kwa moyo wote.

SALA: Mwenyezi Mungu, asante kwa upendo wako kwangu, Wewe uliye mzazi wangu wa kwanza nakupenda na naliheshimu neno lako, niwezeshe nizidi kuwaheshimu wazazi wangu ulionipa wewe na wakubwa wangu, katika jina la Yesu naomba na kupokea, Amen.