Friday, May 3, 2013

Neno la leo

Gal 6:10 “Kwa hiyo kadri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio”

TAFAKARI: Kusaidia jamaa ni kitu muhimu sana. Na Mungu ametusaidia kuona katika uzoefu wa maisha yetu ukarimu wa kitu kidogo unavyokuwa muhimu hasa kwa mtu aliyetendewa vyema. Hii inatusaidia kujenga mahusiano mema na watu watuzungukao.
SALA: Bwana naomba niongoze katika kutenda hasa mambo mema. Niongoze kwa watu unaotaka mimi niwatumikie na kuwasaidia na zaidi tengeneza nia safi ndani ya moyo wangu ili niweze kufanya mema kwa ajili ya utukufu wako na si kwa ajili ya kujivunia mwenyewe. Nisaidie niweze kufikia na kuanzisha mahusiano ya kweli na jamaa zangu, nikikutegemea wewe tu. Katika jina la Yesu naomba na kupokea, Amen.

 

Thursday, May 2, 2013

Neno la leo

Zab 25:4-5 “Ee BWANA, unijulishe njia zako, unifundishe mapito yako, Uniongoze katika kweli yako, na kunifundisha. Maana wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu, nakungoja wewe mchana kutwa”

TAFAKARI: Yatupasa kuondoa upofu wetu kimwili na kiroho ili tuweze kuona uzuri wa ngome ngome aliyotujengea Mungu wetu.
SALA: Baba wa mbinguni, wewe uonae yote yanaoyoendelea katika maisha yangu, nafurahi kwa kutambua hili kwa maana napata amani nikikufikiria wewe katika kila hatua ya maisha ninayopiga. Bado nina shauku la kuendelea kujua nini umeniandalia katika maisha yangu ya baadae, na hivyo naendelea kujitoa kwako unitumie upendavyo.  Naomba hayo na kupokea, katika jina la Yesu Kristo, Amen.

Wednesday, May 1, 2013

Neno la leo

1Pet 3:9 “Watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili mrithi baraka”

TAFAKARI: Kuna wakati mtu akikosewa na mwingine hasira ikimpanda huweza kufanya maamuzi mabaya. Wengine huona kwamba mtu akimfanyia baya basi na yeye hulipiza baya. Maandiko yanatuasa kuishi kwa upendo, kuheshimiana na wenye kuhurumiana.

SALA: Bwana Mungu, mara nyingine nakuwa ni mtu wa kuweka kinyongo badala ya kuachia baraka pindi mtu anaponiudhi. Nahitaji msamaha wako Bwana na niponyeshe na hasira yangu hii ya haraka. Naomba nipe uwezo wa kuelewa utakatifu wako kabla kupatwa na tatizo lolote.Bwana haja yangu ni kurithi baraka zako kwa kueneza ukuu wa pendo lako kwetu. Katika jina la Yesu naomba na kupokea, Amen.

Tuesday, April 30, 2013

Neno la leo

Yoh 1:16 “Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema”

TAFAKARI: Neema yake Mungu imetuwezesha wengi kupata mahitaji yetu. Mara nyingine kulazimisha mambo ili kupata mahitaji yetu na kusahau kwamba ipo neema kubwa tu juu yetu.
SALA: Bwana, nikitazama maisha yangu uliyonipa naona baraka zako kubwa. Neema yako imeniruhusu kufikia malengo yangu. Yapo mambo mengi nataka kufanya lakini nimejifunza kusubiri kwa maana wewe hujibu kwa wakati wako. Nitoe kutoka kwenye fikra za wivu, hukumu na uchoyo, kwa sababu nataka kutoshelezwa na neema yako tu pekee. Katika jina la Yesu naomba na kupokea, Amen.

Monday, April 29, 2013

Neno la leo

Zab 119:90 “Uaminifu wako upo kizazi baada ya kizazi, Umeiweka nchi, nayo inakaa”

TAFAKARI: Mungu aliumba ulimwengu na viumbe vyote ambapo kila kiumbe kilikuwa na madhumuni ya uumbaji wake.
SALA: Mwenyezi Mungu, naomba niweze kuendelea kubeba hadithi za utakatifu wako na kusimulia wengine. Uumbaji wako umetukuka na hakika wewe ni mfalme wa wafalme. Naapa kukutukuza wewe mimi na familia yangu kwa maana uzuri wako hauna kipimo kabisa. Naomba BWANA unifanye niwe mtoto wako mwaminifu hata mpaka ukamilifu wa dahali. Naomba hayo yote na kupokea kupitia mwanao wa pekee, Yesu Kristo, Amen.