Friday, March 22, 2013

Neno la leo

Lk 10:3 “Enendeni, angalieni, nawatuma kama wana kondoo kati ya mbwa-mwitu”

TAFAKARI: Tumetumwa na Mungu kutenda mambo yaliyo mema kwa unyenyekevu katika ulimwengu huu wa sasa ambao una kila aina ya vurugu. Na yeye anaahidi kuwa nasi popote pale tutakapokutana na vikwazo. Yeye hawezi kumtuma mtu mahali ambapo hatakuwepo, kwa maana kwamba amekwisha tangulia mahali hapo.
SALA: Bwana Yesu, tunaomba ulinzi wako ili tuweze kujiamini hata pale tunapokumbana na vikwazo vingi.Katika jina la Yesu tunaomba na kupokea, Amen.

 

Thursday, March 21, 2013

Neno la leo

Lk 10:1 “Basi, baada ya hayo Bwana aliweka na wengine, sabini, akawatuma wawili wawili wamtangulie kwenda kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe”

TAFAKARI: Kwaresma ni wakati ambao tunapewa maagizo kuhusiana na vitu tunavyofanya.Yesu hakuwatuma wanafunzi wake ili awatelekeze, la hasha bali aliwafanya wawe wa kwanza. Katika maisha yetu ya kawaida, tunapofanya jambo kwa wasi wasi ama kukata tamaa, tukumbuke kwamba yeye yupo pamoja nasi na ameshatangulia kufanya lile tuwazalo.
SALA: Bwana Yesu, tunaomba utuongoze kwenye njia yako, ikiwa uko mbele yetu ama uko nyuma basi tunajua ya kwamba ni kwa mapenzi yako na kwamba upo nasi siku zote. Katika jina la Yesu tunaomba na kupokea, Amen.

Wednesday, March 20, 2013

Neno la leo

Mk 10:32 “Nao walikuwako njiani, huku wakipanda kwenda Yerusalemu; na Yesu alikuwa akiwatangulia, wakashangaa, nao katika kufuata wakaogopa. Akawatwaa tena wale Thenashara, akaanza kuwaambia habari za mambo yatakayompata”

TAFAKARI: Ni sawa kuwa na hali ya kushangaa na tunaruhusiwa kufanya hivyo. Unaweza fikiria kwamba watu wanaomfuata Yesu hawawezi kushangazwa na kitu chochote. Lakini habari zinaeleza walishangaa na tena hata kuingiwa na uwoga. Nani ambae hatashangaa wala kuogopa akisikia Yesu alivyotabiri kifo chake na hata miongoni mwa wanafunzi wake watamkana?
SALA: Bwana Yesu, tunaomba utuongoze katika safari zetu na utuzidishie nguvu, ondoa hofu ya uwoga ndani ya mioyo yetu. Katika jina lako takatifu tunaomba na kupokea, Amen.

Tuesday, March 19, 2013

Neno la leo

Mt 9:38 “Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake”

TAFAKARI: Wale wanafunzi 12 wa Yesu ndiyo mavuno ya mwanzo. Lakini Yesu aliona kwamba hawatatosheleza kwa kazi yake. Kutokana na kwamba alikuwa mwenye upendo na wengi hivyo kuona haja ya kuendelea kuwaita karibu watu wake ambao wako tayari kumfuata yeye. Yeye ametumia watu aaminio kwamba watakuwa wavunaji wa wengine na hivyo kuwaokoa. Ahadi yake inasema ombeni nanyi mtapewa basi tusikome kuomba na kuonyesha upendo juu ya wengine.
SALA: Ee Bwana wa mavuno, ulituambia tuombe, na sasa tunafanya hivyo Bwana, tukiomba uzidi kutuma wavunaji wako waje kutuokoa katika dhambi. Tunaomba na kupokea katika jina lako takatifu, Amen.

Sunday, March 17, 2013

Kumtii Mungu

Mzazi anapomuagiza mtoto wake afanye jambo fulani, mara nyingi mtoto anapaswa kutekeleza agizo hilo.  Mzazi anategemea mtoto atafanya alivyoagizwa na si vinginevyo kwamba kutakuwa na mabishano ya kwa nini mtoto huyo anatumwa. Mfano huu wa mzazi ni mfano wa agizo ambali halihitaji mjadala kwa maana nyingine ni agizo kamilifu

Pia kuna amri au maagizo ambayo yanahitaji mjadala ambapo ili zitekelezeke. Kwa mfano amri/agizo zinazowekwa na serikali ni zile amri ambazo mara nyingi zinahitaji mjadala. Yaani zitakapotolewa mtu atauliza kwa nini napaswa kutii hii amri? Kisha ataelezwa matokeo ya kutii na kutotii amri hiyo.
Tukija upande wa Baba yetu mbinguni, amri zake na maagizo yake ni sawa na maagizo au amri atoazo mzazi kwa mtoto wake, yaani  hayahitaji mjadala. Kwa maana nyingine amri/ maagizo hayo ni kamilifu.

Ukisoma kitabu cha KUTOKA 20 habari yote inaelezea amri na maagizo Mungu aliyotoa ambayo ni kamilifu. Mungu wetu ametupa amri kamilifu kwamba hataki kuchanganywa na kitu chochote kwa maana yeye ni Mungu mwenye wivu.  Mstari wa 5 unasema  “Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, BWANA, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao”
Wapendwa katika kipindi hiki cha Kwaresma, tunapotafakari kuteswa  kwa BWANA wetu Yesu Kristo, tunatakiwa kuendelea kuzitii amri zake na kufuata maagizo yake bila mjadala kwani amri zake zimekamilika na ni rahisi kuzifuata. Ni amri ambazo hazina maswali ya “KWA NINI?”

Mbarikiwe!