Friday, April 12, 2013

Neno la leo

Rum 15:4 “Kwa kuwa yote yaliyotangulia kuandikwa yaliandikwa ili kutufundisha sisi; ili kwa saburi na faraja ya maandiko tupate kuwa na tumaini”

TAFAKARI: Maandiko matakatifu yameletwa wazi kwetu ili tutambue uzuri na ukuu wa Mungu. Lakini wengine hudiliki kulichanganua neno la Mungu na kusema halina maana, ukweli ji kwamba hawajazama ndani ya Kristo na kuelewa ukweli wa maandiko hayo. Kupitia neno lake watu wengi wamepokea miujiza.
SALA: Bwana Mungu, busara ya mafundisho yako katika neno lako inasema wazi jinsi maisha yangu yaliyobadilika. Naomba nisaidie niweze kudumu katika mafundisho yako ya Biblia, Bwana kwa maana nataka kuwa mwanafunzi wako wa kudumu na niweze kueneza neno la Upendo kupitia mafundisho hayo. Naomba kupitia Mwana wako Yesu Kristo, Amen.

Thursday, April 11, 2013

Neno la leo

Zab 23:5 “Waandaa meza mbele yangu, machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, na kikombe changu kinafurika"

TAFAKARI: Bwana Mungu huwakaribisha wale wote wamwendeao yeye. Pale mtu anapokutana na maadui wenye nia ya kumwangamiza, Yesu yuko pamoja naye chakulani akishibishwa neno la hekima, busara na ukweli.
SALA: Bwana Yesu nasema Asante kwa maana moyo wangu umejawa na Pendo lako kuu. Nikiwa na hofu juu ya adui zangu, nafikiria tu juu ya ulinzi wa nyumba yako ya milele na kujawa na nguvu mpya. Naomba unikinge zaidi dhidi ya maadui zangu na uniangazie nuru ya uso wako daima milele. Katika jina lako takatifu naomba na kupokea, Amen.

Wednesday, April 10, 2013

Neno la leo

Wim 2:11-12 “Maana tazama, kaskazi imepita, Masika imekwisha, imekwenda zake; Maua yatokea katika nchi, wakati wa kupelea umefika, na sauti ya mwigo husikiwa kwetu”

TAFAKARI: Kuna nyakati mtu hupitia misimu ya matatizo mbali mbali na mambo yake yote kuenda mlama. Pengine kwa kila ashikacho hubomoka ama huharibika kabisa. Lakini pindi mlango wa baraka ukifunguka kila kitu huenda sawa.
SALA: Bwana Mungu asante kwa kunionyesha matumaini pale nilipokata tamaa kabisa. Huu ni wakati wangu wa kufurahia matunda yako. Nakushukuru hata kwa mvua na mafuriko yaliyonipata, kwa maana yamenikuza na kunijenga kiakili na hata kuniletea baraka hizi sasa. Asante Mungu kwa upendo wako, Amen.

 

Tuesday, April 9, 2013

Neno la leo

Ebr 1:1-2 “Mungu ambae alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu”

TAFAKARI: Mungu alikuwa na mpango mzuri wa mawasiliano tangu enzi za kale alipowatumia manabii wake. Anajua mambo ya zamani na hata ya baadae yatakayoikumba ulimwengu. Kwa kutambua hilo alimtoa mwanae wa pekee ambae kupitia yeye tutapata kuokolewa.
SALA: Mwenyezi Mungu ulijua ya kwamba watoto wako tunahitaji kusikia sauti yako hata ukapanga mawasiliano mema kati yetu na wewe. Wakati mwingine natamani kama ingekuwa rahisi kuwatambua manabii wako wengine. Lakini kwa kumtoa mwanao Yesu Kristo nimetambua uzuri wako, nimeona na umenijibu maombi yangu. Asante kwa kutoa mawasiliano yaliyo wazi kupitia nguvu za Mwana wako Yesu Kristo, kwa maana kupitia kwake yeye sisi tumepona.

Monday, April 8, 2013

Neno la leo

Mithali 16:9 “Moyo wa mtu huifikiri njia yake; bali BWANA huziongoza hatua zake”

TAFAKARI: Kwa kawaida mioyo yetu inabeba matumaini na mipango yetu ya baadae, lakini mwenye kujua muelekeo wa mipango hiyo ni Mungu pekee. Na mara nyingine tunashindwa kabisa kukamilisha mipango hiyo kwa wakati muafaka hivyo kukata tamaa. Lakini Mungu huwa upande wetu na kutupa nguvu mpya ya kuendelea.
SALA: Asante Mungu kwa kuniwezesha kukaa katika ulinzi wa mipango yako na si ya kwangu pekee. Mara nyingine mambo yanabadilika haraka na ninapoteza mwelekeo, lakini nikipiga hatua ya njia mpya najua unanibeba na kuniinua juu. Asante kwa kuniongoza katika njia nzuri kila siku. Katika jina la Yesu naomba na kushukuru, Amen.