Friday, May 10, 2013

Neno la leo

Eze 33:5 “Aliisikia sauti ya tarumbeta, wala hakuonywa; damu yake itakuwa juu yake; lakini kama angalionywa, angalijiokoa roho yake”

TAFAKARI: Pale mtu akifanya uovu humuambii damu yake iko juu yako. Mungu hapendezwi na kifo cha mwovu, hivyo basi ni vyema kusaidia wenzetu pale tunapoona wanahitaji kuokolewa ama kukosolewa. Tusikazane kujiokoa wenyewe na kuwanyooshea vidole wengine, bali turudishe kondoo wa bwana kundini kwa kusaidia kukosoa wale wanaoenenda njia za uovu.
SALA: Mwenyezi Mungu, nakuja mbele zako nikiomba msamaha pale ambapo nimeenda kinyume na mapenzi yako. Bwana mara nyingine nimejifikiria mwenyewe na kusahau kutenda kazi yako. Nifanye niwe mfano wa neno lako kwa kusaidia kuwaonya wale waangukao. Zaidi nipe nguvu za kusimama imara katika kuitenda kazi yako. Naomba katika jina la Yesu Kristo, Amen.

Thursday, May 9, 2013

Neno la leo

Zab 89:34 “Mimi sitalisahau agano langu, Sitalibadili neno lililotoka midomoni mwangu”

TAFAKARI: Yote Mungu aliyoyaahidi kwako yatatimia. Yeye ni mwaminifu wa ahadi zake, hivyo unapoamka asubuhi ya leo neno hili likutie nguvu na kukupa ujasiri wa kumwambia shetani leo ni mwisho wa uongo wake katika maisha yako.
SALA: Mwenyezi Mungu nasema asante kwa kunipa nguvu na ujasiri wa kushinda mipango ya ibilisi shetani. Nakataa roho za kukata tamaa na kushindwa, nakataa roho za kiburi, fitina na majivuno. Asante Bwana kwa maana nimeona ahadi zako zikitimia kwangu. Nakushukuru Bwana kwa maana hujaniacha na unisamehe pale ambapo niligeuza uso wangu mbali na macho yako. Katika jina la Yesu naomba na kupokea, Amen.

Wednesday, May 8, 2013

Neno la Leo

Yak 3:17 “Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki”

TAFAKARI: Mtu mwenye hekima huonekana machoni pa watu. Vivyo, hivyo mtu mwenye fitina, mnafiki huonekana wazi pia. Inatupasa kuomba hekima toka kwa Mungu ili tuweze kuishi vyema na jamaa zetu na zaidi ya yote turithi ufalme wa mbinguni.
SALA: Mwenyezi Mungu, wewe uliyesema hekima itokayo kwako ni ya Amani na ni safi yenye upole, naomba nizidishie hekima hiyo ili niweze kushinda hila za mwovu shetani.Nakuomba unimiminie mafuta yako ya baraka uondoe chembe chembe yoyote ya kiburi, unafiki na fitina ndani ya moyo wangu. Nifanye niwe wako Bwana, katika jina la Yesu Kristo naomba na kupokea, Amen.

Tuesday, May 7, 2013

Neno la leo

Rum 13:8 “Msiwiwe na mtu chochote, isipokuwa kupendana; kwa maana ampendaye mwenzake ameitimiza sheria”

TAFAKARI: Upendo ni tunda pekee Mungu alilotuachia. Hatuna budi kupendana kwani kinyume na kuhakikisha wale tuwapendao wako karibu na Mungu.
SALA: Mwenyezi Mungu, naomba Ufunuo wa mahusiano mapya na familia yangu na marafiki zangu. Moyo wangu umejawa na mambo mengi hata mara nyingine nasahau upekee wa kila uhusiano nilio nao kati ya jamaa zangu. Nakushukuru kwa ajili ya watu ulionipa wanaoniletea furaha, wanaoniombea, wanaonifariji na ambao ni mfano wa upendo wako. Naomba uzidi kuimarisha mahusiano yangu na watu hawa ili tudumu katika pendo daima. Katika jina la Yesu naomba na kupokea, Amen.

Monday, May 6, 2013

Neno la leo

Ayu 2:10 “Lakini yeye akamwambia, Wewe wanena kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu anenavyo. Je! Tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi tusipate na mabaya?”

TAFAKARI: Pale mambo yetu yanapoenda kama tulivyopanga hususan kwenye kazi zetu, familia zetu na hata kiroho tunakubali ya kwamba Mungu wetu hajatuacha. Lakini pindi tukipatwa na matatizo basi tunaanza kushuku uwepo wa Mungu na kulalamika kwamba ametuacha.
SALA: BWANA, natambua ya kwamba wewe si Mungu mwenye upendeleo, na huwezi kunipa jaribu nitakaloshindwa kulibeba. Nisaidie niweze kutambua zaidi uwepo wako kwangu, nifundishe rehema zako ili nisiweze kujiuliza mara mbili mbili kuhusu rehema hizo. Zaidi naomba nione kila jaribu nipitalo kama fursa ya kukubali yale yote uliyoniandalia. Naomba na kupokea katika jina la Yesu, Amen.