Friday, March 29, 2013

Neno la leo

Mt 10:38 “Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili”

TAFAKARI: Mtu yeyote ambaye hatatubu dhambi zake na kuacha yale yote maovu yamchukizayo Bwana, itakuwa vigumu kwake yeye kuuona ufalme wa mbinguni.
SALA: Bwana Yesu, tunajua ya kwamba msalaba ni mzito, lakini kwa neema na rehema zako tunaweza kuubeba pamoja na wewe, ili kwamba tuonekane wenye haki ndani yako. Kwa jina lako takatifu tunaomba na kupokea, Amen.

 

Thursday, March 28, 2013

Neno la Leo

1 Yoh 1:7 “Bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote”

TAFAKARI: Tukimfuata Yesu, kamwe hatutakiwi kuyumba ama kupotea. Kwa kumfuata yeye, tunapata kutembea kwenye nuru wakati wa mchana na jioni hata mpaka anapotuongoza kwenye meza yake takatifu tushiriki chakula pamoja naye. Tunatakiwa tuendelee kuombeana na kufarijiana na hivyo tutazidi kung’ara hata kwenye giza na shetani hatopata nafasi kabisa.
SALA: Bwana Yesu, tunaomba utuongoze tutembee kwenye nuru yako, na pia utuongoze kwenye meza yako takatifu tushiriki pamoja nawe chakulani siku zote za maisha yetu. Tunaomba na kupokea katika jina lako takatifu, Amen.

Wednesday, March 27, 2013

Neno la Leo

Mathew 26:58 “Na Petro akamfuata kwa mbali mpaka behewa ya kuhani mkuu, akaingia ndani, akaketi pamoja na watumishi, auone mwisho”

TAFAKARI: Mara nyingine tunajificha tukidhani kwamba Yesu hatuoni. Ama tunaona aibu kujitambulisha kwamba sisi ni watoto wake yaani tunamtumikia Mungu pamoja na Yesu. Petro alijificha ili asikamatwe pamoja na Yesu kwenda kuteswa. Hii inatuonyesha kwamba, hata mmoja wa wafuasi wake wa karibu alimkana, lakini Yesu yeye hakumkana. Basi tudumu katika sala na kuomba neema ya msamaha na tuepukane na majaribu yaliko mbele yetu.
SALA: Bwana Yesu, tunaomba utupe nguvu za kujiamini ili tuweze kutambulika pamoja nawe, na utupe mioyo iliyofunguka ili tufurahie uwepo wako uliopo ndani ya mioyo yetu. Katika jina lako takatifu tunaomba na kupokea, Amen.

Tuesday, March 26, 2013

Neno la Leo

Mk 14:51 “Na kijana mmoja alimfuata, amejitanda mwili wake nguo ya kitani; wakamkamata”

TAFAKARI: Hata yule mfuasi wa mwisho alipoacha kumfuata Yesu, tunaonyeshwa kijana mmoja ambaye hata jina halikufahamika yeye alikuwa anamfuata Yesu, naye akakamatwa kwenda kwenye hukumu ya kifo na Yesu. Tunakumbushwa kuwa upendo wa Yesu uko pale pale na kwa hadithi hii inatuwezesha kubaki ndani ya pendo hilo.
SALA: Bwana Yesu, tunaomba nguvu ya kujiamini kwako na upendo wako vitualike tena ili tuweze tena kukufuata wewe kwenye ile njia ya hukumu ya kifo chako na hata pale utakaposhinda mauti. Katika jina lako takatifu tunaomba na kushukuru, Amen.

Monday, March 25, 2013

Neno la leo

Mk 6:55 “Wakaenda mbio wakizunguka nchi ile yote, wakaanza kuwachukua vitandani walio hawawezi, kwenda kila mahali waliposikia kwamba yupo”

TAFAKARI: Kwenye kipindi hiki cha kwaresma tumesoma habari zionyeshazo watu wakitembea kumfuata Yesu. Tumeona akiwaponya wagonjwa na kuwatangazia mateka uhuru juu ya kutekwa kwao, na hivyo kufanya habari zake njema kuenea kwa haraka. Vivyo hivyo hata tunapokaribia kumaliza kwaresma, yatupasa kuendelea kulieneza neno la Mungu na kuendeleza mwendo kasi wetu katika kutambua yale mazuri yatokanayo na neno lake.

SALA: Bwana Mungu, tunaomba utuwezeshe ili tuweze kukukimbilia wewe na zaidi tusaidie katika njia zote tupitazo ambazo zitatufanya tukufikie wewe. Katika jina la Yesu tunaomba na kupokea, Amen.

Sunday, March 24, 2013

HESHIMA YAKO NI THAMANI KATIKA JAMII

Kila mmoja wetu anapenda kuishi maisha ya uadilifu na ya kuheshimika kwa jamii nzima inayomzunguka. Tunapoteleza kimaadili kwa bahati mbaya au makusudi bado tungependelea heshima yetu kwa jamii ibaki pale pale. Mwenyenzi Mungu ametubariki wanadamu kuwa na hekima na busara katika kufanya maamuzi ambayo yanasaidia kulinda heshima yetu. Ni vizuri kurekebishana kwa heshima pale tunapoona mmoja wetu anapotoka kimaadili ili heshima yake katika jamii ibakie vile vile au kuongezeka zaidi. Inaeleweka katika jamii wanadamu tunaweza kutofautina kimsimamo au kimaamuzi ila tujitahidi isifikie katika hatua ya kuondoleana heshima mbele ya jamii. Haimpendezi Mungu kabisa kuona kwamba mwanadamu anachangia kumwondolea mwanadamu mwenzake heshima yake katika jamii.

Mfano mzuri wa somo la leo tunaupata kutoka katika kitabu cha Mwanzo 9: 20-27 - “Nuhu akaanza kuwa mkulima, akapanda mizabibu; akanywa diva; akalewa; akawa uchi katika hema yake. Hamu, baba wa Kaanani, akauona uchi wa baba yake, akawaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje.  Shemu na Yafethi wakatwaa vazi, wakalitanda mabegani mwao wote wawili, wakaenda kinyumenyume, wakaufunika uchi wa baba yao, na nyuso zao zilielekea nyuma, na wala hawakuona uchi wa baba yao. Nuhu akalevuka katika ulevi wake, akajua mwana wake mdogo alivyomtendea. Akasema, Na alaaniwe Kaanani; Atakuwa mtumwa kabisa kwa ndugu zake. Akasema, Na atukuzwe BWANA Mungu wa Shemu; Na Kaanani awe mtumwa wake. Mungu akamnafisishe Yafethi. Na akae katika hema za Shemu; Na Kaanani awe mtumwa wake.”

Hivyo basi wapendwa, kitabu hiki cha Mwanzo kinatukumbusha ni jinsi gani mwanadamu anavyokwazika pale heshima yake katika jamii inapoondoka. HESHIMA yako katika jamii ndio inayokupa msukumo wa kufanya maamuzi ya busara na ya maendeleo kwako mwenyewe na kwa jamii nzima inayokuzuguka na zaidi kuwa na uhusiano mzuri na baba yetu wa mbinguni. Heshima hiyo ikiondoka, ni vigumu mno kufanya maazuri ya busara na mwisho uhusiano na Mungu wetu unavunjika. Tujitahidi kuwaheshimu wenzetu na vile vile kuwasaidia kurudisha heshima yao pale wanapopotoka bila kukusudia au kwa kukusudia. Hata itakapofikia suluhisho limeshindikana katika maamuzi au misimamo, bado tuna wajibu wa kutunziana heshima. Mwenyenzi Mungu aendelee kutubariki katika kufanya maamuzi ya hekima na busara ili heshima yetu katika jamii iendelee kuthaminika.

Mbarikiwe!