Friday, May 17, 2013

Asante Mnyunyizi wangu...


Neno la Leo

1Kor 14:12 “Vivyo hivyo na ninyi, kwa kuwa mnatamani sana kuwa watu wenye karama za roho, takeni kwamba mzidi sana kuwa nazo ili kulijenga kanisa”

TAFAKARI: Tumuombe Mungu zaidi kwa ajili ya karama za kiroho ili zitusaidie kuinua kanisa lake. Karama hizo ziwe zile zinazomtumikia Mungu kwa ajili ya utukufu wake, kwa maana tunatakiwa kuzirudisha kwakwe na kwa wale wanaomwamini.
SALA: Bwana Mungu, nipatie karama za kiroho ambazo zinakutumikia wewe. Hapo awali katika maisha yangu nilikuwa naomba kwa ajili ya karama zitakazonisaidia kufanikiwa katika maeneo mbali mbali kwneye maisha yangu, lakini sasa nimetambua ya kwamba nahitaji karama za kiroho zaidi. Pia naomba nipe maono ya kutambua karama za wengine ili niweze kuwa chachu ya kuwahimiza wao wakuone wewe katika mwili wa Kristo pekee. Katika jina la Yesu Kristo naomba na kupokea, Amen.

 

 

Thursday, May 16, 2013

Neno la leo

Rum 12:3 “Kwa maana Kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa; bali awe na nia ya kiasi, kama Mungu alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani”

TAFAKARI: Mara nyingine mtu hufanya mambo yake kwa kujitegemea mwenyewe na kujua ni kwa akili zake amefika mahali alipo. Lakini tunasahahu kwamba ni kwa Neema tu pekee tupo hapa tulipo sasa. Neema ya Bwana hutuweka huru kuwa wenyewe na vile vile kuturuhusu kumrudia Mungu. Tunapopata ukweli wa mambo katika maisha yetu ndipo tunagundua jinsi gani ni wadhaifu na kuanza kumlilia Mungu.
SALA: Bwana neema yako imeniwezesha kukurudia wewe, kuwa tegemezi kwako na mwenye moyo wa kushukuru. Asante Bwana kwa maana moyo wangu umejawa na pendo lako, naomba ya kuwa kila hatua ninayopiga iwe na muongozo kutoka kwako. Katika jina la Yesu naomba na kupokea, Amen.

 

Wednesday, May 15, 2013

Neno la leo

Flp (Wafilipi) 4:23 “Neema ya Bwana Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu”

TAFAKARI: Popote tuendapo neema ya Mungu iko juu yetu. Hatuwezi kujificha mbali na neema yake kwa sababu roho mtakatifu hukaa ndani yetu. Mwamini Mungu nawe upate kuona neema hii ya ajabu.
SALA: Bwana Mungu, nasema asante kwa maana umeujaza moyo wangu kwa rehema zako na neema ya msamaha. Ulimwengu haunipi ulinzi na amani, bali napata toka kwako pekee. Nakuandamia wewe tu Bwana kwa maana nataka kufikiria zawadi yako ya neema kupitia maneno na matendo yangu. Naomba nijalie zaidi moyo wa upendo ambao hautasita kueneza neema zako kwa wengine. Naomba kwa ajili ya wengine ambao hawajapata kuona neema hii uwafanye wapate kujua upendo wako na rehema, Katika jina la Yesu Kristo naomba na kupokea, Amen.

Tuesday, May 14, 2013

Neno la Leo

Habakuki 3:2 “Ee BWANA nimesikia habari zako, nami naogopa; Ee BWANA, fufua kazi yako katikati ya miaka, Katikati ya miaka tangaza habari yake; katika ghadhabu kumbuka rehema”

TAFAKARI: “Waonyeshe Mungu” kuna wakati mtu hujikuta akipiga yowe ndani ya kichwa chake pale akiwa amezungukwa na watu wenye mioyo migumu wasioelewa maana ya maisha na kufanya mambo ya ajabu. Hufanya hivyo kwa mfano kama kwamba Mungu ni superman akimuita kuwaokoa, kutuokoa ama kuniokoa.
SALA: BWANA nakuja kwako nikijua wewe ni mwenye nguvu za ajabu, naomba uwaonyeshe watu hawa wasiojua pendo safi na wala msamaha. Badilisha mioyo ya wale walio na nia mbaya siku zote wako macho wazi kutaka kuwaumiza wengine. Ee BWANA sikia sala yangu hii leo, na zaidi nisaidie kuwaonyesha wewe na ukuu wako. Katika jina la Yesu naomba na kupokea, Amen.

Monday, May 13, 2013

Neno la Leo

Mat 6:11 “Utupe leo riziki yetu”

TAFAKARI: Ni vyema tukatoa maisha yetu na kumpa Mungu kwa maana yeye hutoa vitu vingi tena vilivyo vikamilifu. Yeye ni mkate wetu wa maisha na kamwe hawezi kumuacha mtu na njaa.
SALA: Mwenyezi Mungu, wewe uliyenipa maisha na kunipatia kila hitaji langu la kila siku, naja mbele zako nikisema Asante. Pale nilipokuwa sina kitu katika maisha yangu, sasa nimekuwa na mengi ya kushukuru. Hata nitakaponung’unika kwa kuhitaji baraka zaidi, naomba nikumbushe kwamba riziki utoayo kila siku inatosha. Naomba kila iitwapo leo nikufurahishe wewe Mungu wangu. Katika jina la Yesu Kristo naomba na kupokea. Amen.