Friday, May 31, 2013

Neno la leo

Kumb 10: 12-13 “Na sasa, Israeli, BWANA, Mungu wako, anataka nini kwako, ila umche BWANA, Mungu wako na kwenda katika njia zake zote, na kumpenda na kumtumikia BWANA, Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote; na kuzishika amri za BWANA na sheria zake anazokuamuru leo, upate uheri”

TAFAKARI: Jiulize mara ya mwisho ni lini umekaa ukazungumza na Mungu mambo kadhaa kutoka moyoni mwako? Pengine uko kwenye siku ya majonzi ama furaha, ama siku iliyofungamana na yote hayo. Biblia inatuasa kumpenda Mungu wetu ili tuishi kwa amani na tuwe wenye heri duniani.

SALA: BWANA, Mungu nashukuru kwa sababu uko katika maisha yangu. Asante kwa maana siku yangu inaenda kwa jinsi ulivyopanga wewe na nionapo uwepo wako kwangu nafarijika moyoni na kukumbuka ya kwamba ulishaahidi utatembea nami bega kwa bega popote niendapo. Naomba nizidishie moyo huu wa kuamini, kushukuru kuzishika amri zako BWANA. Katika jina la Yesu Kristo naomba na kupokea, Amen.

Thursday, May 30, 2013

Neno la leo

Mit 31:17 “Hujifunga nguvu viunoni kama mshipi; Hutia mikono yake nguvu”

TAFAKARI: Tumuombe Mungu atupe uwezo wa kuzama katika kutekeleza majukumu yetu iwe makazini ama nyumbani. Tuombe kuwa wafanyakazi hodari katika kila Nyanja lakini zaidi tukiweka mitazamo yetu kwake pekee.
SALA: Bwana Mungu, najua kila kitu kipo sawa na haki mbele ya macho yako. Naomba niongoze katika kufanya kazi ambazo unajua zina umuhimu kwako kwa maana nataka kazi zangu zikuridhishe na juu ya yote zinibariki. Naomba hata wakati nikilemewa na majukumu mengi, nisikusahau wewe Mungu bali niwe karibu nawe zaidi. Katika jina la Yesu Kristo naomba na kupokea, Amen.

 

Wednesday, May 29, 2013

Neno la leo



Yak 1:4 “Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno”

TAFAKARI: Kuna wakati mtu anadhan amekabidhi tatizo lake kwa Mungu, lakini mtu huyo huanguka na kutenda dhambi. Yamkini ni kiburi, uzinzi, uongo, uchonganishi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Mtu kama huyo ikiwa hajasimama imara basi kuna wepesi wa kuanguka na kutenda lile tatizo lake. Yatupasa kuomba Mungu atupe nguvu ya kujifunza saburi na kukaa kwake.

SALA: Bwana Mungu, wewe unashangaza kwa matendo yako makuu. Hata pale nilipokukosea, umeendelea kunitimizia mahitaji yangu na tena kwa wakati muafaka, kamwe sijapungukiwa na kitu. Naomba uzidi kufanya kazi ndani ya maisha yangu mpaka hapo ntakapokamilika kwa maana bado ni mchanga sana katika neno lako. Katika jina la Yesu naomba na kupokea, Amen.

Tuesday, May 28, 2013

Neno la leo


Zab 32:7 “Ndiwe sitara yangu, utanihifadhi na mateso. Utanizungusha nyimbo za wokovu”

TAFAKARI: Nyakati ninazopatwa na uwoga huwa najificha. Na kuna wakati nawafwata marafiki ama jamaa ambao naona watanisaidia. Lakini najua wewe ndiye mwenye kuleta tumaini kuu.

SALA: Ee Bwana wangu, niokoe na upweke huu nilio nao kutokana na jambo hili linalonisumbua. Hukusema ya kwamba hautawapa majaribu wanao, kwa maana unatambua ya kwamba ni kupitia majaribu hayo unapima imani zetu juu yako.Nipe nguvu mpya niamke Bwana wangu na moyo wangu ukuimbie nyimbo za wokovu daima. Katika jina la Yesu naomba na kupokea, Amen.