Sunday, October 14, 2012

UMUHIMU WA KAZI KATIKA KUFANIKIWA


Katika Biblia kazi imeonekana kwa sehemu kubwa na hii inaonyesha umuhimu wake jinsi ulivyo. Ni dhahiri kila mmoja wetu anajua umuhimu wa kazi katika maisha ya kila siku ya mwanadamu. Biblia inaonyesha pia ni kwa namna gani mtu ambaye hafanyi kazi atakavyoishi.

Kitabu cha Waraka wa Pili wa Paulo Mtume kwa Wathesalonike kinaonyesha wazi kabisa kuwa asiyefanya kazi na asile. Mtu kama huyo asiwe mzigo kwa wengine kutokana na uvivu wake.

“Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi asile chakula” 2Wathesalonike 3:10

Katika yote haya muda ni muhimu sana kwenye kazi. Pasipo kuzingatia muda basi mtu atajikuta hapati maendeleo kwa sababu hajawekea maanani kipengele cha muda. Wapo watu ambao wanafanya kazi bila kujiwekea malengo fulani ya kufikia kwa wakati muafaka walioweka. Nasema hivi kutokana na kwamba utakuta mtu anafanya kazi ili mradi atimize wajibu wa kuingia ofisini asubuhi na kumaliza jioni. Tena mwingine anaweza kukuambia anasubiria kwa hamu muda wa jioni ufike atoke kazini ama sehemu yoyote ya kibarua afanyacho ili hali siku hiyo hajavuna chochote na muda umeenda.

Ni vyema kujiwekea malengo mazuri katika kazi kwa sababu pia sio kila anaefanya kazi ana mafanikio. Mtu mwingine utakuta anafanya kazi zaidi ya moja lakini haoni mafanikio yake, hii ni kwa sababu hajajiwekea malengo katika kazi yake. Yaani kwa mfano mtu anaweza kusema anafanya kazi ya kufundisha kwa muda wa miaka kumi ama zaidi na  katika kazi hiyo atasave kiasi cha dola kumi ama zaidi ama elfu ishirini kwa kila malipo atakayopata. Na kiasi hicho atakachohifadhi  kitamsaidia kuendeleza shughuli nyingine za kumletea maendeleo.

Kipengele cha muda ni muhimu sana katika kuleta maendeleo. Hata katika Biblia inatuonyesha jinsi Mungu alivyofanya kazi yake na kumaliza kwa wakati.  “Na siku ya Saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya, akastarehe siku ya Saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya” Mwanzo 2:2

Sasa kama mtu atakuwa mvivu na muda unazidi kusonga mbele ni hakika maisha yake yatakuwa ya kuhangaika. Muda ukisogea mbele kamwe haurudi na umri wako unazidi kuongezeka. Swali la kujiuliza ni kwamba  je, muda wako unautumia vizuri? Pengine una wazo la biashara ya aina fulani unataka kuianza na unaona ni vyema kumshirikisha rafiki yako akushauri, na labda atakubali kukushauri na katika ushauri huo itawekwa mbegu ya LAKINI!!! Kwa maana kwamba lakini biashara hiyo unayotaka kufanya haina faida kabisa, tena hasara ni kubwa kuliko faida. Basi kama wewe ni mtu ambaye unapenda kusikia vitu positive tu ni hakika utakwama katika kuanzisha biashara hiyo. Na kila saa maneno ya kukukatisha tamaa ndio yatakujia kila mara na hapo unajikuta unashindwa kutimiza ndoto yako. Cha ajabu utashangaa mtu Yule yule aliyekushauri kutoanzisha hiyo biashara yeye ndo anaifanya, matokeo yake unabaki kulalamika huku muda unazidi kwenda. Tangu una miaka 25 unawaza kufungua kampuni yako ya ukandarasi mpaka unafika miaka 40 bado unaendelea na ndoto yako bila kuamua kuchukua hatua.

Ni muhimu kuelewa kuwa sio kila ndoto yako itakubaliwa na watu, la hasha lazima kuna kupingwa hata na watu wako wa karibu. Kama unaifahamu huduma yako ni muhimu kuifanyia kazi pengine wewe ni fundi muwashi, mwanamuziki ama mpishi jibiidishe katika huduma yako na Mungu atakubariki.

Vifungu vingine vya kusoma kuhusu kazi ni “KUTOKA 5: 9, 13, 1WAKORINTHO 3:12

MAHUSIANO NI KAZI KATIKA FAMILIA

Kuwa na mahusiano mazuri na watu wa familia yako nayo ni sehemu muhimu ya kazi. Kuna watu tangu waanze kufanya kazi zao pengine ni mwaka wa tano hawajawahi kuwasaidia ndugu wanaowazunguka.

Ni vyema kuwasaidia ndugu ambao unadhani wanahitaji msaada nawe utabarikiwa katika kazi yako. Na sio ndugu tu, bali kuna watu wenye shida mbali mbali nao wanahitaji msaada. Naomba pia nieleweke sio tu watu wanaohitaji msaada, wazazi ni sehemu kubwa ya baraka haijalishi wanahitaji msaada ama la cha muhimu ni kwamba unawasaidiaje wazazi wako. Ni baraka kuwakumbuka wazazi au walezi wetu kwa zawadi yeyote. Wanaweza wakawa wamejitosheleza kiuwezo na hawaihitaji msaada lakini zawadi utakayowapa wataifurahia na kukuombea baraka katika kazi na maisha yako.  Hata kama ni matajiri kiasi gani, chochote utoacho kwao wataona unawajali nawe utazipata nyingi baraka.

Kuna watu wanafanya kazi na wanapata pesa ya kutosha lakini haidumu mikononi mwao wanabaki kujiuliza. Ni dhahiri kabisa mtu huwezi pata maendeleo ya kazi yako kama huwasaidii wale wahitaji hususan wazazi wako ama walezi.

“Lakini mtu yeyote asiyewatunza walio wake yaani wale wa nyumbani mwake, hasa ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini,” 1Timotheo 5:8

Ni vyema ukakaa na kujiuliza hasa watu ambao wako mbali na familia zao, ni kwa muda gani umewakumbuka ndugu zao wa mbali na kuwasaidia.
Jumapili Njema!
 

 

No comments:

Post a Comment