Saturday, December 15, 2012

Kwa nini Mungu alimtaka Ibrahimu amtoe Isaka kama sadaka?

Waeb 11:17-19 Kwa imani Ibrahimu alipojaribiwa, akamtoa Isaka awe dhabihu; na yeye aliyezipokea hizo ahadi alikuwa akimtoa mwanawe, mzaliwa pekee, naam yeye aliyeambiwa, Katika Isaka uzao wako utaitwa, akihesabu ya kuwa Mungu aweza kumfufua hata kutoka kuzimu, akampata tena toka huko kwa mfano”  Huu ni utoaji kwa sura ya mtoaji. Biblia inaandika kitu gani kilimsukuma Ibrahimu kutoa sadaka kutoka kwenye sababu ya Ibrahimu.  Mwanzo 22:7-8 “Isaka akasema na Ibrahimu baba yake, akinena, Babangu! Naye akasema, Mimi hapa mwanangu. Akasema, tazama moto upo, na kuni zipo, lakini yuko wapi mwana-kondoo kwa sadaka ya kuteketezwa? Ibrahimu akasema, Mungu atajipatia mwana-kondoo kwa hiyo sadaka mwanangu. Basi wakaendelea wote wawili pamoja,” Isaka aliuliza hili swali kwa sababu alishawahi kumsindikiza baba yake kutoa sadaka wakiwa na mwana-kondoo. Sasa ameuliza asijerudishwa baadae kumleta mwana –kondoo ili hali anajua safari ni ndefu. Ibrahimu akamwambia Mungu atajipatia mwana-kondoo kwa hiyo sadaka, maana yake sadaka nitakayotoa itazaa mwana-kondoo.

Kwa jicho la Mungu, alikuwa anataka nini? Mwanzo 22: 1-2 “Ikawa baada ya mambo hayo Mungu alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema mimi hapa. Akasema, umchukue mwanao, mwana wako wa pekee umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmoja wapo nitakaokuambia,”
Kwa lile neno “Mungu alimjaribu” tunaweza kusema Mungu alimpa mtihani. Jaribu ni jambo linalokuweka njia Panda ya kufikia uamuzi utii unachoambiwa au usitii. Mtihani ni tukio linalopima uwezo wako wa kustahimili na kuyaweza yaliyoko mbele yako katika ngazi inayofuata ya maisha yako.
Wakati Mungu anamuambia Ibrahimu amtoe Isaka kama sadaka ya kuteketezwa, hakuwa na shida na Isaka. Alikuwa na shida na Ibrahimu. Mungu alimpa Ibrahimu maagizo kutaka kujua kama yuko tayari kwa ngazi inayofuata. Yaani kama yuko tayari kufanya kazi ya Mungu anayotaka afanye. Na halikuwa jambo jepesi kwa Ibrahimu. Somo juu ya mtihani huu lilikuwa nini ? Hapa tumepewa somo Mwanzo 22:12Akasema usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno, kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee”
Mungu alimuambia Ibrahimu sasa najua,ya kwamba wewe ni mcha Mungu. Mungu alikuwa anampa mtihani Ibrahimu kwa njia ya sadaka ili kucheki kiwango chake cha Uchaji (kumcha Bwana). Ni wachache sana wakitoa sadaka wanajifunza uchaji. Wengi wanatoa sadaka kwa kutegemea kupata in return. Mungu akikutana na sadaka yako cha kwanza anaangalia Imani yako.
Mbarikiwe!

No comments:

Post a Comment