Friday, December 14, 2012

Ee Mungu tupe Amani....

Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu. Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, kando ya maji ya utulivu huniongoza. Hunihuisha nafsi yangu; na kunio­ngoza katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, sitaogopa ma­baya; kwa maana wewe upo pamoja nami, gongo lako na fimbo yako vyanifariji. Waandaa meza mbele yangu, ma­choni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, na kikombe changu kinafurika. Hakika wema na fadhili zitanifuata siku zote za maisha yangu; nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (ZAB 23:1-6).
Tukiwa katika kipindi cha majonzi kutokana na tukio la kusikitisha la jana Ijumaa lililotokea katika shule ya elementary ya Sandy Hook huko Newtown,Connecticut,(USA)ni maswali mengi tunayojiuliza kwa nini mambo haya ya kusikitisha na kutisha yanatokea hasa kwa watoto wa kati ya umri wa miaka 5 na 10. Ni kipindi kigumu hasa kwa wazazi ambao huwa wanawaaga watoto asubuhi wakienda shuleni na wakitegemea kwamba watakuwa salama siku nzima. Watoto wadogo huwa na mategemeo mengi ya maisha ya mbeleni na hasa katika kipindi hiki tunachokaribia sikukuu ya kukumbuka kuzaliwa kwa mwokozi wetu Yesu Kristo. Ni jambo la kusikitisha mategemeo na ndoto zao zilivyokatishwa ghafla na matukio ya duniani ambayo mengi yanasababishwa na kutokuwa na upendo na amani. Pamoja na tukio la jana, bado tunakumbushwa kwamba bwana ndiye mchungaji wetu na atatupitisha katika majaribio mengi ambapo wakati mwingine tulifikiria kukata tamaa. Tuendelee kumtegemea Mwenyezi Mungu naye atatupitisha katika vipindi vyote vigumu na mwisho tutakaa naye milele. Zaidi ya yote, tupendane sisi kwa sisi kama alivyotupenda yeye na pia tuwe na amani.
Kwa kumalizia, tunaomba Mwenyenzi Mungu azifariji na kuzipa nguvu familia za wale wote waliopoteza maisha katika tukio la jana. Pia awapumzishe mahali pema watoto wote na watu wazima waliopoteza maisha yao jana. Zaidi awanyooshee mkono wa uponyaji majeruhi wote kwa uponyaji wa haraka.

 

 

No comments:

Post a Comment