Zaburi 100 "Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote, mtumikieni Bwana kwa furaha, njooni mbele zake kwa kuimba. Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu; ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake,
na tu watu wake, na kondoo wa malisho yake. Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru, nyuani mwake kwa kusifu; mshukuruni, lihimidini jina lake. Kwa kuwa Bwana ndiye mwema, rehema zake ni za milele, na uaminifu wake vizazi na vizazi"
Unapouaga mwaka 2012, hauna budi kumshukuru mungu kwa matendo mengi na makuu aliyokutendea. Umebarikiwa kwa mambo mengi mwaka unaisha leo na inakupasa kumshukuru Mwenyenzi Mungu kwa baraka zote na hata pale ambapo matarajio yako hayakukamilika. Wapo wengi waliotaka kuiona siku na saa kama hii lakini hawapo na sisi. Jihesabie ya kuwa wewe umepata neema ya pekee kwa kuumaliza mwaka huu salama. Kabla ya kulalamika na kulaumu ya kwamba mwaka huu 2012 haukuwa wa matunda kwako, jiulize ni wangapi ambao walishindia mlo mmoja ili hali wewe unakula mara tatu kwa siku na una kazi inayokuingizia kipato, jiulize wakati unalalamika maisha magumu, kuna mwingine anaomba hata tone la mvua lidondoke apate kukinga kinywa chake kwa sababu tu ya kukosa maji, chakula, malazi n.k? Kuna mambo mengi ambayo Mungu amekuepushia hivyo ni vyema kumrudishia sifa na utukufu yeye. Unapoumaliza huu mwaka 2012, mwombe Mungu msamaha pale ambapo ulisahau kumshukuru alipokubariki. Vilevile akusamehe ili uweze kuwasamehe waliokukosea mwaka 2012 na pia usamehewe na uliowakosea ili kesho uanze ukurasa mpya wa mwaka 2013 na baraka pamoja na furaha tele moyoni. Ukianza mwaka mpya na furaha moyoni, hakika kila jambo utakalolifanya mwaka 2013 litabarikiwa.
Mwenyenzi Mungu akupe hekima na busara ya kutafakari mwaka uliopita na kupanga malengo mapya ya mwaka ujao.
Ubarikiwe!
No comments:
Post a Comment