Saturday, November 17, 2012

UPENDO


1 Yohana 4:16"Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake".
Upendo wa Mungu wetu ni mkuu sana na unapita vitu vingi mno. Hata mtu akianza kuandika leo hii juu ya Upendo wa Mungu wino utakwisha kwa maana ni mkubwa mno hauelezeki. Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa mwana wake wa pekee Yesu Kristo ili kila amwaminie yeye asipotee bali awe na uzima wa milele. Yesu alitufia msalabani kwa ajili ya dhambi zetu, hii inadhihirisha jinsi gani Mungu amempenda mwanae huyo wa pekee afe kwa ajili ya mimi na wewe.
Upendo huleta amani, furaha na faraja. Ndani ya moyo wangu nina amani tele na furaha. Nampenda Kristo kwa sababu ameniokoa kwa damu ya thamani. “Utanijulisha njia ya uzima; mbele za uso wako ziko furaha tele; na katika mkono wako wa kuume mna mema ya milele,” Zaburi 16:11
Upendo hutoka kwa Mungu na kila mwenye upendo ni mtoto wa Mungu. “Twampenda yeye kwa sababu yeye alitupenda kwanza na akaichukua mioyo yetu kwake mwenyewe” 1 Yohana 4:19. Hakuna kitu muhimu katika maisha ya binadamu kama UPENDO.Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabiri; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote. Upendo haupungui neno wakati wowote - 1Wakorintho 13:4-8
Mtu mwenye kukosa upendo huyo hayuko ndani ya Kristo na siku zote huwa na chuki. Hata katika Biblia imeonyeshwa kwamba mtu akisema anampenda Mungu ana anachukia ndugu yake ni muongo. “1Yohana 4:20 Mtu akisema, nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona”.
Si vyema kuchukiana juu ya mambo madogo madogo.Huna sababu ya kumchukia ndugu yako sababu ya wivu ama kumchukia jirani yako sababu ana maendeleo ambayo wewe huna. Hata amri ya pili inasema mpende jirani yako kama nafsi yako, sasa iweje unamchukia jirani ama ndugu yako wa kuzaliwa naye. Hii haimpendezi Mungu na yakupasa kumrudia yeye na kujifunza neno lake ndipo utaelewa maana halisi ya upendo.  Tuzishike amri za Mungu na kukaa katika pendo lake.
Upendo haujalishi umpendaye ni tajiri ama maskini. Kuna watu ambao huchagua watu wa kuwapenda yaani ambao wanaona wako kwenye status zao. Huo sio upendo bali ni kutafuta watu ambao unadhani utapata furaha kwa sababu tu pengine anaendesha benzi, anakula sehemu za bei ya juu, anavaa vitu vya bei na vitu vingine vinavyofanana na hivyo.
Tuwe na upendo wapendwa kwa sababu ukiwa na upendo siku zote utakua na amani. Kwa maana mtu mwneye Upendo hulipa mabaya kwa mazuri, kamwe hawi wenye visasi. Mwenye upendo siku zote ni mnyenyekevu mbele za watu na hujali wengine zaidi yake mwenyewe.
Usiruhusu mwanadamu akurudishe nyuma na ukatoka katika pendo. Binafsi tangu niijue Biblia maisha yangu yamekuwa ya furaha sana na amani. Na ndiyo maana nasema maisha yangu ni biblia yangu mahali ambapo napata faraja kila nisomapo. Through biblia nimejifunza nini maana halisi ya upendo, na mambo mengine mazuri.
Tujitunze katika upendo wa Mungu, huku tukingojea rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo kwa kutazamia uzima wa milele. Na haya yote yanapatikana kwa kumuomba roho mtakatifu akuongoze uwe na upendo.
Mimi nawapenda, muwe na Jumapili njema.

No comments:

Post a Comment