Saturday, October 27, 2012

VIFUNGO VYA LAANA


Neno LAANA katika kamusi limetafsiriwa kama ukosefu wa radhi za mwenyezi Mungu, hasira ya Mungu. Au ni apizo atoalo mtu kwa mtu mwingine ili afikwe na ubaya, uovu, msiba au hasira ya Mungu. LAANI  limetafsiliwa kama, shtakia kwa Mungu, au ombea uovu.

Zipo laana nyingi lakini leo ningependa kuzungumzia laana zifuatazo:-

  1. Ukoo/familia:- laana zinazojiendeleza kwenye ukoo hutokana na matokeo ama matunda ya dhambi. Kwa mfano unakuta katika familia husika kuna wengine wana laana za magonjwa sugu kama kansa, kwenye hiyo hiyo familia wengine hawaolewi, wengine wameolewa lakini ndoa hazidumu, wengine hawapati mimba. Familia nyingine utakuta kuna vifo vya ghafla, wanaanza maisha na kufanikiwa na kuwa na mali na biashara kubwa au kazi lakini mwisho wao wanaishia kufilisika na kufa kwa mateso makali.Unatakiwa kuomba maombi ya rehema na toba na lazima utamke kilichofanyika na matokeo yake.  Kwa sababu kila dhambi iliyofanyika ni kutokana na kuwa na miungu mingine. Dhambi inatokea pale mtu anapomwacha Mungu wa kweli na kusikiliza miungu mingine. Sasa unapokosa msaada wa Mungu wa kweli unapata misaada ya miungu inayokusababisha wewe kutenda kinyume na Mungu. “Usiwe na miungu mingine ila Mimi- Kumbukumbu la torati 5:7”
  2. Laana za kulaaniwa na mtu mwingine:- Yawezekana ulikosana na rafiki yako ama mtu mwingine pengine mwalimu wako wa shule akakuchukia na kukulaani. Anaweza kukulaani kuwa na kamwe hutakaa uendelee kwa kila utakalofanya usifanikiwe.
  3. Laana za kujilaani mwenyewe:- Kuna watu hawaridhiki na jinsi walivyo ama niseme viungo vya miili yao, yaani kwa ufupi hawajikubali ama kujiamini. Utakuta mtu analalamika na kusema “aah mimi kwa ufupi huu sidhani kama nitakaa nipate mwanamke mrefu atakaenipenda, ama mwingine atajilaani kwa kusema kamwe hawezi kuwa mtu wa kwanza darasani kwa sababu tu ya mtu fulani nyumbani kwao hajawahi kuwa” Siku zote maneno huumba na kujiumba, kwa maana hiyo yale uyatamkayo mdomoni kwako vivyo hivyo yanafanyika.
  4. Laana ya vitu visivyoisha: Kuna watu wamelaaniwa kwa kila wakigusacho kisiendelee na matokeo yake hujikuta wameanzisha vitu mbali mbali bila hata kimojawapo kukamilika. Mfano mtu anataka kujenga lakini anaishia nusu na kuanza kitu kingine ambacho nacho hakifiki mbali. Nataka kuanzisha biashara ya nguo, atanunua sehemu ya kuuzia nguo lakini hakuna kitakachoendelea. Watu kama hawa ni wale wanaonena kwa midomo lakini hawatekelezi.
  5.  Laana ya kufanya tendo la ndoa na dada yako au kaka yako, baba yako au mama yako
    Kuna mambo mengine sio rahisi hata kuelezea lakini yapo na yanafanyika mtu amelala na Dada yake, mwingine na kaka yake, laana ya Mungu imeagizwa juu
    yao “Kumb 27:22 Na alaaniwe alalaye na umbu lake, binti ya babaye au Binti ya mamae. Na watu wote waseme Amina”

Haya yote yanatokana na UPOFU wa mawazo. Akili ikifungwa mtu hawezi kufanya maamuzi yoyote. Pia akili ikifungwa mtu haoni ugumu wa dhambi. “2Wakorintho 3:14 ila fikira zao zilitiwa uzito. Kwa maana hata leo hivi wakati lisomwapo Agano la kale, utaji uo huo wakaa, yaani haikufunuliwa kwamba huondolewa katika Kristo”. Soma pia Waefeso 4:18

NAVUNJAJE VIFUNGO?
Biblia inapozungumza habari ya watu waliofungwa wapate kufunguliwa, hii ina maana ya kuwa kuna watu wamefungwa chini ya utawala wa nguvu za giza katika ulimwengu wa Roho. Watu hawa wamefungwa kwenye magereza na Ibilisi.
Tutambue ya kuwa Yesu aliposema amekuja kutuokoa hii inamaanisha kwamba kuna mahali ambako tusingeweza kujikwamua wenyewe bila nguvu yake yeye mwenywe kuingia kati yetu.
Aliyahidhirisha haya kwenye kitabu cha nabii Isaya 61:1-2 Roho ya Bwana Mungu i juu yangu kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema, amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao”.
Vunja uhusiano wako na hiyo miungu pamoja na kazi zake na agano lililofanyika kati ya familia au ukoo wako na hiyo miungu. Kila unapotamka mwisho wake sema kwa sababu nimesamehewa. Ipo mistari mingi ya kuvunja maagano lakini mimi nitakupa kifungu hiki cha mstari katika kuvunja maagano na mapoozo ya aina yoyote. “Tena itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa kwa sababu ya kutiwa mafuta” Isaya 10:27
Kifungu kingine ambacho waweza tumia ni kwa kutaja maneno haya wakati wa kuvunja vifungo ama laana “Bwana Yesu, nasimama mbele zako na katika ulimwengu wa roho, kujiachanisha nafsi yangu (Taja jina lako) na vifungo vya kuzimu kwa upande wa baba yangu na mama yangu kwa sababu nimesamehewa.” Endelea vivyo hivyo kwa kutaja, roho na mwili kwa kutumia maneno hayo hayo uponyaji hufanyika katika nafsi, mwili na roho.
Mtegemee Roho Mtakatifu kwa maana atakufundisha mengi ikiwemo kuomba na maagizo ya Yesu. Na kwa kufuata maagizo ya Yesu na kuenenda kwa roho hivyo vifungo vya nafsi vitakwisha. Soma Wagalatia 5:16-25, Luka 22:40-46. Kudumu katika maombi, kuenenda kiroho na kuepuka uovu ni muhimu kwa sababu kwa kufuata misingi hiyo ndipo unafunguliwa vifungo kwa kuombewa ama kwa nguvu inayotenda kazi ndani yako kupitioa roho mtakatifu. Lakini pia ni muhimu kujua ya kwamba sala ya toba pekee haitoshi kumfungua mtu kama ana vifungo na sio imani tu bali na juhudi binafsi ya mtu itasaidia katika kumuweka huru. Wapo watu wanaotaka kupokea miujiza bila ya kuwa na mabadiliko yoyote, ama bila kusoma neno la Mungu na kukua kiroho ama bila kuomba. Wao husubiria siku za maombi, ama mikesha ama makongamano ya maombi ili waombewe kisha baada ya hapo hawajishughulishi katika kukua kiimani.
Kuwa hodari katika Bwana ili upate ulinzi wa Mungu. Waefeso 6:10-11 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu mpate kuweza kuzipinga hila za shetani”
Maana ya kuwa hodari katika Bwana ni kukaa kwenye maombi, kusoma na kulishika neno lake liwe ndani yako, na kutaka kumjua yeye zaidi. Sikuzote Sali kwa bidii katika kupambana na muovu shetani ndo mana tunaambiwa vaeni silaha zote za Mungu ili kuweza kupingana na hila za muovu shetani.

Mbarikiwe na Mungu!

 

5 comments:

  1. Mungu akubaliki somo zuri mno limenibariki na kunipa nguvu dhidi ya nguvu za giza!!

    ReplyDelete
  2. Somo fupi la undani nimejifunza kitu, UBARIKIWE MTUMISHI.

    ReplyDelete
  3. Amen somo nzuri sana navunja laana za familia yangu zinazonifuatilia kwa Jina la Yesu

    ReplyDelete