Sunday, November 25, 2012

JE UNAKUMBUKA KUSHUKURU BAADA YA KUPATA?


Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya bwana, dunia na wote wakao ndani yake (Zaburi 24:1). Mwenyenzi Mungu ametukabidhi mamlaka ya kumiliki vitu vyote vilivyopo duniani, hivyo hatuna budi kumshukuru na kumrudishia yeye sifa.
Mara nyingi watu wanapopata walichoomba kwa Mungu kisha wanasahau kusema asante. Na pengine huweka ahadi kwa Mungu kwamba endapo watajibiwa haja zao basi watatoa kitu fulani ama watafanya jambo fulani kama shukrani kwa Mungu.
Kama ulimuomba Mungu akutimizie kitu chako ama tatizo lako pengine ni kupata mtoto halafu ukaahidi kumtolea sadaka ya pekee Mungu wako basi fanya kama ulivyoahidi pasipo kusahau.
Ahadi unayoweka kwa Mungu ni NADHIRI yako na endapo hujaitimiza Mungu anaihesabia kama dhambi na itakufwatilia maishani mpaka hapo utakapotimiza.
Lakini kuna wale wachache wanakumbuka kusema asante na kutoa shukrani zao pindi wapatapo miujiza yao. Mfano mzuri ni ile hadithi ya wenye ukoma kumi,walipopaza sauti na kuita Ee Yesu, Bwana mkubwa uturehemu. Yesu alipowaona akawaambia enendeni mkajionyeshe kwa makuhani na walipokuwa wakienda walitakasika. Na mmoja wao alipoona amepona alirudi akimtukuza Mungu kwa sauti kuu na kuanguka miguuni mwake akamshukuru. Mtu huyu ameshukuru kwa sababu ameuona ukuu wa Mungu, ameguswa kwa namna ya kipekee.(Luka 17:11-19).
Ni mangapi Mungu wetu anatutendea mambo makubwa na mara nyingine tunashangaa miujiza hiyo lakini tunasahau kumshukuru angalau hata kwa kupiga magoti na kusema asante Mungu.
Kama umeweka nadhiri ya kumtolea Mungu sadaka ya shukrani itimize. Labda niseme maana ya Nadhiri nijuavyo mimi ni sadaka uitoayo kwa kinywa chako mwenyewe. Tukumbuke kuwa mara nyingi Nadhiri hutolewa madhabahuni ambapo ni sehemu takatifu.
Madhabahu ni sehemu ambayo inatunza kumbukumbu kwa kila aliyetamka nadhiri yake.Sasa tujiulize tunapotoa nadhiri zetu bila kuzikamilisha hatuogopi madhabahu ama?
Nakumbuka mafundisho ya Mchungaji Christopher Mwakasege juu ya mfano wa wanandoa wawili waliokuwa wanatafuta mtoto kwa muda mrefu bila mafanikio. Wakawa wamezunguka kila sehemu zenye huduma za maombi. Siku moja wakaenda kusali kwa Mchungaji mmoja kimoyo moyo wakasema ‘Mungu ukitupa mtoto tunaahidi kutoa sadaka yetu kwa Mchungaji huyu na kusaidia kanisa lake. Baada ya muda Mungu akawajibu kwa kuwapatia mtoto. Wale wanandoa wakajisahau na kuendelea na maisha yao kama kawaida. Baada ya kipindi kidogo yule mtoto mdogo akaanza kuugua magonjwa mbali mbali hata madaktari wenyewe wasielewe. Ndipo wakamkumbuka Mungu na kuanza kusali.
Mchungaji Mwakasege alifunuliwa na Mungu ya kwamba watu hao walitoa nadhiri mahali fulani na hawajaitimiza, waulize watakuambia wenyewe. Alipowauliza ndipo walipokumbuka ya kwamba hawakutimiza ahadi yao. Wakatubu na kurudi kwenye Kanisa ambapo walipata muujiza na kutubu dhambi zao na kutoa nadhiri yao. Mungu akawasamehe na mtoto akapona.
Huu ni mfano ambao kwangu mimi ulinigusa kwa namna ya pekee. Sijui wewe mwenzangu Mungu amekutendea mangapi na umesahau kumrudishia shukrani.
Kama uliweka nadhiri ya kusaidia ujenzi wa Kanisa mahali ambapo ulipokea muujiza fanya hivyo. Kwa maana wengine hupata muujiza wao sehemu fulani na kwenda kutoa shukrani kanisani kwao walikozoea kusali.
Mwenyenzi Mungu atujalie hekima ya kumshukuru yeye kwa kila jambo!
Mungu awabariki!

 

Friday, November 23, 2012

You hold me now!

No weeping, no hurt or pain, no suffering.... Thank you Jesus for loving me. I will forever be thankful to you.

 

Monday, November 19, 2012

Ujumbe wa Leo

“Angalia, siku zinakuja, asema Bwana Mungu, ambazo nitaleta njaa katika nchi, si njaa ya kukosa chakula, wala kiu ya kukosa maji, bali ya kukosa kuyasikia maneno ya Bwana.” Amosi 8:11
Tumia wakati wako vizuri kumtafakari Mungu na ukuu wake wa ajabu. Kama maandiko yanavyosema hapo juu, kuna wakati utatafuta walau mtu wa kukufundisha neno la Mungu hautapata. Kuna wakati utahitaji huduma za kiroho toka kwa watumishi mbali mbali hautaupata. Tusingojee wakati huo ufike ambapo tutalia na kusaga meno kwa kiu ya kutaka kuskia neno la Mungu. Mtumikie Bwana na tafakari maandiko yake matakatifu nawe utaona raha ya kuishi kwa kumtegemea yeye.
Muwe na Siku njema!

Saturday, November 17, 2012

UPENDO


1 Yohana 4:16"Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake".
Upendo wa Mungu wetu ni mkuu sana na unapita vitu vingi mno. Hata mtu akianza kuandika leo hii juu ya Upendo wa Mungu wino utakwisha kwa maana ni mkubwa mno hauelezeki. Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa mwana wake wa pekee Yesu Kristo ili kila amwaminie yeye asipotee bali awe na uzima wa milele. Yesu alitufia msalabani kwa ajili ya dhambi zetu, hii inadhihirisha jinsi gani Mungu amempenda mwanae huyo wa pekee afe kwa ajili ya mimi na wewe.
Upendo huleta amani, furaha na faraja. Ndani ya moyo wangu nina amani tele na furaha. Nampenda Kristo kwa sababu ameniokoa kwa damu ya thamani. “Utanijulisha njia ya uzima; mbele za uso wako ziko furaha tele; na katika mkono wako wa kuume mna mema ya milele,” Zaburi 16:11
Upendo hutoka kwa Mungu na kila mwenye upendo ni mtoto wa Mungu. “Twampenda yeye kwa sababu yeye alitupenda kwanza na akaichukua mioyo yetu kwake mwenyewe” 1 Yohana 4:19. Hakuna kitu muhimu katika maisha ya binadamu kama UPENDO. “Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabiri; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote. Upendo haupungui neno wakati wowote - 1Wakorintho 13:4-8
Mtu mwenye kukosa upendo huyo hayuko ndani ya Kristo na siku zote huwa na chuki. Hata katika Biblia imeonyeshwa kwamba mtu akisema anampenda Mungu ana anachukia ndugu yake ni muongo. “1Yohana 4:20 Mtu akisema, nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona”.
Si vyema kuchukiana juu ya mambo madogo madogo.Huna sababu ya kumchukia ndugu yako sababu ya wivu ama kumchukia jirani yako sababu ana maendeleo ambayo wewe huna. Hata amri ya pili inasema mpende jirani yako kama nafsi yako, sasa iweje unamchukia jirani ama ndugu yako wa kuzaliwa naye. Hii haimpendezi Mungu na yakupasa kumrudia yeye na kujifunza neno lake ndipo utaelewa maana halisi ya upendo.  Tuzishike amri za Mungu na kukaa katika pendo lake.
Upendo haujalishi umpendaye ni tajiri ama maskini. Kuna watu ambao huchagua watu wa kuwapenda yaani ambao wanaona wako kwenye status zao. Huo sio upendo bali ni kutafuta watu ambao unadhani utapata furaha kwa sababu tu pengine anaendesha benzi, anakula sehemu za bei ya juu, anavaa vitu vya bei na vitu vingine vinavyofanana na hivyo.
Tuwe na upendo wapendwa kwa sababu ukiwa na upendo siku zote utakua na amani. Kwa maana mtu mwneye Upendo hulipa mabaya kwa mazuri, kamwe hawi wenye visasi. Mwenye upendo siku zote ni mnyenyekevu mbele za watu na hujali wengine zaidi yake mwenyewe.
Usiruhusu mwanadamu akurudishe nyuma na ukatoka katika pendo. Binafsi tangu niijue Biblia maisha yangu yamekuwa ya furaha sana na amani. Na ndiyo maana nasema maisha yangu ni biblia yangu mahali ambapo napata faraja kila nisomapo. Through biblia nimejifunza nini maana halisi ya upendo, na mambo mengine mazuri.
Tujitunze katika upendo wa Mungu, huku tukingojea rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo kwa kutazamia uzima wa milele. Na haya yote yanapatikana kwa kumuomba roho mtakatifu akuongoze uwe na upendo.
Mimi nawapenda, muwe na Jumapili njema.

Thursday, November 15, 2012

Ujumbe wa leo


"Msitende neno lolote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine. Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu" Wafilipi 2:3-5
Mungu anakupenda ndiyo maana unaishi mpaka leo hii. Mungu wetu hapendezwi na majivuno wala kiburi hupendezwa na wale wenye unyenyekevu. Mungu anatuasa kuacha majivuno na kujiona ni bora kuliko mtu mwingine. Pia anasema tuache kushindana kwa lolote hususan yale tunayoshindania hayana baraka kwake wala hayajengi. Ubinafsi usichukue nafasi ndani ya mioyo yetu, hii itasababisha kututenga mbali na Mungu kwa maana mtu binafsi na mwenye kufanana na mambo kama hayo huhesabiwa maovu na baba yetu wa mbinguni.
Mbarikiwe!

Wednesday, November 14, 2012

Zaburi ya Leo

Zaburi 119: 41-48 "Ee Bwana, fadhili zako zinifikie na mimi, naam wokovu wako sawasawa na ahadi yako. Nami nitamjibu neno anilaumuye, kwa maana nalitumainia neno lako. Usiliondoe neno la kweli kinywani mwangu kamwe, maana nimezingojea hukumu zako. Nami nitaitii sheria yako daima, naam milele na milele. Nami nitakwenda panapo nafasi, kwa kuwa nimejifunza mausia yako. Nitazinena shuhuda zako mbele ya wafalme, wala sitaona aibu. Nami nitajifurahisha sana kwa maagizo yako ambayo nimeyapenda. Na mikono yangu nitayainulia maagizo yako niliyoyapenda, nami nitazitafakari amri zako".
Muombe Mungu akupe fadhili zake na udumu katika neno lake. Kwa maana ni neno lake pekee litatuokoa. Songa mbele usisikilize watu wasemayo na siku zote mwanadamu hakosi la kusema. Iwe ni juu ya mafanikio yako ama jambo lolote bado kutakuwa na neno juu yake. Mtumainie Mungu na umuombe sana asiliondoe neno lake kinywani mwako. Zitafakari na kuzifuata amri zake hakika utaona uzuri wa kuishi kwa kumtegemea Mungu.

Mbarikiwe sana!