Sunday, November 25, 2012

JE UNAKUMBUKA KUSHUKURU BAADA YA KUPATA?


Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya bwana, dunia na wote wakao ndani yake (Zaburi 24:1). Mwenyenzi Mungu ametukabidhi mamlaka ya kumiliki vitu vyote vilivyopo duniani, hivyo hatuna budi kumshukuru na kumrudishia yeye sifa.
Mara nyingi watu wanapopata walichoomba kwa Mungu kisha wanasahau kusema asante. Na pengine huweka ahadi kwa Mungu kwamba endapo watajibiwa haja zao basi watatoa kitu fulani ama watafanya jambo fulani kama shukrani kwa Mungu.
Kama ulimuomba Mungu akutimizie kitu chako ama tatizo lako pengine ni kupata mtoto halafu ukaahidi kumtolea sadaka ya pekee Mungu wako basi fanya kama ulivyoahidi pasipo kusahau.
Ahadi unayoweka kwa Mungu ni NADHIRI yako na endapo hujaitimiza Mungu anaihesabia kama dhambi na itakufwatilia maishani mpaka hapo utakapotimiza.
Lakini kuna wale wachache wanakumbuka kusema asante na kutoa shukrani zao pindi wapatapo miujiza yao. Mfano mzuri ni ile hadithi ya wenye ukoma kumi,walipopaza sauti na kuita Ee Yesu, Bwana mkubwa uturehemu. Yesu alipowaona akawaambia enendeni mkajionyeshe kwa makuhani na walipokuwa wakienda walitakasika. Na mmoja wao alipoona amepona alirudi akimtukuza Mungu kwa sauti kuu na kuanguka miguuni mwake akamshukuru. Mtu huyu ameshukuru kwa sababu ameuona ukuu wa Mungu, ameguswa kwa namna ya kipekee.(Luka 17:11-19).
Ni mangapi Mungu wetu anatutendea mambo makubwa na mara nyingine tunashangaa miujiza hiyo lakini tunasahau kumshukuru angalau hata kwa kupiga magoti na kusema asante Mungu.
Kama umeweka nadhiri ya kumtolea Mungu sadaka ya shukrani itimize. Labda niseme maana ya Nadhiri nijuavyo mimi ni sadaka uitoayo kwa kinywa chako mwenyewe. Tukumbuke kuwa mara nyingi Nadhiri hutolewa madhabahuni ambapo ni sehemu takatifu.
Madhabahu ni sehemu ambayo inatunza kumbukumbu kwa kila aliyetamka nadhiri yake.Sasa tujiulize tunapotoa nadhiri zetu bila kuzikamilisha hatuogopi madhabahu ama?
Nakumbuka mafundisho ya Mchungaji Christopher Mwakasege juu ya mfano wa wanandoa wawili waliokuwa wanatafuta mtoto kwa muda mrefu bila mafanikio. Wakawa wamezunguka kila sehemu zenye huduma za maombi. Siku moja wakaenda kusali kwa Mchungaji mmoja kimoyo moyo wakasema ‘Mungu ukitupa mtoto tunaahidi kutoa sadaka yetu kwa Mchungaji huyu na kusaidia kanisa lake. Baada ya muda Mungu akawajibu kwa kuwapatia mtoto. Wale wanandoa wakajisahau na kuendelea na maisha yao kama kawaida. Baada ya kipindi kidogo yule mtoto mdogo akaanza kuugua magonjwa mbali mbali hata madaktari wenyewe wasielewe. Ndipo wakamkumbuka Mungu na kuanza kusali.
Mchungaji Mwakasege alifunuliwa na Mungu ya kwamba watu hao walitoa nadhiri mahali fulani na hawajaitimiza, waulize watakuambia wenyewe. Alipowauliza ndipo walipokumbuka ya kwamba hawakutimiza ahadi yao. Wakatubu na kurudi kwenye Kanisa ambapo walipata muujiza na kutubu dhambi zao na kutoa nadhiri yao. Mungu akawasamehe na mtoto akapona.
Huu ni mfano ambao kwangu mimi ulinigusa kwa namna ya pekee. Sijui wewe mwenzangu Mungu amekutendea mangapi na umesahau kumrudishia shukrani.
Kama uliweka nadhiri ya kusaidia ujenzi wa Kanisa mahali ambapo ulipokea muujiza fanya hivyo. Kwa maana wengine hupata muujiza wao sehemu fulani na kwenda kutoa shukrani kanisani kwao walikozoea kusali.
Mwenyenzi Mungu atujalie hekima ya kumshukuru yeye kwa kila jambo!
Mungu awabariki!

 

2 comments:

  1. amen nimebarikiwa pia lakini ninamaswali ni wapi mtu ana takiwa atoe nadhiri yake.either ni lazima iwe madhabahuni au waweza saidia mtu asiye jiweza au .

    ReplyDelete
    Replies
    1. Ndiyo unaweza saidia mtu asiyejiweza kama nadhiri yako. Lakini hiyo inatokea pale ambapo ulisema ukipata kitu ama pesa kiasi fulani umepanga kutoa msaada kwa mtu asiyejiweza, hivyo huna budi kuhakikisha unatimiza ahadi hiyo. Ubarikiwe

      Delete