Wednesday, October 10, 2012

Utajuaje Umesamehe/samehewa


Utajua kuwa jeraha limepona kwa mfano mara ya kwanza ulikuwa ukimuona ama ukikutana na mtu aliyekukosea mwili unasisimka na unapandwa na hasira ukitamani ubadilishe njia ama umralue mtu huyo. Lakini ukiongea nae na kusameheana pindi mkikutana sehemu ama mkionana moyo wako unakuwa una amani na furaha na mnaongea kawaida, hapo utajua kuwa umepona jeraha lako. Kipimo kingine cha kujua umemsamehe/ samehewa na mtu uliyekosana nae ni kwamba je maongezi yenu yanaweza kudumu angalau kwa nusu saa mnaongea na kucheka? Kama hilo haliwezekani basi jua hujasamehe ama huyu mtu mwingine hajakusamehe.
Mara nyingine kuna watu wa aina ya kusameheana na mara wanajikuta wanagombana mara kwa mara. Katika hali kama hiyo endapo wewe umegundua mwenye shida ni mwenzako na umechoka na hiyo hali ya kukoseana na kusameheana kila wakati basi yakupasa umuombe Mungu akupe ujasiri wa kusonga mbele.
Kwanza inabidi ujiulize kwa mfano je nikiacha kujishughulisha na huyu rafiki yangu ni mangapi napungukiwa? Wakati tukiwa hatupo pamoja ni mangapi nafanya na kufanikiwa? Na wakati tukiwa hatupo pamoja ni mambo mangapi hayaendi sawa? Jiulize nitakosa nini kama nitaamua kutojishughulisha nae tena? Lakini hii haina maana kuwa usisalimiane nae, la hasha unamwambia ukweli kwamba umechoka na maisha ya namna hiyo cha muhimu kila mtu aendelee na maisha yake lakini bado tutabaki kuwa marafiki na kusaidiana kwenye shida na raha. Binafsi mimi huu ni ushauri wangu na nimeona ukifanya kazi kwa baadhi ya watu wa namna hiyo. Cha muhimu moyo wako uwe umesamehe kweli na una amani kabisa ndani ya moyo wako.
Pengine umekosana na ndugu yako wa damu na ili hali unajiita mkristo kila siku unahudhuria Kanisani na unamtolea Mungu sadaka. Lakini kama ndani ya moyo wako unajua wewe umemkosea ndugu yako hata kama unamcha Mungu kiasi gani unahitaji neema ya kukuongoza kuombana msamaha na ndugu yako kwa sababu sadaka yako haipokelewi.
Maandiko yanatuambia “Basi ukileta  sadaka yako madhabahuni na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako iache sadaka yako mbele ya madhabahu uende zako, upatane kwanza na ndugu yako kasha urudi uitoe sadaka yako” Mathayo 5: 23-24
Mind you, sio kitu kinatokea kwa siku moja, la hasha ni hatua ya muda na inayohitaji roho mtakatifu akuongoze. Muombe Mungu akupe neema ya Msamaha na neema ya kudumu ndani ya moyo wako.
Kwa hiyo tunahitaji kuongozwa sana na roho mtakatifu katika kutoa msamaha na kujisamehe wenyewe pia.

No comments:

Post a Comment