Friday, October 19, 2012

UJUMBE WA LEO


“Amka Amka jivike nguvu zako Ee Sayuni; jivike Mavazi yako mazuri, Ee Yerusalemu, mji mtakatifu kwa maana tokea sasa hataingia ndani yako asiyetahiriwa wala aliye najisi, jikung’ute mavumbi uondoke, uketi ee Yerusalem. Jifungulie vifungo vya shingo yako Ee Binti Sayuni uliyefungwa” Isaya 52:1-2

MAANA YAKE: Unapoamua kufuata mwelekeo mpya wa maisha unatakiwa kuwa tayari kuacha mambo ya zamani yanayokuzuia. Kwa maana umepewa tohara ya moyo kwa kuokolewa. Kama wewe ni mfanyabiashara uachane na vitu ambavyo vinakurudisha nyuma na kukukwamisha.Kama maisha yako yalikuwa ya starehe kabla ya biashara, basi yakupasa kufikiria zaid jinsi ya kupunguza matumizi yako katika starehe pindi umekuwa na biashara yako na unataka maendeleo. Think out of the box kwamba nini kitafanya biashara yako ikue. Pengine ulikuwa mtu wa kusema watu, mchonganishi kama umeamua kumfuata Yesu achana na hivyo vitu na jitenge kabisa na watu wanaopenda mambo kama hayo. Jikung'ute nguo zako na usonge mbele. Usijali watu watakuonaje ama kukusemaje, mfuate Mungu pekee ndo rafiki wa kweli.
Mimi nimeonja utamu wa Yesu sijui wewe ndugu yangu...

Thursday, October 18, 2012

NENO LA LEO


“Ndugu sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika ila natenda neno moja tu nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachumilia yaliyo mbele” Wafilipi 3:13

Pengine unajiskia mnyonge na kujilaumu kutokana na mambo uliyoyafanya wakati uliopita na vile vile haupo pale ambapo Mungu anataka uwepo. Mungu anajua kila chaguo baya la mtu, anajua magumu unayopitia, kila baya ulilotenda na hakika amekuandalia mpango wa kukurudisha kwake. Usikate tamaa kwa maana kushindwa sio mwisho wa kila kitu, Mungu pekee ndiyo mwenye kuamua katika mambo yote. Makosa uliyoyafanya yasiwe sababu ya kukukosesha kuwa karibu na Mungu. Pengine leo hii uko kwenye uhusiano ambao huoni mwanga mbele yako ama una matatizo ya kifedha na magonjwa yanakuandama, Mungu pekee ndiye atakayekuokoa. Endelea kumtumaini na kumwamini yeye hakika atakuinua na kukupitisha kwenye vizingiti ambavyo hukudhani kama utaweza kupita. Mungu amemuandalia kila mtu destination yake, so never lose hope.
I love this song, such moving words it carries!
 

Sunday, October 14, 2012

UMUHIMU WA KAZI KATIKA KUFANIKIWA


Katika Biblia kazi imeonekana kwa sehemu kubwa na hii inaonyesha umuhimu wake jinsi ulivyo. Ni dhahiri kila mmoja wetu anajua umuhimu wa kazi katika maisha ya kila siku ya mwanadamu. Biblia inaonyesha pia ni kwa namna gani mtu ambaye hafanyi kazi atakavyoishi.

Kitabu cha Waraka wa Pili wa Paulo Mtume kwa Wathesalonike kinaonyesha wazi kabisa kuwa asiyefanya kazi na asile. Mtu kama huyo asiwe mzigo kwa wengine kutokana na uvivu wake.

“Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi asile chakula” 2Wathesalonike 3:10

Katika yote haya muda ni muhimu sana kwenye kazi. Pasipo kuzingatia muda basi mtu atajikuta hapati maendeleo kwa sababu hajawekea maanani kipengele cha muda. Wapo watu ambao wanafanya kazi bila kujiwekea malengo fulani ya kufikia kwa wakati muafaka walioweka. Nasema hivi kutokana na kwamba utakuta mtu anafanya kazi ili mradi atimize wajibu wa kuingia ofisini asubuhi na kumaliza jioni. Tena mwingine anaweza kukuambia anasubiria kwa hamu muda wa jioni ufike atoke kazini ama sehemu yoyote ya kibarua afanyacho ili hali siku hiyo hajavuna chochote na muda umeenda.

Ni vyema kujiwekea malengo mazuri katika kazi kwa sababu pia sio kila anaefanya kazi ana mafanikio. Mtu mwingine utakuta anafanya kazi zaidi ya moja lakini haoni mafanikio yake, hii ni kwa sababu hajajiwekea malengo katika kazi yake. Yaani kwa mfano mtu anaweza kusema anafanya kazi ya kufundisha kwa muda wa miaka kumi ama zaidi na  katika kazi hiyo atasave kiasi cha dola kumi ama zaidi ama elfu ishirini kwa kila malipo atakayopata. Na kiasi hicho atakachohifadhi  kitamsaidia kuendeleza shughuli nyingine za kumletea maendeleo.

Kipengele cha muda ni muhimu sana katika kuleta maendeleo. Hata katika Biblia inatuonyesha jinsi Mungu alivyofanya kazi yake na kumaliza kwa wakati.  “Na siku ya Saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya, akastarehe siku ya Saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya” Mwanzo 2:2

Sasa kama mtu atakuwa mvivu na muda unazidi kusonga mbele ni hakika maisha yake yatakuwa ya kuhangaika. Muda ukisogea mbele kamwe haurudi na umri wako unazidi kuongezeka. Swali la kujiuliza ni kwamba  je, muda wako unautumia vizuri? Pengine una wazo la biashara ya aina fulani unataka kuianza na unaona ni vyema kumshirikisha rafiki yako akushauri, na labda atakubali kukushauri na katika ushauri huo itawekwa mbegu ya LAKINI!!! Kwa maana kwamba lakini biashara hiyo unayotaka kufanya haina faida kabisa, tena hasara ni kubwa kuliko faida. Basi kama wewe ni mtu ambaye unapenda kusikia vitu positive tu ni hakika utakwama katika kuanzisha biashara hiyo. Na kila saa maneno ya kukukatisha tamaa ndio yatakujia kila mara na hapo unajikuta unashindwa kutimiza ndoto yako. Cha ajabu utashangaa mtu Yule yule aliyekushauri kutoanzisha hiyo biashara yeye ndo anaifanya, matokeo yake unabaki kulalamika huku muda unazidi kwenda. Tangu una miaka 25 unawaza kufungua kampuni yako ya ukandarasi mpaka unafika miaka 40 bado unaendelea na ndoto yako bila kuamua kuchukua hatua.

Ni muhimu kuelewa kuwa sio kila ndoto yako itakubaliwa na watu, la hasha lazima kuna kupingwa hata na watu wako wa karibu. Kama unaifahamu huduma yako ni muhimu kuifanyia kazi pengine wewe ni fundi muwashi, mwanamuziki ama mpishi jibiidishe katika huduma yako na Mungu atakubariki.

Vifungu vingine vya kusoma kuhusu kazi ni “KUTOKA 5: 9, 13, 1WAKORINTHO 3:12

MAHUSIANO NI KAZI KATIKA FAMILIA

Kuwa na mahusiano mazuri na watu wa familia yako nayo ni sehemu muhimu ya kazi. Kuna watu tangu waanze kufanya kazi zao pengine ni mwaka wa tano hawajawahi kuwasaidia ndugu wanaowazunguka.

Ni vyema kuwasaidia ndugu ambao unadhani wanahitaji msaada nawe utabarikiwa katika kazi yako. Na sio ndugu tu, bali kuna watu wenye shida mbali mbali nao wanahitaji msaada. Naomba pia nieleweke sio tu watu wanaohitaji msaada, wazazi ni sehemu kubwa ya baraka haijalishi wanahitaji msaada ama la cha muhimu ni kwamba unawasaidiaje wazazi wako. Ni baraka kuwakumbuka wazazi au walezi wetu kwa zawadi yeyote. Wanaweza wakawa wamejitosheleza kiuwezo na hawaihitaji msaada lakini zawadi utakayowapa wataifurahia na kukuombea baraka katika kazi na maisha yako.  Hata kama ni matajiri kiasi gani, chochote utoacho kwao wataona unawajali nawe utazipata nyingi baraka.

Kuna watu wanafanya kazi na wanapata pesa ya kutosha lakini haidumu mikononi mwao wanabaki kujiuliza. Ni dhahiri kabisa mtu huwezi pata maendeleo ya kazi yako kama huwasaidii wale wahitaji hususan wazazi wako ama walezi.

“Lakini mtu yeyote asiyewatunza walio wake yaani wale wa nyumbani mwake, hasa ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini,” 1Timotheo 5:8

Ni vyema ukakaa na kujiuliza hasa watu ambao wako mbali na familia zao, ni kwa muda gani umewakumbuka ndugu zao wa mbali na kuwasaidia.
Jumapili Njema!
 

 

Wednesday, October 10, 2012

Utajuaje Umesamehe/samehewa


Utajua kuwa jeraha limepona kwa mfano mara ya kwanza ulikuwa ukimuona ama ukikutana na mtu aliyekukosea mwili unasisimka na unapandwa na hasira ukitamani ubadilishe njia ama umralue mtu huyo. Lakini ukiongea nae na kusameheana pindi mkikutana sehemu ama mkionana moyo wako unakuwa una amani na furaha na mnaongea kawaida, hapo utajua kuwa umepona jeraha lako. Kipimo kingine cha kujua umemsamehe/ samehewa na mtu uliyekosana nae ni kwamba je maongezi yenu yanaweza kudumu angalau kwa nusu saa mnaongea na kucheka? Kama hilo haliwezekani basi jua hujasamehe ama huyu mtu mwingine hajakusamehe.
Mara nyingine kuna watu wa aina ya kusameheana na mara wanajikuta wanagombana mara kwa mara. Katika hali kama hiyo endapo wewe umegundua mwenye shida ni mwenzako na umechoka na hiyo hali ya kukoseana na kusameheana kila wakati basi yakupasa umuombe Mungu akupe ujasiri wa kusonga mbele.
Kwanza inabidi ujiulize kwa mfano je nikiacha kujishughulisha na huyu rafiki yangu ni mangapi napungukiwa? Wakati tukiwa hatupo pamoja ni mangapi nafanya na kufanikiwa? Na wakati tukiwa hatupo pamoja ni mambo mangapi hayaendi sawa? Jiulize nitakosa nini kama nitaamua kutojishughulisha nae tena? Lakini hii haina maana kuwa usisalimiane nae, la hasha unamwambia ukweli kwamba umechoka na maisha ya namna hiyo cha muhimu kila mtu aendelee na maisha yake lakini bado tutabaki kuwa marafiki na kusaidiana kwenye shida na raha. Binafsi mimi huu ni ushauri wangu na nimeona ukifanya kazi kwa baadhi ya watu wa namna hiyo. Cha muhimu moyo wako uwe umesamehe kweli na una amani kabisa ndani ya moyo wako.
Pengine umekosana na ndugu yako wa damu na ili hali unajiita mkristo kila siku unahudhuria Kanisani na unamtolea Mungu sadaka. Lakini kama ndani ya moyo wako unajua wewe umemkosea ndugu yako hata kama unamcha Mungu kiasi gani unahitaji neema ya kukuongoza kuombana msamaha na ndugu yako kwa sababu sadaka yako haipokelewi.
Maandiko yanatuambia “Basi ukileta  sadaka yako madhabahuni na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako iache sadaka yako mbele ya madhabahu uende zako, upatane kwanza na ndugu yako kasha urudi uitoe sadaka yako” Mathayo 5: 23-24
Mind you, sio kitu kinatokea kwa siku moja, la hasha ni hatua ya muda na inayohitaji roho mtakatifu akuongoze. Muombe Mungu akupe neema ya Msamaha na neema ya kudumu ndani ya moyo wako.
Kwa hiyo tunahitaji kuongozwa sana na roho mtakatifu katika kutoa msamaha na kujisamehe wenyewe pia.