Kila mmoja wetu anapenda kuishi
maisha ya uadilifu na ya kuheshimika kwa jamii nzima inayomzunguka.
Tunapoteleza kimaadili kwa bahati mbaya au makusudi bado tungependelea heshima
yetu kwa jamii ibaki pale pale. Mwenyenzi Mungu ametubariki wanadamu kuwa na
hekima na busara katika kufanya maamuzi ambayo yanasaidia kulinda heshima yetu.
Ni vizuri kurekebishana kwa heshima pale tunapoona mmoja wetu anapotoka
kimaadili ili heshima yake katika jamii ibakie vile vile au kuongezeka zaidi.
Inaeleweka katika jamii wanadamu tunaweza kutofautina kimsimamo au kimaamuzi
ila tujitahidi isifikie katika hatua ya kuondoleana heshima mbele ya jamii.
Haimpendezi Mungu kabisa kuona kwamba mwanadamu anachangia kumwondolea
mwanadamu mwenzake heshima yake katika jamii.
Mfano mzuri wa somo la leo
tunaupata kutoka katika kitabu cha Mwanzo 9: 20-27
- “Nuhu akaanza kuwa mkulima, akapanda mizabibu; akanywa diva; akalewa; akawa
uchi katika hema yake. Hamu, baba wa Kaanani, akauona
uchi wa baba yake, akawaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje. Shemu na Yafethi wakatwaa vazi, wakalitanda
mabegani mwao wote wawili, wakaenda kinyumenyume, wakaufunika uchi wa baba yao,
na nyuso zao zilielekea nyuma, na wala hawakuona uchi wa baba yao. Nuhu
akalevuka katika ulevi wake, akajua mwana wake mdogo alivyomtendea. Akasema, Na
alaaniwe Kaanani; Atakuwa mtumwa kabisa kwa ndugu zake. Akasema, Na atukuzwe
BWANA Mungu wa Shemu; Na Kaanani awe mtumwa wake. Mungu akamnafisishe Yafethi.
Na akae katika hema za Shemu; Na Kaanani awe mtumwa wake.”
Hivyo basi wapendwa, kitabu hiki
cha Mwanzo kinatukumbusha ni jinsi gani mwanadamu anavyokwazika pale heshima
yake katika jamii inapoondoka. HESHIMA yako katika jamii ndio inayokupa msukumo
wa kufanya maamuzi ya busara na ya maendeleo kwako mwenyewe na kwa jamii nzima
inayokuzuguka na zaidi kuwa na uhusiano mzuri na baba yetu wa mbinguni. Heshima
hiyo ikiondoka, ni vigumu mno kufanya maazuri ya busara na mwisho uhusiano na
Mungu wetu unavunjika. Tujitahidi kuwaheshimu wenzetu na vile vile kuwasaidia
kurudisha heshima yao pale wanapopotoka bila kukusudia au kwa kukusudia. Hata
itakapofikia suluhisho limeshindikana katika maamuzi au misimamo, bado tuna
wajibu wa kutunziana heshima. Mwenyenzi Mungu aendelee kutubariki katika
kufanya maamuzi ya hekima na busara ili heshima yetu katika jamii iendelee
kuthaminika.
Mbarikiwe!